Sumbawanga
Wadau mbalimbali mkoani Rukwa wamekutana katika mkutano maalum uliojadili changamoto ya utapeli wa kimtandao uliopo mkoani humo, huku wakitoa mapendekezo kadhaa yenye lengo la kudhibiti vitendo hivyo vinavyoleta athari kwa wananchi kiuchumi na kijamii.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na washiriki wa mkutano huo ni kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kukaa na makampuni ya watoa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti ili kuangalia namna bora ya kuimarisha zoezi la usajili wa laini za simu ambao ndio limekuwa chanzo kikubwa cha uwepo wa laini zinazotumika kwaajili ya utapeli mtandaoni.
Akifungua mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mheshimiwa Peter Lijualikali ameitaka TCRA kuongeza ufuatiliaji wa masuala ya utapeli wa kimtandao kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo hasa kwa mkoa wa Rukwa. Pia ameiasa jamii kujenga utamaduni wa kuuliza, kuhakiki na kuripoti matukio ya uhalifu kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua mahususi zichukuliwe haraka.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya sekta ya mwasiliano nchini inayoishia Juni 2026 inaonesha kuwa mkoa wa Rukwa na mataukio 2495 (sawa na asilimia 34 ya matukio yote nchi nzima) na mkoa Morogoro ukiwa una matukio ya ulaghai yaliyoripotiwa 2129 (sawa na asilimia 29 ya matukio yote nchi nzima). Kwa mkoa wa Rukwa wilaya inayoongoza kwa matukio ya utapeli ni Sumbawanga ikiwa na matukio 1,330, ikifuatiwa na wilaya ya Kalambo yenye matukio 612 na mwisho ni Nkasi yenye matukio yaliyoripotiwa 553.
“TCRA imekuwa ikitoa hizi taarifa za takwimu ili wadau wanaohusika na Masuala ya Uhalifu pamoja na watoa huduma waweze kutambua maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele na kuyafanyia kazi” Mkurugenzi Mkuu TCRA.
Wawakilishi kutoka kamati ya maadili ya mkoa wa Rukwa walipendekeza kuwepo kwa muda wa saa 24 kabla ya mtu kuruhusiwa kusajili laini nyingine ya simu huku pia wakilitaka Bunge kutunga sheria itakayoweka wazi adhabu kwa watu wanaojihusisha na utapeli wa kimtandao.
Kwa upande wao viongozi wa dini walisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa jamii ili kuwa na vijana wanaojiepusha na shughuli zisizo halali huku wakiliomba jeshi la polisi pamoja na TCRA kuweka wazi taarifa za matapeli na kutoa mrejesho kwa wananchi wanaporipoti matukio ya utapeli. Walieleza kuwa upatikanaji wa taarifa za watapeli kwa wakati unaweza kusaidia kupunguza kasi ya vitendo hivyo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Meneja wa Ufuatiliaji na Utekelezaji TCRA Mhandisi Mwesiga Barongo alisema hatua zilizochukuliwa na TCRA katika kukabiliana na utapeli mtandaoni ni pamoja na kuweka utaratibu wa usajili wa laini kwa njia ya biometriki inayosaidia kumtambua mtu anayesajili laini ya simu, Kufungia namba ya simu, IMEI na kitambulisho cha taifa – kwa laini zinazobainika kuhusika na utapeli, kuweka Muda wa dakika 30 kabla ya usajili mwingine wa laini ya simu ili kudhibiti udanganyifu na pia kuwapa nafasi wale wenye nia njema ya kusajili laini kwa matumizi binafsi.
Hatua nyingine ni Kushirikiana na watoa huduma kuboresha taratibu za usajili wa laini za simu na kuendesha Kampeni za elimu kwa umma ili kuhamasisha jamii kuhusu kuripoti na kujilinda dhidi ya utapeli wa kimtandao.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi lilieleza kuwa ingawa sheria zipo, bado kuna umuhimu mkubwa wa kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya utapeli wa kimtandao, hii ikiwa ndiyo sababu ya kuendelea kutoa elimu kwa umma. Ilielezwa kuwa kuna takribani sheria tano zinazosimamia masuala ya mawasiliano na uhalifu wa kimtandao nchini, na kwamba kwa kushirikiana, jamii inaweza kutokomeza tatizo hili.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Rukwa SACP Shadrck Masija aliwataka wananchi kuripoti mara moja endapo watapoteza mali zao, ikiwemo laini za simu na simu, ili kujiepusha na usumbufu endapo vifaa hivyo vitaingia mikononi mwa matapeli. Amehimiza wananchi kuepuka kununua simu kutoka kwa watu wasiojulikana bila kujiridhisha chanzo cha simu hiyo, kwani inaweza kuwa imetumika kutekeleza uhalifu — jambo linaloweza kuwaingiza wananchi wasio na hatia katika matatizo ya kisheria.
Jeshi hilo pia lilieleza umuhimu wa kuwajengea uwezo viongozi wa kata na serikali za mitaa ili kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utapeli, ikiwemo umuhimu wa kutoa ushahidi mahakamani, jambo ambalo baadhi ya wananchi bado wanaliogopa licha ya umuhimu wake.
"Tushirikiane kutoa taarifa za haraka pindi tunapobaini vitendo vya utapeli, na kuendelea kutoa elimu kwa umma" SACP Shadrack Masija.
Washiriki wa mkutano walisisitiza kuwa elimu kuhusu utapeli wa kimtandao inapaswa kuwafikia wananchi wote, hususan wale walioko vijijini, ili kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uelewa wa kutosha kujilinda dhidi ya vitendo hivyo vinavyoendelea kuathiri jamii kiuchumi na kijamii.




