MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA TEHAMA KWA WASICHANA - 2021
KUTOKA KWA, DKT. JABIRI K.BAKARI MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
KAULI MBIU: “MAWASILIANO KWA WASICHANA, KUWEZESHA MAISHA BORA YA BAADAE”
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na nchi zingine duniani ambao ni wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU) katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya TEHAMA kwa Wasichana. Siku hii inaadhimishwa kila Alhamisi ya nne ya mwezi Aprili, ambapo kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 22 Aprili, 2021 na ikiwa inafikisha miaka 10, kwa Kauli mbiu “Mawasiliano kwa Wasichana, Kuwezesha Maisha Bora ya Baadae”
ITU ni shirika la Umoja wa Mataifa lililoundwa ili kusimamia mawasiliano kwa ujumla pamoja na mgawanyo wa masafa na kusimamia viwango vya vifaa vya mawasiliano na kuhakikisha kuwa mawasiliano (TEHAMA) yanawafikia wananchi wote duniani bila kujali eneo la kijografia, Jinsia au hali ya kiuchumi.Tunapoadhimisha siku hii, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikiandaa shughuli mbalimbali zinazoshirikisha wadau kutoka kwenye sekta mbalimbali na hasa wale wanaotumia mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kuwapa elimu na uelewa Wasichana, na kuwa hamasisha katika kupenda na kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu. Sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu, tunawajibika katika kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha Wasichana waweze kutumia TEHAMA vema katika shughuli mbalimbali za masomo, kiuchumi na kijamii ili iweze kuwa wekea msingi mzuri kwa maisha bora ya baadae. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania katika kutekeleza majukumu yake ya kimkakati inasaidia miradi mbalimbali inayochochea ufikishaji wa huduma za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vifaa vya TEHAMA mashuleni, zikiwemo shule mchanganyiko na zile za Wasichana na utoaji wa vifaa vya TEHAMA kwenye vituo vya TEHAMA vya jamii “Telecentres”. Mamlaka ya Mawasiliano pia inaendesha programu za ushindani ambapo Wasichana hupewa kipao mbele kushiriki. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania katika majukumu yake hutoa leseni kwa watoa huduma mbalimbali kwenye sekta ya mawasilianoili kuwezesha ufikishwaji wa mawasiliano katika sehemu mbalimbali nchini. Hii huwezesha vijana ikiwa ni pamoja na Wasichana kutumia mawasiliano ili kupunguza au kuondoa kabisa tabaka la upatikanaji wa huduma za TEHAMA na mawasiliano kwa ujumla. Natoa wito kwa Wasichana hasa walioko mashuleni waongeze bidii katika kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu; na kutumia vema TEHAMA kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi ili kujijengea msingi wa maisha bora ya baadae.




