JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tanzania Yashiriki Mkutano Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Duniani-2022


Tanzania Yashiriki Mkutano Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Du...

 

Bucharest. Tanzania imeshiriki Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Umoja wa Mawasiliano 2022 (ITU PP22) unaofanyika Bucharest nchini Romania kuanzia leo Jumatatu Septemba 26 Septemba hadi 14 Oktoba.

Katika mkutano huo, Tanzania imewakilishwa na ujumbe wa viongozi wa Sekta ya Tehama ambao wataongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye anatarajiwa kuwasilisha tamko la Kisera la Tanzania Septemba, 29 mwaka huu katika mkutano mkuu huo.

Akizungumza mapema kabla ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jim Yonazi amesema "Tanzania inalenga kuiweka Tanzania katika nyanja ya maendeleo ya Tehama duniani na kukuza ushawishi wake kama kitovu cha Tehama katika ukanda wa Kati na Kusini mwa Afrika ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayofanyika kila siku duniani kote" alisema Dk Yonazi.

Amesema Tanzania itautumia mkutano huo kuhakikisha inanufaika na mpango mkakati mpya wa ITU unaolenga kuleta  muunganisho wa mawasiliano kwa wote na mabadiliko endelevu ya kidijitali. Pia kushawishi na kuvutia miradi ya kimataifa, makampuni na washirika wa maendeleo katika Tehama ili kujenga uwezo na kukuza ubunifu wa vijana kutumia teknolojia zinazoibuka katika nchi yetu.

Mkutano Mkuu wa ITU 'Plenipotentiary' unawaleta pamoja wawakilishi wa  nchi wanachama 193 wa Umoja huo.  

Mkutano huu ambao ni chombo cha juu zaidi cha kutengeneza sera cha Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) hufanyika kila baada ya miaka minne, ni tukio muhimu ambalo nchi wanachama wa ITU huamua juu ya jukumu la baadaye la Umoja, na hivyo kuamua uwezo wa shirika kushawishi na kukuza maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) duniani kote.

Akiwakaribisha wajumbe kwenye Mkutano wa 21st Plenipotentiary huko Bucharest, Katibu Mkuu wa ITU alisema Mkutano huu utakuwa wa Kihistoria.

"Nchi wananchama zitaungana katika Mkutano Mkuu wa ITU “Plenipotentiary” 2022 ili kuweka mwelekeo wa mabadiliko ya kidijitali kwa miaka ijayo, kwa manufaa ya sayari yetu na ubinadamu." Katibu Mkuu wa ITU alisema katika taarifa yake.

Mkutano huo unaweka sera za jumla za Umoja huu, hupitisha mipango mikakati na fedha ya miaka minne na kuchagua Viongozi Waandamizi wa Umoja, nchi wanachama wa Baraza, na wajumbe wa Bodi ya Kanuni za Redio.

Katika Mkutano huu, Tanzania inagombea kuwa katika mjumbe katika Baraza la ITU kwa kipindi cha 2023 hadi 2026 ambapo kuna wagombea 17  wa nafasi 13 za Afrika katika Baraza.

MWISHO

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!