JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Australia Yaonyesha nia kushirikiana na Tanzania Kukuza TEHAMA


Australia Yaonyesha nia kushirikiana na Tanzania Kukuza TEHA...

 

  • Majadiliano yafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani - ITU WTDC – 2022 Kigali, Rwanda

Na Mwandishi Maalum/ Kigali, Rwanda

Tanzania inatarajia kunufaika kwa ushiriki wake kwenye Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani (ITU WTDC - 2022), unaofanyika jijini Kigali - Rwanda, kujadili na kuweka mipango ya Maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano Duniani; ukiandaliwa na Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (ITU). Mkutano huo unafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika ukilenga kuweka mikakati ya kuhakikisha jamii zote duniani zinaunganishwa kwenye mifumo ya mawasiliano.  

Katika Mkutano huo Tanzania ilikutana na kufanya mazungumzo na Serikali ya Australia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya nchi hiyo, ambapo mbali na kuomba uungwaji mkono ili nchi hiyo iipigie kura Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la ITU pia walijadili masuala ya kuongeza ushirikiano kwenye maeneo ya sera, masuala ya ufundi na taluma na utafiti.

Akizungumzia mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa ITU WTDC – 2022 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari alibainisha kuwa Australia imekubali kuiunga mkono Tanzania katika maeneo yote ya majadiliano na kwamba imefurahishwa na ushiriki wa taasisi za elimu ya juu kwenye mkutano huo wa Rwanda.

“Kiufupi tumekubaliana kushirikiana na Australia kwenye maeneo matatu, eneo la sera, eneo la taaluma na utafiti, masuala ya kiufundi kwenye eneo lote la TEHAMA ambayo yanahusisha usalama mtandaoni, wameonesha kuvutiwa kwao na uwepo wa vyuo vikuu vitatu UDOM UDSM na DIT na kuahidi kuendeleza mashirikiano kati yao na taasisi za elimu ya Juu za Tanzania” alibainisha Bakari.

Ikiwa ni mwanachama hai na mshiriki wa mkutano huo, Tanzania itatumia fursa hiyo kuomba uungwaji mkono kutoka nchi wanachama wa ITU kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la ITU kwenye mkutano mkuu wa Shirika hilo utakaofanyika mjini Bucharest, Romania, itakapowadia mwezi Septemba baadae mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akizungumzia vipaumbele vya mdhibiti wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania alisisitiza kuwa Mamlaka anayoiongoza imejidhatiti kuwa mshiriki anaekwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa kuhakikisha inashirikiana na nchi nyingine duniani kupokea na kuyatekeleza mageuzi muhimu ya TEHAMA.

"Matarajio yetu ni kuona mkutano huu unaiwezesha TCRA kuelewa upi hasa ni mwelekeo wa sekta ya mawasiliano na TEHAMA katika ujumla wake duniani ili nasi kama nchi tusiachwe nyuma; ushiriki wetu unaipa Mamlaka nguvu ya kuwa mshiriki thabiti kwenye mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia duniani; hasa ukizingatia kuwa sekta ya mawasiliano ina kasi kubwa ya ukuaji, nasi tunataka kuwa sehemu ya mabadiliko hayo," alifafanua Bakari na kuongeza.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!