JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA na Miongo Sita ya Mapinduzi katika Sekta ya Utangazaji wa Redio Tanzania


TCRA na Miongo Sita ya Mapinduzi katika Sekta ya Utangazaji...

 

Kutokuwepo kwa huduma za utangazaji wa redio sio tu kunazuia kuendea kwa maarifa na taarifa miongoni mwa wanajamii; lakini pia kunakosesha wananchi fursa muhimu za kukuza uchumi wa nchi. Huduma za utangazaji wa Redio huongeza ufahamu na kujenga uwezo kwa wananchi kwa sababu huarifu na kuelimisha kwa haraka zaidi. Huduma za utangazaji wa redio pia, huokoa maisha, ni huduma inayopatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi ya yote huzileta jamii pamoja hivyo kudumisha umoja na mshikamano katika jamii mambo ambayo ni tunu katika kudumisha Amani na upendano katika jamii.

Vipindi mbalimbali kama vile Michezo, afya, Habari, elimu, burudani, matangazo ya huduma na bidhaa, taarifa za hali ya hewa, taarifa za masoko, kilimo, biashara, uvuvi, ufugaji, masuala ya uhamiaji nakadhalika huwawezesha wananchi kufahamu masuala mtambuka yenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya watu na nchi kila siku.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni chombo kilichoanzishwa kisheria kusimamia sekta za mawasiliano na utangazaji nchini Tanzania. Kilianzishwa chini yas sheria Na. 13 ya mwaka 2003 iliyounganisha Tume ya Mawasiliano Tanzania na Tume ya Utangazaji Tanzania. TCRA ilianza kazi rasmi 2003 na kuchukua majukumu ya tume hizo mbili zilizovunjwa kwa ukamilifu.

Majukumu ta TCRA ni pamoja na kuhimiza ipasavyo ufanisi wa ushindani na uchumi; kulinda maslahi ya walaji; kulinda uwezo wa fedha na ufanisi wa wagavi; kuhimiza upatikanaji wa huduma zilizosimamiwa kisheria kwa walaji wakiwemo wenye kipato cha chini na walaji wa vijijini na wapambizoni, kukuza mwamko, maarifa na uelewa wa jamii kuhusu sekta zinazosimamiwa ikiwemo kuzingatia haja ya kulinda na kuhifadhi mazingira, haki na wajibu wa walaji na wagavi wanaosimamiwa. TCRA pia inasimamia jinsi malalamiko na migogoro inavyoweza kupokewa na kutanzuliwa na majukumu, kazi na shughuli za Mamlaka.

Mwaka 2022 tarehe 13 Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Redio ambayo huadhimisha umuhimu wa teknolojia hii muhimu ya mawasiliano iliyowezesha Mamilioni ya raia kote ulimwenguni Tanzania ikiwemo kupata taarifa mbalimbali. Nchini Tanzania sekta ya Utangazaji ambayo husimamiwa na TCRA imeendelea kukua kwa kasi inayoleta Matumaini kwamba wananchi wengi zaidi wanaendelea kupata taarifa, kuelimika na kuburudika kupitia mawasiliano ya utangazaji wa redio.

Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani 2022 iliyoadhimishwa Kitaifa jijini Dar es salaam katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam TCRA imedhihirisha kwamba sekta ya utangazaji wa redio hasa redio-jamii imeendelea kukua kwa kiwango cha Matumaini. Hadi Desemba 2021 zaidi ya vituo 205 vya redio vilikuwa vimesajiliwa nchini Tanzania ikiwa ni Ongezeko la kiwango cha kuridhisha katika sekta hii muhimu.

Uimarishaji wa mfumo wa upatikanaji wa maudhui ya utangazaji na maudhui-mtandao

Huduma za utangazaji kupitia mifumo ya kawaida na ya mtandao zimepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 60 iliyopita. Sekta ya utangazaji mathalani imetanuka kutoka kituo kimoja cha utangazaji mwaka 1977 hadi kufikia zaidi ya vituo 210 mwaka 2021. Mathalani vituo vya Redio 99 vimesajiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano katika kipindi cha 2015-2021 na kuongeza idadi kutoka vituo vya redio 106 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 205 mwaka 2021.

 

Idadi ya Watoa Huduma za Utangazaji  2015 – 2021

Huduma/watoa huduma

2015

2016

2017

2018

2019

2020

2021

Radio

106

148

156

158

183

199

205

 

Kwa ujumla, mapinduzi ya kihistoria ya vyombo vya habari vya kielektroniki duniani yanabebwa kwa sehemu kubwa na uvumbuzi wa mawimbi ya redio uliowezeshwa na mteknolojia bwana Heinrich Hertz mwishoni mwa miaka ya 1880, uvumbuzi wake ambao umeboreshwa kwa nyakati tofauti, hadi sasa umeendelea kuwa wenye umuhimu mkubwa.

Redio kimekuwa chombo cha Habari cha kutumainiwa kwa Makundi yote ya jamii kwa sababu teknolojia yake ni rahisi na inayohamishika kwa urahisi hivyo huwezesha wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma zake. Pia, huduma za utangazaji wa redio ni nafuu zaidi kwa hadhira kuliko vyombo vingine vya Habari kama vile magazeti ya kuchapishwa au huduma za Habari kupitia majukwaa ya mtandaoni.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA bwana Semu Mwakyanjala katika mahojiano Maalum na Mwandishi wa Makala haya alisema wakati Tanganyika (Tanzania) inapokea Uhuru kutoka kwa Waingereza, taifa ambalo wakati huo lilikuwa na idadi ya watu milioni 9 palikuwa na kituo kimoja tu cha utangazaji cha redio. Vifaa vya redio vilirithiwa kutoka kwa serikali ya kikoloni ya Uingereza; hata hivyo mara baada ya Uhuru, Tanzania imekuza sekta ya utangazaji wa redio kutoka kituo kimoja cha utangazaji mwaka 1961 hadi kupindukia vituo vya utangazaji zaidi ya 200 vinavyofanya kazi kote nchini hivi sasa.

Nchini Tanzania, redio za jamii zinayo nafasi muhimu katika mfumo wa ikolojia ya Habari na utangazaji. Mathalani kuanzishwa kwa vituo vya utangazaji wa redio za jamii umesaidia sana kukuza maendeleo katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikiwemo kuwezesha ukuzaji na usambaaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi, kuwapa wananchi elimu ya afya, kutanua uelewa wa kilimo na ufugaji bora pamoja na manufaa mengine. Mathalani redio za jamii kama vile Orkonolei ORS ya Simanjiro mkoani Manyara imewezesha jamii inayohudumiwa kutanua uelewa na matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa utaratibu Maalum uliowekwa wakati wa uanzishwaji wake ili kuhudumia jamii ya eneo husika kwa lugha-mama kisha kupasisha matumizi ya Kiswahili kupitia lugha-mama za wakazi wa eneo hilo.

Aidha redio jamii zimewezesha wananchi wa maeneo husika kupata taarifa za mahali pamoja tofauti na matangazo ambayo wangeweza kupata kupitia vituo va utangazaji vya Kitaifa.

Mamlaka ya Mawasiliano inayo matarajio kwamba uwekezaji zaidi hasa katika kuanzishwa vituo vya redio-jamii utawezesha wananchi wengi zaidi kupata taarifa, burudani na kuelimika na kuwawezesha kutatua changamoto zao kwa kushirikiana na Viongozi katika maeneo yao. Matarajio ya ukuaji wa sekta ya utangazaji kwa siku za usoni ni makubwa ambapo TCRA imeendelea na mikakati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kikanda na Kimataifa kuona namna Tanzania itakavyowezesha upatikanaji wa teknolojia ya utangazaji wa redio kidijitali ili kuwezesha ukuaji zaidi wa sekta hii muhimu katika maendeleo ya nchi. Ujio wa redio-dijitali utasaidia kukuza sekta ya utangazaji nchini.

 

 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!