JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015
Dkt. Fatuma Simba Ikuja
Dkt. Fatuma Simba Ikuja
Mjumbe wa Bodi

Dkt. Fatuma Simba Ikuja ni Mhadhiri na Mtafiti katika Idara ya Sayansi ya Kompyuta na Uhandisi, Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akiwa na uzoefu na utaalamu mkubwa, Ikuja hushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali na majukumu ya ushauri katika uga wake. Maeneo yake ya utafiti yanajumuisha mitandao ya mawasiliano ya kasi, Elimu kwa njia ya Mtandao, usalama wa mtandao na uhandisi wa programu za TEHAMA. Dkt. Ikuja pia huwafundisha wanafunzi wa shahada ya uzamili katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha (NM-AIST) kama kazi ya muda wa ziada, pia, anafundisha kozi za shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Dkt. Ikuja amesimamia wanafunzi mbalimbali wa shahada za uzamili na uzamivu katika safari zao za kitaaluma. Amehudumu kama mtahini wa ndani na nje kwa maandiko ya wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika UDSM na NM-AIST. Aidha, Dkt. Ikuja ni mjumbe wa Bodi ya Wahariri wa Jarida la Tanzania la Uhandisi na Teknolojia (TJET), https://journals.udsm.ac.tz/index.php/tjet. Utaalamu wake pia unatambuliwa kupitia jukumu lake kama mchambuzi wa maandiko ya kitaalamu yakiwemo ya mikutano ya IEEE Africon (2015, 2021) na IFIP WG 9.4.

Mwezi Novemba 2021, Dkt. Ikuja aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Elimu Mtandao (CVL) cha UDSM, ambacho kinawezesha utoaji elimu kwa njia ya mtandao unaowezeshwa na TEHAMA.  Pia alifanya kazi kama Mtaalamu wa Ushirikiano wa kisekta katika UDSM akihudumu kwa miaka mitano (2016-2021) katika mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Zaidi ya kujihusisha na masuala ya taaluma, Dkt. Ikuja anapendelea ubunifu na ujasiriamali. Anashiriki kikamilifu kama Mwalimu Mwelekezi katika Kituo cha Kuboresha na Kukuza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDICTI), ambacho kinahusika kukuza na kuunga mkono bunifu za wanafunzi na wahitimu wa chuo kikuu kuwawezesha kubadilisha mawazo yao kuwa biashara zinazochipukia. Zaidi ya hayo, Dkt. Ikuja anatoa mchango wake kikamilifu katika programu ya "SmartGirlz in ICT", inayoelimisha na kuwezesha wasichana wa shule za sekondari kujifunza masomo na kazi katika fani inayokua ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Programu hii inapata hamasa kutoka mradi wa "Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA" unaoratibiwa na Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (ITU) lililoko Geneva.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!