JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Ushirikiano Baina Ya Tanzania Na Burundi Katika TEHAMA kuwezesha ukuzaji uchumi ukanda wa maziwa makuu


Ushirikiano Baina Ya Tanzania Na Burundi Katika TEHAMA kuwez...

 

MAHUSIANO ya Burundi na Tanzania; ni ya kitambo na madhubuti. Burundi ni mshirika wa kimkakati wa Tanzania katika maeneo mengi, hasa biashara. Kwa kuwa Burundi ni nchi isiyo na bandari, karibu 80% ya bidhaa zake hupitishwa kwa barabara kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Burundi ni mshirika wa kimkakati katika masuala ya ushirikiano wa forodha na biashara; na imekuwa mshirika thabiti.

Mara baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo mwaka 1977 na hatimae kuundwa upya kwa Jumuiya hiyo Julai 2000, Tanzania imekuwa mshirika muhimu wa kiuchumi siyo tu wakati Burundi ilipojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ya sasa mnamo Julai 2007, bali pia kabla na wakati nchi hizi zikiwa nje ya ushirikiano wa kikanda.

Burundi siyo tu mshirika wa moja kwa moja wa kibiashara na Tanzania lakini pia nchi hiyo ni lango muhimu la kupitisha bidhaa kutoka Bandari ya Dar es salaam kwenda Mashariki mwa DRC. Ushirikiano huu hauishii kwenye bidhaa pekee bali pia katika kusambaza na kufikisha huduma zikiwemo za Mawasiliano. Katika kusambaza huduma za mawasiliano Tanzania hapa inaiona fursa ya kushirikiana na Burundi kukuza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kupeleka huduma hiyo kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Umoja wa Mawasiliano wa Afrika (ATU) ni shirika barani Afrika linalounganisha nchi na watoa huduma za mawasiliano ukiwa na shabaha ya kuongeza kasi ya maendeleo ya usambazaji wa miundombinu ya TEHAMA; Tanzania kwa kuzingatia kuwa ni mwanachama hai wa Umoja huu imejidhatiti kuhakikisha inakuwa kinara wa usambazaji wa miundombinu hii hasa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ikiwa ni kuunga mkono juhudi za ATU kutimiza azma yake ya kufikisha huduma za TEHAMA kote barani Afrika.

Tanzania inatarajia kujenga mfumo imara wa ikolojia ya kidijitali na kuifanya nchi kuwa kitovu cha TEHAMA kikanda, dhamira hii ya serikali imeelezwa mara nyingi na viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Ashatu Kijaji (MB), kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Kwa kutambua ukweli huo Burundi imekuwa ikifanya ziara mara kwa mara Tanzania na hasa kuonana na watendaji wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na taasisi nyingine za TEHAMA ili kujifunza namna Tanzania inavyoweza kushirikiana na Burundi kukuza TEHAMA.

Ukuzaji ushirikiano katika sekta ya Mawasiliano baina ya Tanzania na Burundi utamaanisha kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi ambapo mapema mwezi Novemba mwaka huu katika ziara yao kwenye ofisi za TCRA, Menejimenti ya Shirika la Posta Burundi ilieleza kufurahishwa kwao na namna walivyojifunza na kuridhishwa kwao na hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kukuza TEHAMA kwenye sekta ya Posta na kusisitiza kuwa Burundi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye sekta hiyo kongwe, yenye mustakbali  chanya katika Maendeleo ya nchi hizo mbili.

Miongoni mwa masuala waliyoelezwa Menejimenti hiyo ni namna Tanzania kupitia Shirika la Posta inavyoweka mikakati ya kukuza Posta kidijitali ili kuhakikisha huduma za Posta zinafikia maeneo ya ndani na nje ya nchi kwa urahisi zaidi mambo ambayo Menejimenti hiyo ilieleza kujifunza na kwenda kutendea kazi ili kubadili taswira ya huduma za posta nchini mwao.

Pembezoni mwa mazungumzo na ujumbe huo pia, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari aliueleza ujumbe huo kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano barani Afrika inaimarika na ndiyo sababu inakuza mashirikiano na Shirika la Posta Afrika (PAPU) kuhakikisha kwamba sekta ya Posta inakuwa thabiti kote barani na kwenye ukanda. Akaeleza kuwa Tanzania imejidhatiti kuhakikisha ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya PAPU unaendelea kwa kasi stahiki jijini Arusha ili kwa kadri itakavyofaa mwaka 2022 ujenzi ukamilike. Lengo halisi ni kuhakikisha Tanzania inakuwa mwimo thabiti wa mawasiliano kwenye eneo la ukanda wa Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na kote barani.   

Ushirikiano wa Tanzania na Burundi kwenye sekta ya TEHAMA unachagizwa na kuunganishwa kwa huduma na miundombinu ambapo Tanzania kupitia Kampuni ya Mawasiliano ya Simu (TTCL) imejielekeza kufikisha huduma Burundi kupitia vituo vya Kabanga na Manyovu mbali na vituo vingine. Uunganisho huo chini ya TTCL ukiratibiwa kwa pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) unaendeleza azma ya serikali ya awamu ya sita kuhakikisha nchi jirani zote ikiwemo Burundi zinafikishiwa na kuunganishwa na Tanzania kupitia Mkongo wa Mawasiliano. Mkongo wa mawasiliano hauishii Burundi pekee bali unazifikia nchi za Zambia, Malawi, Rwanda, na Msumbiji mbali na nyingine.

Mkurugenzi Mkuu wa Posta ya Burundi Lea Ngabire wakati wa ziara yake kwenye ofisi za TCRA na Shirika la Posta Tanzania alionesha matumaini makubwa waliyonayo kwa kufafanua kuwa mara baada ya wakuu wa nchi hizi mbili kukutana mnamo Julai 2021 wao kama watendaji wakuu wa taasisi za mawasiliano Burundi waliona sababu ya kufika Tanzania ili kuanza utekelezaji wa maazimio ya wakuu hao wa nchi hizi mbili yaani Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Evariste Ndayishimiye ambao walikubaliana nchi hizi mbili zikuze zaidi ushirikiano kwenye masuala mbalimbali yenye maslahi ikiwemo kujenga kituo cha huduma za pamoja eneo la mpakani la Manyovu Mugina ili kukuza muingiliano wa sekta mbalimbali za uchumi.

Katika mwaka 2021, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeiwezesha Burundi kupata taarifa muhimu za namna mifumo ya fedha mtandao inavyofanya kazi, namna ya kudhibiti uhalifu kwenye mtandao kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ujenzi wa mifumo laini inayowezesha shughuli za udhibiti wa mawasiliano na jinsi Tanzania inavyojidhatiti kuboresha huduma za Posta kidijitali; haya pamoja na mengine mengi ambayo yaliwezekana kutoka na ziara angalau tatu za mafunzo zilizofanywa na maafisa mbalimbali wa Burundi nchini Tanzania yanaleta mwanga kwamba Tanzania na Burundi sasa zinapiga hatua kubwa katika ushirikiano kwenye eneo la kukuza TEHAMA.

Ushirikiano wa Burundi na Tanzania katika sekta ya Mawasiliano na TEHAMA unaleta ishara nzuri kwamba nchi hizi mbili zitakuza uchumi wa kisasa pamoja utakaowezesha kuleta ukuaji wa haraka wa Maendeleo ya nchi hizo mbili, hasa ikizingatiwa kwamba muelekeo wa uchumi wa kisasa unaegemea pakubwa uboreshaji wa mifumo na njia za mawasiliano suala ambalo Tanzania inalisimamia kwa dhati chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!