JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yahimiza Uimarishaji Elimu Wezeshi Kidijiti


TCRA yahimiza Uimarishaji Elimu Wezeshi Kidijiti

Na mwandishi wetu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatafsiri vipaumbele vya kitaifa kwenye sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuendeleza mipango inayolenga kuimarisha ujuzi na vipaji.    

TCRA inaendeleza mipango ya aina mbili – kuendeleza vilabu vya kidijiti na kuwezesha uvumbuzi na ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano.

Mipango hii inaonesha namna TCRA inavyochangia kufikiwa kwa malengo kwenye  Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 (TDV 2025), Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano (FYDPIII) na  Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali utakaotekelezwa kati ya 2024 na 2034.

TCRA inahimiza na kuendeleza uanzishaji wa vilabu vya kidijiti katika ngazi  mbalimbali za elimu – kuanzia shule za chekechea hadi vyuo vikuu. Mpango huu unakusudiwa  kukabili mapengo katika utoaji wa elimu ya sayansi, ambayo itawezesha kujengwa Tanzania ya kidijiti.

Vilevile TCRA inatoa, bure na kwa muda, raslimali za mawasiliano kwa wavumbuzi/wabunifu kujaribu miradi yao inayolenga kupanua wigo wa mawasiliano nchini na kutatua changamoto.

Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali unahimiza wadau kuendeleza  elimu na uelewa wa masuala ya kidijiti kama sehemu muhimui ya  kufanikisha ujenzi wa uchumi wa kidijiti Tanzania. Unataka juhudi zifanyike kuwezesha upatikanaji wa elimu, ujuzi na kujenga stadi za kidijiti katika ngazi zote.

Aidha unasisitiza umuhimu wa kuendeleza  ari ya masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STUH). Haya yanawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yatakayowapa uelewa wa masuala ya teknolojia zinazowezesha uchumi wa kidijiti.

Dira ya Maendeleo 2025 na FYDPIII vina mikakati ya kuendeleza TEHAMA kwenye ngazi zote kujenga uchumi wa kidijiti Tanzania. Uchumi wa Tanzania unatakiwa kushindana na wa nchi nyingine, sio Afrika tu bali ulimwenguni pote.

Uchumi huu utawezeshwa kwa kujenga mwelekeo tawala wa matumizi ya TEHAMA kwenye sekta zote. Hizi ni pamoja na uendeshaji, uzalishaji, biashara, utoaji huduma za jamii na uendeshaji wa serikali na taasisi za umma.

Dira inalenga kujenga jamii ya kidijiti Tanzania kuanzia umri mdogo. Mfumo wa elimu Tanzania unatakiwa kujenga ndani ya wanafunzi utamaduni wa sayansi na teknolojia kwa rika zote za wanafunzi.

Inataka umuhimu uwekwe  kwenye masomo ya sayansi na hisabati ili kuwezesha wanafunzi kukabiliana na mahitaji ya teknolojia za kisasa, ambazo zinabadilika kwa kasi. Masomo haya ni pamoja na STUH, yanayoweka msingi imara wa uchumi wa kidijiti.

 Wataalamu wamethibitisha kwamba STUH ina faida  kwa taifa na kwa wanafunzi, kwa namna na hatua tofauti. Pamoja na kuwezesha ujenzi wa uchumi wa kidijiti, masomo haya yanawapatia wanafunzi zana za kujenga maisha yao ya baadaye ya ajira au kujiajiri kwenye mazingira yanayotawaliwa na TEHAMA.

Inakisiwa kwamba katika miaka michache ijayo, TEHAMA itaondoa asilimia 50 ya kazi zinazofanywa na wataalamu walioajiriwa. Kwa maneno mengine, kujiajiri kutatawala maisha miaka ijayo.

 Vilevile, watafiti wameonesha kuwa asilimia 25 tu ya wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu kwenye nchin nyingi za Afrika wanachukua masomo ya STUH au yatakayowawezesha kuajiriwa au kujiajiri kwenye shughuli zinazohusisha TEHAMA.

Baadhi ya vikwazo ni uhaba wa vifaa na miundombinu ya kuwezesha STUH. Hii ni pamoja na kutokuwepo maabara kamili. Vingine ni  uchache wa walimu na wakufunzi. Vile vile kuna kasumba na fikra potofu kuhusu masomo ya sayansi, hasa kwa baadhi ya wanafunzi, hasa wasichana kuona hisabati ni ngumu kuimudu.

Kwenye makala ya jarida la kitaaluma kuhusu changamoto za  masomo ya sayansi Tanzania, watafiti Ladislaus Semali na Khaujan Mehta wanataja uelewa mdogo wa baadhi ya walimu na wakufunzi wa STRUH kama kikwazo kingine. Aidha, kuna wakufunzi wasioweza kupitisha wanafunzi kwenye elimu kwa vitendo.

Kikwazo kingine ni wanafunzi wasichana kuogopa masomo ya sayansi kwa kudhania ni magumu na  madarasa kulundika wanafunzi  kupita idadi inayokubalika. Mitaala isiyo na uhalisia pia ni tatizo, wameongeza.

Wanasema ingawaje kati ya 1965 na 2007 Tanzania imetekeleza mipoango kadhaa ya kuboresha elimu ya sayansi nchi bado haijaboresha utoajni wa masomo ya STUH Makala hiyo inapatikana touvoti ya https://www.sciencedirect.com/.

Hoja ya huo ugumu wa hisabati imepingwa na kutolewa maelezo jana, Jijini Dar Es Salaam wakati wa mahojiano maalum  na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, ambapo alisema hisabati ni rahisi, na kinachotakiwa ni kuijua misingi yake.

Wataalamu wa elimu wanapendekeza kuendeleza mafunzo ya walimu yanayowezesha STUH. Vilevile kuwe na motisha kwa vyuo vinavyowezesha masomo hayo ili vipanue uwezo wao.

Mipango ya uanzishaji klabu za kidijiti na kuendeleza uvumbuzi/ubunifu, inayoratibuwa na TCRA ni sehemu ya njia za kuondoa vikwazo hivi.

Kilabu za kidijiti zinawezesha utoaji wa elimu na uelewa wa STUH kuanzia ngazi ya chini kabisa ya elimu.

Dkt. Jabiri Bakari anaeleza kuwa misingi imara ya STUH ni muhimu kujenga Tanzania ya kidijiti, itakayofanikishwa na ushiriki wa wadau wengi wenye stadi na ujuzi wa masuala ya kidijiti. 

STUH itawezesha Tanzania kuwa na kiwango kikubwa cha uelewa wa masuala ya kidijiti; na  na kujenga jamii shirikishi kidijiti.

Klabu za kidijiti zinawezesha wanafunzi kuwa na uelewa mpana, elimu na ujuzi kuhusiana na masuala ya TEHAMA na mawasiliano kwa ujumla. Klabu hizi zinawafanya wanafunzi kujamini na kuwawezesha kujijengea utamaduni wa masuala ya kidijiti.

Vilevile klabu zitatoa fursa kwa wanafunzi wa shule mbalimbali kushirikiana katika masuala yanayahusiana na STUH na mawasiliano kwa ujumla, Klabu zitawezesha kufanyika midahalo mbalimbali yenye tija kwenye masuala mbalimbali ya kiteknolojia na mawasiliano kwa ujumla.

Midahalo itajenga umahiri wa wanafunzi kujieleza na kudadisi mambo kwa kutumia taarifa sahihi.

TCRA imechapisha mwongozo wa uanzishaji wa klabu hizi za kidijiti. Vilevile inaandaa dirisha maalum kwenye tovuti yake – www.tcra.go.tz – kwa ajili ya klabu. 

Mwongozo huo utawezesha ulinganisho wa njia za kuanzisha  na kuendesha klabu.

Dirisha hilo litatumika kusajili klabu na kuweka kumbukumbu za shughuli za vilabu mbalimbali. Lengo ni kuwafikia wadau wengi na kuhakikisha uendelevu wa mipango ya kutoa elimu, na kujenga uelewa wa masuala ya kidijiti.

Dirisha hilo litakuwa na sehemu mbalimbali kwa makundi tofauti yanayohusika kwenye vilabu vya kidijiti. Kwa mfano dirisha la chekechea litakuwa na picha na michoro ya kuvutia na maudhui yake yatakuwa rahisi sana kufuatilia,

Maudhui kwa shule za msingi yataweka uwiano wa vitu vya kufurahisha na vya elimu. Kutakuwa na michezo[m1]  inayoelimisha, chemsha bongo shirikishi, hadithi za kusisimua na  zenye msukumo wa kupenda masuala ya kidijiti. Pia kutakuwa na masomo yanayowezesha STUH.

Shule za sekondari zitawekewa maudhui yenye elimu kwa ndani na makala za kusisimua na kutoa moyo, zinazoelimisha. Pia kutakuwa na maudhui yenye msaada wa ziada wa kusoma, video za kuhamasisha na vidokezo vya fursa za ajira au kujiajiri. 

Wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati watawekewa masomo ya kina na masuala ya kujiendeleza kwenye TEHAMA. Kutakuwa na maudhui yenye STUH kwa kina na yanayohusiana na utafiti wa kitaalamu.

Dirisha la klabu za kidijiti kwenye tovuti ya TCRA pia litakuwa na  maudhui kwa makundi mengine kwenye mfumo wa uanzishaji wa klabu za kidijiti. Kutakuwa na maudhui ya namna ya kujiendeleza kitaaluma, fursa za kugharimia elimu, na maelezo kuhusu raslimali za kufundishia. Watawezeshwa pia kuingia kwenye kanzidata mbalimbali za kisayansi, kupata majarida ya kitaaluma na kuwasiliana na wadau wengine.

 Wazazi na walezi wanahamasishwa kuwa na utamaduni wa kushiriki kupata maudhui mitandaoni, Hii itawawezesha kufuatilia maudhui yanayoangaliwa na watoto wao mitandaoni. 

Sehemu ya wazazi na walezi kwenye tovuti itakuwa na namna ya kufuatilia elimu ya watoto wao, mwelekeo wa elimu kitaifa na ulimwenguni na pia mbinu za kuwezesha watoto wao kujifunza wakiwa nyumbani.  

TCRA inaendesha kampeni nchi nzima kuongeza uelewa wa umma na wadau kwenye masuala ya kidijiti na uanzishaji wa klabu za kidijiti. Elimu pia inahusisha fursa za kutumia raslimali za mawasiliano kwa ajili ya uvumbuzi/ubunifu kwenye TEHAMA na mawasiliano kwa ujumla.

Elimu hii inachangia kufanikisha mojawapo ya mikakati ya Dira ya Maendeleo Tanzania 2025,

Dira inahimiza  elimu na uelewa  kuhusu masuala ya sayansi na teknolojia na matumizi yake, ili kuleta tija kwenye sekta mbalimbali. Inasisitiza kwamba elimu hiyo ienezwe kwenye jamii yote kupitia kampeni endelevu za mafunzo na elimu.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!