JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni taasisi ya Serikali inayosimamia sekta ya mawasiliano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. TCRA ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania namba 12 ya mwaka 2003 baada ya kuunganishwa Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) na Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC). TCRA inasimamia sekta ndogo za mawasiliano ya simu, intaneti, maudhui ya utangazaji (katika redio na televisheni) na huduma za posta.

Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) iliundwa mwaka 1993 ikiwa na jukumu la kusimamia mawasiliano na huduma za posta. Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC) ilianzishwa mwaka 1993 ikiwa na jukumu la kusimamia sekta ya utangazaji.

Kufuatia maendeleo ya teknolojia, ilionekana haja ya kuunganisha Taasisi mbili za TCC na TBC na kuunda Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania-TCRA mnamo mwaka 2003 kwa lengo la kupunguza urasimu, kuongeza ufanisi na kukuza ubora zinazosimamiwa.

TCRA ilianza kutekeleza majukumu yake mnamo tarehe 1 Novemba, 2003 ikichukua majukumu ya TCC na TBC zilizounganishwa. Hatua hii ilitekelezwa chini na kifungu cha 4 (1) hadi (7) cha Sheria ya TCRA, 2003.

DIRA YETU

Kuwa na jamii iliyowezeshwa kwa huduma za Mawasiliano ya kielektroniki na posta zenye hadhi ya kimataifa.

DHAMIRA YETU

Kusimamia huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kwa kuhimiza ushindani wenye tija, ufanisi wa kiuchumi na upatikanaji wa huduma bora kwa wote; pamoja na kulinda maslahi ya wadau kwa ustawi wa jamii ya Kitanzania

LENGO KUU

Kuboresha maisha ya Watanzania kupitia udhibiti wenye ufanisi, unaochochea na kukuza ubunifu na ambao unahakikisha kupatikana kwa huduma bora na imara za mawasiliano kwa wote na ambazo zinatolewa kwa gharama nafuu.

MALENGO MAKUU YA KIMKAKATI

  1. Kuzifanya shughuli za TCRA kuwa za kisasa kwa kutumia teknolojia sahihi; kuimarisha tafiti zenye ubora katika huduma zinazodhibitiwa, uwezo na umahiri wa watumishi.
  2. Kukuza ufanisi; kuaminika na kuhakikisha usalama wa miundombinu ya mawasiliano na matumizi yake.
  3. Kukuza ufanisi na unafuu wa huduma za Mawasiliano na kuongeza upatikanaji wa huduma za Posta na TEHAMA katika maeneo yasiyohudumiwa ipasavyo na yale yasiyo na huduma kabisa.
  4. Kulinda maslahi ya wadau na kukuza uelewa wa haki na wajibu wao.
  5. Kufuatilia utendaji wa huduma zinazosimamiwa na kuhakikisha utekelezaji wa Sheria na Kanuni kwa viwango vinavyostahili.
  6. Kuratibu utekelezaji wa ahadi za kisekta kitaifa, kikanda na kimataifa.

SERA YETU YA UBORA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imejikita katika kuhakikisha inafikia malengo yake ya kimkakati na kuhakikisha kwamba wateja wake wanaridhika na huduma zake zitakazotolewa kwa Mfumo wa Usimamizi wa Ubora.

MALENGO YA UBORA

  1. Kuboresha utaratibu na hatua za usimamizi wa sekta ya mawasiliano.
  2. Kufikia kiwango cha juu ya kuridhisha wateja kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa TCRA.
  3. Kuendelea kuzingatia matakwa ya kisheria na kiusimamizi.
Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!