JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Ujumuishi Kifedha Tanzania Wazidi Kukua, Mawasiliano Kwa Wote Yaimarika


Ujumuishi Kifedha Tanzania Wazidi Kukua, Mawasiliano Kwa Wot...

 

Miamala ya kifedha kupitia simu za mkononi Tanzania imeongezeka kwa asilimia 30 kati ya Septemba na Desemba 2023 na kwa asilimia 44 ndani ya mwaka mmoja (Januari hadi Desemba 23), hali inayoakisi kukua mfumo jumuishi wa kifedha nchini, huku mipango ikikamilika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika sehemu nyingi; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeeleza.

Taarifa ya robo mwaka ya Oktoba hadi Desemba 2023, iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari pia imesema uwiano wa mawasiliano ya simu kwa idadi ya watu imeongezeka na simu za ulaghai zimepungua kati ya Januari na Desemba 2023.

Septemba 2023 akaunti za pesa kwa simu zilikuwa 51,369,347 ambazo zilifanya miamala 422,390,546  na Desemba 2023 zilifikia 52,875,129 zilizofanya miamala 549,529,470. Miamala 380,561,622 ilifanywa kupitia akaunti 42,120,445 Januari mwaka jana.

 TCRA inatoa leseni kwa watoa huduma za simu za mkononi na kuwapa namba za mawasiliano na misimbo, au namba fupi ya kuwezesha miamala hiyo. Benki Kuu ya Tanzania inasimamia sekta ya fedha kwa ujumla na inatoa leseni za huduma za fedha mitandaoni. Taasisi hizi zinashirikiana kwenye masuala ya fedha mtandaoni.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikakati imekamilika kutatua changamoto ya huduma za utangazaji wa redio kutofika baadhi ya sehemu nchini zenye hali ya mazingira magumu kijiografia, hasa zilizo pembezoni na maeneo yenye milima na mabonde.

Dkt Bakari amesema TCRA imeainisha maeneo yenye huduma hafifu na yasiyo na huduma za mawasiliano ya simu na intaneti baada ya kufanya utafiti ncnhini kote. Imewasilisha taarifa ya utafiti huo kwa huduma ili waboreshe huduma kwenye maeneo hayo.

Vilevile Mamlaka imeendelea kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) juu ya uwezekano wa kujenga miundombinu mipya kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara kwa wawekezaji na ambayo hayajafikiwa na huduma ipasavyo.

TCRA, ambayo imetimiza miaka 20 Novemba 2023, inasimamia sekta ya mawasiliano nchini kwa kutoa leseni, kufuatilia masharti ya leseni na kanuni, kubuni mipango ya kuendeleza sekta hiyo na kusimamia sera za sekta ya mawasiliano.

Taarifa hiyo imetaja uwepo wa Sera imara, sheria nzuri na mifumo wezeshi ya kiusimamizi na utoaji leseni kuwa imewezesha mafanikio hayo.

Taarifa hiyo imeonesha kuwa dakika za simu za kimataifa zinazoingia nchini zimeongezeka kwa asilimia 29.2; kutoka 2,216,904 Septemba 2023 hadi  3,129,711 Desemba 2023. Dkt Jabiri amefafanua kuwa kuongezeka kunasababishwa na mabadiliko yanayoendelea ya kuoanisha upigaji simu ndani ya nchi za Afrika Mashariki, ambapo kwa sasa mtumiaji anapiga simu kwenda nchi nyingine ukanda huu kama yuko nchini kwake.

Taarifa hiyo ya robo mwaka imeeleza kwamba simu za  uzao wa pili (2G) zimefikia asilimia 98 ya watu nchini, uzao wa  tatu (3G) umefikia asilimia 86, uzao wa nne (4G) asilimia 79.

Kijiografia, uzao wa tatu umefika asilimia 70 ya nchi na uzao wa nne aslimia 63.. Simu za 2G zinawezesha huduma za sauti na ujumbe mfupi, yaani meseji; 3G zinawezesha watumiaji kupata huduma zinazowezeshwa na 2G, na pia kutuma na kupokea barua pepe kwa wingi mara moja. Uzao wa 4G unawezesha maongezi, meseji, data, video, picha na hata televisheni kupitia simu ya mkononi.

Simu zenye uwezo mkubwa, au simu janja,  zimeenea kwa asilimia  32 miongoni mwa watu.

Dkt. Bakari alidokeza kwamba TCRA itafuatilia kwa kina gharama za simu janja kwani  kutokuenea kwa simu janja kwa watumiaji wengi ni mojawapo ya sababu za kutokuenea kwa matumizi ya intaneti kwa kasi.

“Uwiano kati ya mitandao na matumizi ya intaneti unaonesha kuwa maeneo mengi yamefikiwa na huduma za intaneti ila kuna watumiaji wachache; sababu ikiendelea kuwa ni idadi ndogo ya watumiaji wenye simu janja,” amesema.

Taarifa hiyo imebainisha kwamba Tanzania imepata masafa mapya yatakayowezesha huduma ya intaneti ya kasi (5G) ambayo ni muhimu katika kuchochea uchumi wa kidijitali. Masafa hayo yalitolewa kwenye mkutano wa kila miaka minne wa masuala ya masafa unaoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU) uliofanyika Dubai Falme za Kiarabu Desemba mwaka jana.

Tanzania pia ilipata nafasi katika obiti ya satelaiti kwa ajili ya satelaiti ya Utangazaji; mafanikio yatakayowezesha kuenea huduma za utangazaji hasa kwenye maeneo yasiyo na usikivu mzuri wa redio yaliyopo pembezoni mwa nchi na yaliyozungukwa na milima ambapo matangazo ya mfumo wa utangazaji wa  FM hayafiki.

 Mawimbi ya FM yana changamoto ya kutofikisha matangazo mabondeni na sehemu zilizokingwa na milima ambapo watu wanaishi kama vile maeneo ya Rombo mkoani Kilimanjaro na kwingineko.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba maeneo kumi (10) yenye changamoto hizi yametambulika baada ya utafiti na uchambuzi wa pamoja wa TCRA na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na yanategemewa kutengewa fedha kupitia utaratibu maalumu uliowekwa na Mfuko huo.

Juhudi za kukabiliana na simu za ulaghai na zinazotumika kwa utapeli zinaelekea kuzaa matunda kutokana na  kupungua kwa matukio yaliyoripotiwa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, simu za ulaghai zimeshuka kutoka asilimia 2 ya idadi ya laini za simu zilizosajiliwa Septemba 2022 hadi asilimia 0.01 Desemba 2023. Simu za ulaghai zilianza kupungua Novemba 2022.

Simu zilizofungiwa baada ya kuripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu pia zilipungua kwa asilimia 13.03 kati ya Septemba na Desemba 2023.

Namba tambulishi zilizofungiwa kati ya Oktoba na Desemba 2023 baada ya kuripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu zimepungua kwa asilimia 13. Laini 30,309 zilifungiwa Desemba ukilinganisha na 34,848 zilizofungiwa Septemba 2023.  Laini zinafungiwa kuwezesha kupunguza matukio ya wizi na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya Mawasiliano vyenye ubora kwenye soko.

Kwa upande wa huduma za posta, taarifa hiyo imesema huduma za usafirishaji vifurushi umeendelea kufanywa na Posta ta Taifa na watoa huduma binafsi, na idadi ya vitu vilivyotukwa nje ya nchi imeongezeka kutoka 239,239 Desemba 2022  hadi   243,199 Desemba 2023.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!