Mwanzo
Kuhusu
Huduma
Viunganishi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wajumbe wa Bodi

Mhandisi Othman Sharif Khatib
Mhandisi Othman Sharif Khatib
Mwenyekiti wa Bodi

Mhandisi Othman Sharif Khatib ni Mtaalamu na Mhandisi wa Mawasiliano ya Simu mwenye uzoefu wa miaka mingi kwenye sekta ya mawasiliano na amekuwa kwenye utumishi wa umma katika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi zake. Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Septemba 2022.

Mhandisi Khatib ana shahada ya Uzamivu ya Sayansi katika Uhandisi wa Mawasiliano ya Simu kutoka Chuo Kikuu cha Hochschule für Vehrkehrswessen cha Dresden, Ujerumani. Amepata mafunzo mbalimbali ya mawasiliano ya simu, uongozi na usimamizi wa sekta ya mawasiliano kwenye vyuo mbalimbali vya kimataifa.

Amekuwa Naibu Mkurugenzi, Usimamizi wa Masafa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Meneja wa Ofisi ya TCRA Zanzibar, Mhandisi Mtendaji Mkuu kwenye lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania (TPTC) na baadae Shirika la Simu Tanzania (TTCL). Mhandisi Khatib alianza kazi Wizara ya Nchi, SMZ kama Mhandisi wa mitambo ya mawasiliano ya redio.   Alistaafu Desemba 2019 akiwa TCRA.

Mhandisi Khatib amekuwa mjumbe wa Bodi za taasisi mbalimbali zinazohitaji utaalamu, zikiwemo Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar (ZICTIA).

Bw. Khalfan S. Saleh
Bw. Khalfan S. Saleh
Kaimu Mwenyekiti

Bw. Khalfan S. Saleh ni Mtumishi wa Serikali katika Ofisi ya Rais. Ana Shahada ya Uzamili katika fani ya Mitandao ya Mawasiliano ya Kielekroniki (MSc Data Telecommunication Networks) kutoka Chuo Kikuu cha Salford, Uingereza. Amekuwa Serikalini kwa zaidi ya miaka 25 ambapo amepata fursa ya kufanyakazi katika Serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT). Nafasi alizowahi kushika ni pamoja na Balozi Mdogo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar na Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.

Bi. Vupe Ursula Ligate
Bi. Vupe Ursula Ligate
Mjumbe wa Bodi

Bi. Vupe Ursula Ligate ni wakili wa Mahakama Kuu. Ni mtaalamu na mzoefu wa kutatua migogoro kwa njia mbadala, zikiwemo usuluhisi. Ana shahada ya uzamili katika Masuala ya Jinsia na maendeleo (MA (Gender and Development) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza na Shahada ya Sheria (LLB) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amehudhuria mafunzo mafupi ndani  na nje ya nchi kama vile Uingereza, Marekani, Ufilipino, Malaysia, Singapore na  China. Alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa uliokuwa Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) kati ya Machi 2006 na Agosti 2018 ambapo pia alikuwa Mwekyekiti wa Bodi ya Uhariri ya Mfuko huo.

Amekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma kuanzia Agosti mwaka 2018 hadi sasa. Kutokana na wadhifa huo ni mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Mwenyekiti wa Bodi  ya Uhariri ya Mfuko huo. Vilevile amewahi kuwa Mkurugenzi wa Utetezi wa Kisheria wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA).

Dkt. Mzee Suleiman Mndewa
Dkt. Mzee Suleiman Mndewa
Mjumbe wa Bodi

Dkt.  Mndewa ana shahada ya Uzamivu ( Ph.D.) katika uhandisi wa vifaa na mifumo inayotumia mwanga kwa mawasiliano (Optoelectronic information engineering kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia cha  Huazhong, Wuhan – China; Shahada ya Uzamili ya Teknolojia ya Habari ( Information Technology) kutoka Chuo Kikuu cha Griffiths, Queensland, Australia; Shahada ya  Sayansi ( Electroniki) kutoka Chuo Kikuu cha Osmania Hyderabad, India) na Cheti cha juu (Full  Technicians Certificate) ya  Uhandisi wa Umeme kuoka Chuo cha Ufundi cha Karume, Zanzibar.

Hivi sasa ni Mkurugenzi wa  Mawasiliano, Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Usafirishaji, Zanzibar. Amekuwa mjumbe wa timu ya wataalamu wa Mkongo wa taifa wa mawasiliano (NICTBB kuanzia 2004. Nyadhifa nyingine alizoshika ni pamoja na Mkurugenzi wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Chuo Kikuu cha Dodoma; Mshauri wa masuala ya TEHAMA kwenye Serikali ya Tanzania na mjumbe na msimamizi wa timu ya kitaalamu kuhusu mtandao na miundombinu kwa ajili ya mradi wa serikali mtandao (e-government), Zanzibar.

Bw. Ndalahwa Habbi Gunze
Bw. Ndalahwa Habbi Gunze
Mjumbe wa Bodi

Bw. Ndalahwa Habbi Gunze, ni msimamizi wa sekta ya utangazaji na amekuwa mjumbe wa Bodi ya TCRA tangu Julai 2021.  Ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, chombo cha TCRA cha kusimamia watoa huduma za maudhui kuhakikisha kwamba wanazingatia masharti ya leseni zao na wanafuata sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kuhusiana na maudhui ya utangazaji.

Bwana Gunze, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa la Taifa tangu 2018, amejihusisha katika masuala ya usimamizi wa vyombo vya habari vya utangazaji kwa miaka 26 kuanzia mwaka 1995 alipoteuliwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC) hadi 2015 alipostaafu kutoka TCRA ambako alikuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Utangazaji; nafasi aliyokuwa nayo tangu 2003. Alisimamia kikamilifu mabadiliko ya msingi ya kiteknolojia ya mfumo wa utangazaji wa televisheni za mfumo wa ardhini kutoka analojia kwenda dijitali.

Ana Shahada za masuala ya Uhusiano wa Kimataifa na uandishi wa habari. Alianza kazi Idara ya Habari (MAELEZO) kama Afisa Habari Msaidizi na baadaye alijiunga na Kampuni ya Magazeti ya Serikali, yanayochapisha Daily News kama mwandishi na Mhariri Msaidizi. Mwaka 1985 aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, wakati huo akiwa Mhe. Joseph Sinde Warioba.

Dkt. George Mulamula
Dkt. George Mulamula
Mjumbe wa Bodi

Dkt. George Mulamula ni Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya Technovate Advisory Services (TAS), inayojihusisha na kuendeleza ubunifu na uvumbuzi wa kidijitali na mipango endelevu ya maendeleo ya kiuchumi kwa kushirikiana na mamlaka za Tawala za Mikoa kupitia matumizi ya nvenzo mbalimbali  za kidijitali.

Ni mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa mpango wa Atamizi ya Kuendeleza Shughuli za TEHAMA, unaojulikama kama DTBi, ambacho ni kifupisho cha Dar Teknohama (ICT) Business Incubator. Mpango huo, unaojihusisha na kuendeleza ujarisiamali, ubunifu na uvumbuzi, unasimamiwa na Tume ya Tanzania ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na ni mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki na ni atamizi pekee nchini. Ameshastaafu. Wakati akiwa DTBi  alisimamia mpango wa kutumia vyombo vidogo vya angani vinavyoendeshwa kutoka ardhini (drone) kwa shughuli za afya, kusambaza madawa na vifaa tiba muhimu katika eneo la Ziwa Victoria.  Vilevile alifanya kazi na TCRA katika kuhamasisha na kuendeleza ujasiriamali kwenye sekta ya kidijitali na mawasiliano ya simu na mitandao. Ameshawahi kuwa Mshauri Mwandamizi wa Serikali kwenye masuala ya ujasiriamali, ubunifu na uvumbuzi katika TEHAMA na mawasiliano ya simu na mitandao, mkazo mkubwa ukiwa katika kujenga mazingira na mfumo wezeshi ya shughuli hizo.

Kwa muda wa miaka minane, Dkt. Mulamula alikuwa Bingwa wa kwanza mwandamizi mwenye asili ya Afrika wa masuala ya kiufundi katika kushughulikia hakimiliki kwa kutumia vifaa vinavyojiendesha vyenyewe katika  Shirika la Hakimiliki Duniani (WIPO), lenye makao yake makuu Geneva, Uswisi. Alifanya kazi na serikali za nchi za Afrika Kusini mwa Sahara kwenye matumizi ya TEHAMA katika uvumbuzi na ubunifu wa hakimiliki. Vilevile, alikuwa chachu ya kukibadillisha Kituo cha Afrika cha Mafunzo ya Ngazi ya juu ya Mawasiliano ya Simu (AFRALTI) kilichoko Nairobi, Kenya kuwa kituo cha Mafunzo Bora cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano ya Simu (ITU).

© 2023 TCRA, Haki zote zimehifadhiwa.