JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Menejimenti ya Masafa

Masafa ya Redio ni moja ya rasilimali adimu kwa nchi zenye thamani kubwa kiuchumi kwa kuzingatia matumizi yake katika mawasiliano ya simu (yanayohusisha simu za mezani na jongefu), utangazaji, jeshi na utafiti wa kisayansi sanjari na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi kama vile huduma za jamii, Utekelezaji wa sheria, elimu, huduma za afya, na usafirishaji.

Usimamizi wa masafa unajumuisha mchanganyiko wa utaratibu wa kiutawala, kisayansi, na kiufundi unaohitajika ili kuhakikisha matumizi yenye ufanisi wa masafa ya redio bila kusababisha muingiliano.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ina jukumu la kusimamia Mpangilio wa Masafa Kitaifa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

TCRA inatumia Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroni na Posta, Sura ya 306, ("EPOCA") na kanuni zake kama vile Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroni na Posta (Masafa) kutekeleza jukumu hili.

Sheria hii pamoja na kanuni zake zinaipa TCRA mamlaka ya kutenga, kugawa, kutoa, kusambaza, kurejesha, kusimamisha, kufuta au kurekebisha mgawanyo miongoni mwa watumiaji au wenye leseni za mawasiliano ya masafa ya redio au chaneli nyingine za masafa.

TCRA inasimamiaje Masafa ya Redio?

Katika kutekeleza majukumu yake, TCRA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) na mashirika mengine ya mawasiliano ya kikanda yakiwemo Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU), Shirikisho la Mawasiliano la Afrika Mashariki (EACO) na Umoja wa Mamlaka za Usimamizi wa Mawasiliano kwa nchi za Kusini mwa Afrika (CRASA) inasimamia masafa kupitia upangaji, ugawaji, utoaji leseni, ufuatiliaji na utekelezaji.

  • Upangiliaji na ugawaji wa Masafa

Upangiliaji na ugawaji wa masafa hufanywa kulingana na Kanuni za Redio za ITU. Mpangilio wa Matumizi ya masafa umebainishwa kwa kina katika Jedwali la Mpangilio wa Masafa Kitaifa (National Frequency Allocation Table )

  • Utoaji leseni

TCRA hutoa leseni za masafa ya redio kwa watumiaji wanaokidhi vigezo. Mchakato wa utoaji wa leseni hufanywa kwa njia ya kawaida au kwa ushindani kulingana na uhitaji na upatikanaji wa masafa.

Masafa yenye uhitaji mkubwa hutolewa kulingana na mwongozo wa TCRA katika wakati husika. Hivi karibuni, masafa yenye uhitaji mkubwa kwa njia ya Mnada wa Masafa. Taarifa za kina za mnada huo zinapatikana hapa.

Masafa ambayo hupatikana kwa utaratibu wa  ‘aliyewahi kufika, ahudumiwe kwanza’ unaweza kupatikana kwa kutumia mfumo wa Tanzanite portal.

  • Ufuatiliaji na Utekelezaji.

TCRA hutumia vifaa na mbinu za kitaalaamu kugundua mawimbi ya redio au mawasiliano katika bendi tofauti za masafa ya redio. Zoezi hili hutekelezwa sambamba na tathmini ya mgawanyo wa chaneli za masafa, kukagua  bendi za masafa na umiliki wa chaneli za masafa, kugundua muingiliano wa masafa ya redio, kuzingatia eneo na kubainisha transmeta zisizo halali, ili kuhakikisha matumizi yenye tija ya masafa.

Uratibu wa matumizi ya masafa ya redio kimataifa, kikanda na kanda ndogo.

Masafa ya redio hayatambui mipaka ya kijiografia; hivyo yanapaswa kusimamiwa kwa ushirikiano na nchi nyingine.

TCRA hufanya uratibu wa pande mbili au zaidi na nchi zilizo jirani ili kuhakikisha hakuna muingiliano wa utendaji kazi wa mifumo iliyopo na ijayo ya ardhini katika nchi jirani kwenye maeneo ya mipaka.

Kwa huduma za satelaiti, uratibu wa masafa hufanywa na Shirika la Mawasiliano Duniani-ITU. ITU huratibu utaratibu wa utoaji wa masafa kama ilivyoainishwa katika Kanuni za ITU za Masafa ya Redio kuhusu matumizi yenye ufanisi ya masafa na obiti kwa nchi wanachama.

Ili kampuni iweze kuendesha mtandao wa satelaiti nchini Tanzania, lazima iombe nafasi katika mzunguko wa satelaiti kutoka ITU kupitia TCRA. Ili mtandao wa satelaiti upate ulinzi wa kisheria chini ya Kanuni za Redio za ITU, kampuni lazima isajiliwe kwenye Rejesta Kuu ya Kimataifa ya Masafa (MIFR) kupitia utaratibu unaohusika wa ITU.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!