Mwanzo
Kuhusu
Huduma
Viunganishi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
Ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu

Wasifu

Dkt. Jabiri Kuwe Bakari
Dkt. Jabiri Kuwe Bakari
Mkurugenzi Mkuu

Jabiri Kuwe Bakari (PhD) ni msomi wa Kitanzania; tajiriba yake inagusa nyanja zote za kitaaluma na kiutendaji. Ni mtafiti, mkufunzi, mchambuzi na mshauri mwenye sifa na uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika Usimamizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Dkt. Bakari ana Shahada ya Uzamivu ya Falsafa katika Sayansi ya Kompyuta na Mifumo kutoka Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden (2007) alikopata ubobevu katika masuala ya Usimamizi wa Usalama na Vihatarishi vya TEHAMA; alipata Shahada ya Uzamili (Uhandisi) ya Mawasiliano ya Data kutoka Ndaki ya Uhandisi wa Elektroniki na Umeme ya Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza (1999), na Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Tanzania (1996).

Kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) nafasi aliyoipata kwa uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Aprili 2021. Aidha alihudumu kama Mtendaji Mkuu wa kwanza wa iliyokuwa Wakala wa Serikali Mtandao, tangu ilipoasisiwa mnamo Aprili 2012 hadi Januari 2020. Aliongoza ukuaji wa Wakala tangu kuanzishwa kwake hadi kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao, 2019, ambapo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wake wa kwanza hadi Aprili 2021 alipoteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA.

Katika kipindi chake kama Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, aliiongoza taasisi hiyo tangu ikiwa taasisi changa hadi kuwa taasisi yenye sifa nzuri, iliyoanzishwa na yenye mafanikio makubwa kutokana na kuendeleza mifumo na miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Umma (TEHAMA), kuboresha ushauri kwa Serikali kuhusu matumizi ya huduma za mtandao na mifumo-saidizi ya kiufundi na kuratibu mipango ya Serikali Mtandao kupitia utekelezaji wa Mifumo, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao. Dkt Bakari anafahamika kwa kusimamia falsafa yake ya "Kuimarisha Mifumo ya TEHAMA iliyoundwa ndani ili kutatua changamoto za TEHAMA na kujenga mifumo thabiti ya Serikali-mtandao".

Kabla ya kufanya kazi na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bakari alikuwa Mhadhiri Mwandamizi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Elimu (IET), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), 2007-2012 nafasi aliyotumikia baada ya miaka 10 ya kushika nafasi za kiufundi, usimamizi na uongozi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ikiwemo nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UCC), 1996-2007. Akiwa UCC, alihusika katika jukumu muhimu la kuleta mageuzi ya Kituo hicho hadi kuwa kampuni iliyoimarika mnamo mwaka 2000 wakati huu akihudumu katika nafasi ya Naibu Mkurugenzi Mkuu Nafasi aliyoitumikia hadi alipoenda kujiendeleza masomoni kwa Shahada ya Uzamivu mwaka 2003. Aliporejea, mwaka 2007, alirejeshwa kwenye Nafasi yake kama Naibu Mkurugenzi Mkuu, akisimamia Fedha, Utawala na Huduma za TEHAMA, UCC.

Akihudumu katika nafasi ya Mkurugenzi na Mhadhiri katika Taasisi ya Teknolojia ya Elimu (IET) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, alichangia mageuzi ya taasisi hiyo iliyoshuhudia kuanzishwa kwa Vituo vya Mafunzo ya TEHAMA vya chuo hiki kote nchini Tanzania hasa katika vituo vya mikoa. Aidha, akiwa Mratibu wa Kikanda wa taasisi ya Cisco na mhadhiri wa taasisi ya CISCO aliyeidhinishwa, alitoa mchango mkubwa katika kuanzisha kwa Taasisi ya Cisco Tanzania mwaka 2000. Aliongoza uanzishaji wa Mtandao wa Elimu na Utafiti Tanzania (TERNET) na alikuwa Katibu Mtendaji wake wa kwanza hadi 2012.

Kazi zake za Utafiti zimejikita kwenye tasnia ya TEHAMA zaidi katika eneo la Usimamizi wa Usalama wa mifumo ya TEHAMA, ambapo amechapisha na kuwasilisha taarifa kadha wa kadha kwenye mikutano ya kimataifa ya vyombo vinavyoshughulika na usimamizi na usalama wa mitandao kama vile Chama cha Usalama wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari (ISSA), Shirikisho la Kimataifa la Uchakataji wa Habari (IFIP) na kwenye mikutano ya kimataifa ya Taasisi ya Wahandisi wa Umeme na Elektroniki (IEEE).

Pamoja na haya, ni mjumbe mshiriki wa tawi la Tanzania la chama cha ukaguzi na uthibiti wa mifumo ya kompyuta na mawasiliano (ISACA) ambapo amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti kati ya 2011 na 2015. Vilevile, tangu 2017 hadi leo amekuwa Mkurugenzi aliyeidhinishwa na anajishughulisha kwenye Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania, yaani Institute of Directors in Tanzania (IoDT) kama mwezeshaji wa mipango ya wakurugenzi inayolenga kutumia TEHAMA katika undeshaji wa taasisi.  Dkt Jabiri pia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) tangu 2018.

Aidha, ni mwanachama hai wa Chama cha Ukaguzi na Udhibiti wa Mifumo ya Taarifa (ISACA), tawi la Tanzania, pia aliwahi kuhudumu nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti, 2011-2015. Pia ni Mkurugenzi aliyeidhinishwa na mwezeshaji wa muda wa programu za Ukurugenzi zinazoangazia Usimamizi wa TEHAMA katika Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT) akihudumku kwenye nafasi hiyo tangu 2017 hadi sasa. Pia anahudumu kama mjumbe wa Bodi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) tangu 2016, na Shirika la Reli Tanzania (TRC) tangu 2018.

© 2022 TCRA, Haki zote zimehifadhiwa.