JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wanaohitaji Leseni za Mawasiliano Sasa Mambo Waah! - TCRA


Wanaohitaji Leseni za Mawasiliano Sasa Mambo Waah! - TCRA

 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imethibitisha kwamba huduma kwa watoa huduma za mawasiliano au wanaohitaji kutoa huduma hizo sasa zimekuwa rahisi zaidi baada ya kukamilisha mfumo wa Tanzanite Portal unaowaleta pamoja watoa huduma za mawasiliano nchini, wakiwemo watoa huduma wakubwa na wadogo.

Akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Unguja, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Jabiri Bakari, alisisitiza kwamba mfumo huo sasa unaowezesha TCRA kutoa huduma mbalimbali kwa wateja wake ambao ni watoa huduma za mawasiliano nchini, ikiwamo kuwezesha usajili wa bidhaa na huduma za sekta ya mawasiliano, utoaji wa leseni, na ulipaji wa tozo.

"Tumeongeza ufanisi katika kuhudumia mteja kupitia dirisha moja la maombi ya leseni za aina zote, utoaji wa vyeti vya uhakiki wa vifaa vya kielektroniki, kanzidata ya anuani za makazi, na dawati la huduma kuwezesha mawasilisho ya malalamiko ya wateja," alibainisha Dkt. Jabiri.

Aliongeza kwamba mfumo huo unawezesha uwasilishaji wa maombi ya leseni na nambari za mawasiliano bila mwombaji kulazimika kufika kwenye ofisi za TCRA.

Pia, unawezesha upangaji, ugawaji, na ufuatiliaji wa postikodi za anwani za makazi; ushughulikiaji wa maoni, changamoto, na taarifa mbalimbali kutoka kwa wateja wa TCRA ambao ni Watoa Huduma za mawasiliano nchini. Mfumo huo pia alieleza unaiwezesha TCRA kubainisha leseni za Watoa Huduma (Know Your Customer), kupata taarifa za watoa huduma kiurahisi zaidi pamoja na kuwezesha mamlaka hiyo kupata taarifa za malipo za watoa huduma za mawasiliano.

Aliongeza kuwa, mfumo huo pia unarahisisha ushughulikiaji wa maombi ya uhakiki wa vifaa vya kielekroniki (Online Type Approval), na kumwezesha mwananchi au mwenye leseni ya mawasiliano kukamilisha uhakiki wa leseni za mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi kupitia msimbo wa USSD *150*52#. Msimbo huo unamwezesha Mwananchi kuhakiki uhalali wa huduma zinazotolewa na mtoa huduma ili kuhakikisha kunakuwapo udhibiti wa watoa huduma za mawasiliano wasioidhinishwa na Mamlaka hiyo iliyopewa jukumu la kutoa, kuhuisha na kutwaa leseni za mawasiliano nchini.

Jabiri, alisema kuwa mfumo wa Tanzanite Portal ni wa kipekee na una manufaa makubwa kwa watoa huduma za mawasiliano. Mfumo huo unarahisisha utoaji wa huduma kwa watoa huduma, na unasaidia kuboresha ufanisi na uwazi katika usimamizi wa huduma za mawasiliano nchini.

“Tanzanite Portal umeundwa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau wote wa sekta ya mawasiliano nchini. Mfumo huu umeunganisha huduma mbalimbali katika dirisha moja, kutoa urahisi na ufanisi zaidi katika mchakato mzima wa huduma za TCRA,” aliongeza.

Wakizungumzia Mfumo huo baadhi ya wadau wa sekta ya mawasiliano wakiwamo watoa maudhui ya habari kwenye mtandao na Wauzaji wa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki walisifu hatua ambazo TCRA imechukua kuweka dawati la pamoja la mtandaoni linalowakutanisha na Msimamizi huyo wa sekta.

“Mafanikio haya yanathibitisha dhamira ya TCRA katika kuleta mageuzi chanya katika sekta ya mawasiliano, huu Mfumo naamini utatuondolea usumbufu wa kutumia muda mwingi kufuatilia leseni na masuala mengine pale TCRA, wamesaidia sana kuleta hili jukwaa,” alibainisha Lucas mmoja wa watoa huduma za mawasiliano nchini.

Chalila Kibuda miongoni mwa wadau wa maudhui mtandaoni alibainisha kuwa, “Jukwaa hili kwa jinsi Mkurugenzi Mkuu alivyoelezea litatufaa sana Wanahabari wa mtandaoni kushughulikia masuala ya kupata leseni na taarifa, tunawapongeza Mamlaka kwa hatua hii muhimu,” alibainisha.

Dkt Jabiri alibainisha mafanikio hayo kwenye Mkutano wake ambao hufanywa na Mamlaka hiyo kila Robo ya Mwaka wa Fedha ukiwasilisha taarifa za mwenendo wa usimamizi wa sekta ya mawasiliano nchini ambapo Mamlaka hiyo pia hutoa takwimu mbalimbali za mwenendo wa sekta ndogo za simu, Intaneti, Utangazaji na posta.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!