JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mpango wa Klabu za Kidijiti chachu kuendeleza Teknolojia Tanzania


Mpango wa Klabu za Kidijiti chachu kuendeleza Teknolojia Tan...

Na Mwandishi Wetu, GEITA

KATIKA hatua muhimu ya kujenga kizazi chenye umahiri wa kidijitali, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inahimiza uanzishaji wa klabu za kidijiti kwenye taasisi za elimu nchini kote.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema kwenye mahojiano jijini Dar es Salaam jana kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa  klabu za kidijiti zinaanzishwa katika kila ngazi ya elimu Tanzania. Mamlaka hiyo kushirikiana na wadau wengine wa elimu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye kutelekeza mpango huo, alieleza.

Dkt Bakari amesema TCRA imeanza kampeni nchi nzima kuelimisha wadau na kuhamasisha uanzishwaji wa klabu za kidijiti kwa hiali, kuanzia ngazi ya elimu ya Chekechea, Msingi, Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu.

Aliongeza kwamba mpango huo ni sehemu ya mkakati wa TCRA kuhamasisha ukuaji wa matumizi ya TEHAMA ambazo zinawezesha kutumia mifumo ya kidijiti na program wa TEHAMA katika ngazi zote za matumizi kwenye sekta mbalimbali.

Aidha ameeleza kwamba uanzishwaji wa klabu za kidijiti ni msingi mkuu wa kuwezesha ubunifu wa ndani Tanzania na uvumbuzi unaolenga kutatua changamoto za maeneo husika kwa kutumia wataalamu wa hapa Nchini.

Kampeni inayoendelea inatekelezwa kupitia ofisi ya TCRA Zanzibar na ofisi za kanda. TCRA ina ofisi kwenye kanda tano – Mashariki (Dar es Salaam), Ziwa (Mwanza), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kati (Dodoma) na Kaskazini (Arusha).  

Akihojiwa na redio za Storm FM na Blessed Hope, zote za Geita, Meneja wa Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Salum, amesisitiza umuhimu na mchango wa hizi klabu kwa kuwa zinawezesha vijana wa Kitanzania kupata stadi zinazohitajika ili kushiriki uchumi wa kidijiti.  

Kwa mujibu wa Mhandisi Imelda Salum, klabu hizi zinaundwa kwenye ngazi zote za elimu na zitakuwa majukwa muhimu ya kielimu yatakayozalisha wavumbuzi na viongozi wapya kwenye teknolojia.

" Vilabu vya kidijiti sio tu shughuli za ziada mashuleni. Kama ilivyoainishwa kwenye mwongozo wa TCRA  wa uanzishaji wa klabu, hizi zitakuwa majukwaa kwenye taasisi za elimu yatayowapatia watoto na wanafunzi kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu stadi za kidijiti wanazohitaji kufanikiwa kwenye uchumi wa kidijiti.” alifafanua.

Alitoa wito kwa wadau wote wa elimu kuunga mkono mpango huu wa klabu za kidijiti kwa kuwa zina manufaa.

"Klabu hizi ni muhimu katika kujenga jamii inayoelewa, yenye stadi na uwezo wa  kuchangia katika kufikia malengo yetu ya kitaifa, ambayo yatafanikiwa kwa kutekeleza kikamilifu mipango ya kujenga Tanzania ya kidijiti," Mhandisi Imelda Salum aliongeza.

Mpango huo pia unaenda sambamba na hatua za kuendelea masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) na pia kuimarisha fikra za wanafunzi na uwezo wao wa kuvumbua. Mhandisi Imelda amefafanua kuwa  klabu hizo ziko wazi kwa wanafunzi wote na sio tu wale wanaochukua masomo hayo. Kila mwanafunzi anaweza kushiriki kwenye klabu hizo, amesema.

Uanzishaji, uendeshaji na uendelevu wa klabu hizi vinahitaji juhudi za ushirikiano wa wadau mbalimbali. Hao ni pamoja na taasisi za elimu, wanafunzi, wazazi na walezi na jamii kwa ujumla.

Shule zitatoa na kuwezesha kutumika miundombinu, raslimali na teknolojia, wakati wazazi  na jamii wanategemewa kuunga mkono na kuhimiza vijana kuanzisha na kujiunga na klabu hizi.

TCRA imechapisha taarifa kuhusu utaratibu kwa wanaopenda kuanzisha klabu za kidijiti.  Wanaweza kujisajili kwenye tovuti maalum ya mpango huo, ambayo ni: digitalclubs.tz. Taarifa zaidi zinapatikana kwa kupiga simu ya bure, namba 0800008272, au fuata Link:  https://digitalclubs.tz/

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!