JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Maadhimisho ya Siku ya TEHAMA Ulimwenguni 17 Mei 2021


Maadhimisho ya Siku ya TEHAMA Ulimwenguni  17 Mei 2021

 

UJUMBE KUTOKA KWA DKT. JABIRI K. BAKARI, MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

KAULI MBIU: "KUHARAKISHA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA VIPINDI VYA CHANGAMOTO" 

Leo tarehe 17 Mei 2021, ni siku ya TEHAMA ulimwenguni, ambapo tunaadhimisha siku iliyosainiwa makubaliano ya Telegrafu na kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mawasiliano (ITU). Shirika hili liliundwa ili kuweza kusimamia mawasiliano ya kimataifa, kugawa masafa ya Kimataifa ya radio na satellite, pamoja na kuandaa viwango vya vifaa vya mawasiliano, ili kuwezesha upatikanaji wa mawasiliano na kuweza kuunganisha mawasiliano kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maboresho ya mifumo ya TEHAMA kwenye maeneo yasiyofikiwa na huduma za mawasiliano Duniani kote.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuharakisha Mabadiliko ya Kidijitali Katika Vipindi vya

Changamoto” kauli mbiu hii inafafanua jukumu halisi la mifumo ya mawasiliano na TEHAMA katika kujenga mifumo imara inayosaidia wakati wa maafa; pamoja na kuwezesha nchi wanachama wa ITU kuwasaidia katika kuokoa maisha na kuendelea na shughuli za kiuchumi.

Matumizi mazuri ya mifumo ya TEHAMA yamewezesha nchi mbalimbali kuweza kukabiliana na mabadiliko ya maisha wakati wa maafa kama vile ya COVID-19 na kuweza kuendelea kuendesha shughuli mbalimbali za biashara na uchumi kwa ujumla kwa njia ya mtandao.

TEHAMA ina nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuboresha maisha na kuleta maendeleo kwa wananchi hasa wale wa vijijini, kuwezesha wakulima kupata masoko ya bidhaa zao, pamoja na kupata huduma mbalimbali za jamii zinazowezesha kuinuwa uchumi kwa akina Mama, vijana na wananchi kwa ujumla.

Kauli mbiu ya mwaka huu inahimiza wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano, kujikita zaidi katika kutumia mifumo ya TEHAMA katika kuleta mabadiliko ya kidijitali ili kuweza kulifikia lengo na ajenda ya “Unganisha 2030”, ambapo mifumo ya mawasiliano pamoja na TEHAMA itawezesha na kuharakisha ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kila mwananchi.

Mfumo wa leseni wa Tanzania unaruhusu utoaji wa huduma za mawasiliano bila kujali aina ya teknolojia, au aina ya huduma hivyo basi imejikita zaidi katika kuchochea ubunifu katika utoaji wa huduma mbalimbali. Tumejifunza kutokana na changamoto ya COVID-19 kuwa watu waliowezeshwa kuwa na mawasiliano wanaweza kuwasiliana na kufanya kazi kwenye mtandao kutoka mahali popote duniani, wanaweza kupata taarifa na kujifunza nyenzo mbalimbali za kufanyia kazi na kuboresha biashara zao hata wakati wa majanga.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kufanya kazi na Wadau mbalimbali wa mawasiliano katika kukabiliana na mambo yote iwe ni changamoto au mafanikio katika kuleta mabadiliko ya kidijitali na kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafaidika na mafanikio yanayotokana na faida za mitandao katika kuelekea kwenye mapinduzi ya kidijitali.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inahimiza watoa huduma wote wa Sekta ya mawasiliano kuendelea kuwekeza kwenye  miundo mbinu ya TEHAMA na kutoa huduma mbalimbali za mifumo ili kuiwezesha nchi kuwa na miundombinu imara ya mawasilaino ambayo ndio kigezo muhimu katika kuelekea kwenye mabadiliko ya kidijitali. 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!