JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Serikali Kuboresha Matumizi ya TEHAMA


Serikali Kuboresha Matumizi ya TEHAMA

 

Serikali imeeleza kwamba dhamira yake ni kurahisisha upatikana wa huduma mbalimbali kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha maisha ya Wananchi nakuongeza kasi ya Maendeleo ya Taifa.

Akizindua Mpango Mkakati wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, na Tovuti Mpya, Jijini Dodoma tarehe 01/07/2021, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Faustine Ndugulile amesema matumizi sahihi ya TEHAMA huongeza Ufanisi katika upatikanaji wa huduma na huokoa mda. 

“Malengo mahsusi ya Mpango Mkakati ni Upatikanaji wa Huduma za Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Posta zilizoboreshwa; Uwezeshaji wa kidijitali unaongezwa; Uwezo wa kitaasisi wa kusimamia Huduma za Teknolojia ya Habari unaimarika, Mawasiliano na Huduma za Posta unaboreshwa; pamoja na uwezo wa kitaasisi kutoa Huduma unafanyika katika viwango vinavyotarajiwa.

Mhe. Waziri Ndugulile amesema Utekelezaji wa malengo haya; pamoja na mambo mengine ni pamoja na wizara kutimiza mikakati ifuatayo; Kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa kutoka asilimia 1.5 hadi asilimia 3;Kufikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya kasi (broadband services)  nchini kutoka asilimia 45 hadi 80%, Kuwezesha uunganishaji wa huduma za mawasiliano ya kasi kwa Taasisi za Serikali kutoka asilimia 20 hadi asilimia 70; na Kuongeza ufikishwaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yale yenye huduma duni mjini kutoka asilimia 94 hadi 100.

Aidha, Mhe Waziri amesema Serikali kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (blue print) inaendelea na utekelezaji wa Mpango kazi wake ambapo kwenye Sekta ya Mawasiliano juhudi zilizofanyika ni pamoja na kutambua tozo zilizokuwa zinatozwa kwa kujirudia. Aidha, Serikali inaendelea kuhuisisha Sera ikiwemo Sera ya Posta pamoja na Sheria yake ambazo zitaongeza ushindani wa soko.

Amesema Wizara iko mbioni kutunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo inalenga kudhibiti matumizi mabaya ya taarifa binafsi.  Sheria hii itakuwa Sheria mahsus kwenye suala zima la ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo kuendana na matakwa ya Kikatiba ya kulinda faragha za wanachi wanapopata huduma mbalimbali zinazohusu TEHAMA. Aidha, sheria hii ni muhimu kwa ajili ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuwa ni moja ya sharti katika miongozo ya Kikanda na Kimataifa inayotumiwa na makampuni makubwa kama kigezo cha  kuwekeza.

“Vile vile Serikali inaandaa Sheria ya TEHAMA itakayowezesha utekelezaji wa malengo yaliyomo kwenye Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016. Pamoja na kuwepo kwa Sheria mbalimbali kama TCRA, 2003, EPOCA, 2010 na e-transaction Act, 2015 na Cyber Crime Act, 2015 bado kumekuwepo na ombwe la kisheria la kudhibiti masuala ya TEHAMA kiujumla nchini. Kutokana na mapungufu yaliyopo, Serikali imeona ni vyema kutunga Sheria hii mahususi” amefafanua Mhe. Waziri.

Wadau kutoka sehemu mbalimbali za Nchi  zikiwemo na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Baraza ya Ushauli ya Watumiaji huduma (TCRA-CCC), Shirika la Posta na Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL),  wamehudhulia mkutano huo ambao ulirushwa Mubashara na Televisheni ya Taifa TBC1.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!