JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA na COSTECH Waja na Hatua Muhimu Kukuza Sekta ya Teknolojia ya Kidijiti Tanzania


TCRA na COSTECH Waja na Hatua Muhimu Kukuza Sekta ya Teknolo...

 

Dar es Salaam, Julai 20, 2023 - Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) zimeungana kwa lengo la kutoa rasilimali za mawasiliano bila malipo kwa kampuni zinazochipukia katika sekta ya teknolojia za kidijiti. Hatua hii inalenga kuweka mazingira bora ya kuvutia uvumbuzi wa kidijiti nchini na kuhakikisha kuwa kampuni hizo zina nafasi ya kukua na kufanikiwa.

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, alisisitiza kuwa mpango huu unalenga kuwapa vijana wabunifu zana wanazohitaji kwa majaribio ya huduma zao kwa kipindi maalum.

"Hapo awali, ili uweze kujaribu kitu chochote katika anga la mtandao, ilibidi upate leseni na kutoa gharama kubwa. Sasa tunasema kama wewe ni mwanafunzi au mbunifu umeingia kwenye ulimwengu wa kidijiti, umegundua kitu, na umetengeneza kitu kinachoweza kuleta manufaa makubwa, na unataka kukijaribu, na katika kukijaribu unahitaji rasilimali kama namba, masafa, au hata kushirikiana na kampuni za simu; tunasema majaribio kama hayo ni bure," alisisitiza Dkt. Bakari.

Hadi kufikia Juni 2023, TCRA ilikuwa tayari imetoa rasilimali hizi muhimu kwa kampuni nne. Dkt. Bakari aliwahimiza wajasiriamali vijana, wabunifu, na watafiti kuwasilisha mawazo yao ya kibunifu kwa COSTECH na kuwahakikishia kwamba baada ya idhini kutoka COSTECH, watapata rasilimali hizi bila gharama yoyote.

Rasilimali za mawasiliano ni msingi wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kama vile huduma za pesa za simu na huduma nyingine zinazotegemea teknolojia za kidijitali kama vile kilimo cha kisasa, biashara mtandao, usafirishaji, uendeshaji wa taasisi binafsi miongoni mwa zingine.

"Ugawaji wa rasilimali hizi unawezesha huduma za mtandao zenye kasi kubwa, jambo muhimu katika uchumi wa kidigitali," alisisitiza Dkt. Bakari na kuongeza kuwa wabunifu wenye bunifu zinazoleta Suluhu kwa changamoto za jamii sasa wataweza kushirikiana na TCRA,COSTECH na Watoa huduma hasa mitandao ya simu ili kuzibeba bunifu hizo.

Miongoni mwa rasilimali zinazotolewa na TCRA ni pamoja na rasilimali-namba (numbering resources), masafa (frequency spectrum), postikodi, na anwani za makazi.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA alisema mpango huu ni endelevu na kuwa TCRA na COSTECH wanahimiza wajasiriamali vijana, wabunifu, na watafiti kuwasilisha mawazo yao ya kibunifu kwa COSTECH. Baada ya kupata idhini, watapata rasilimali hizi bila gharama yoyote na kuzitumia kwa kipindi cha majaribio ya miezi mitatu pamoja na uwezekano wa kuongezewa muda wa kufanya majaribio yao..

Meneja wa Chama cha Wabunifu, Tanzania Start-Ups Association (TSA), Praygod Japhet, akizungumzia mpango huu alisema kuwa,  hapo awali rasilimali hizo za mawasiliano zililipishwa kwa kiwango kikubwa, mara nyingi hadi kufikia milioni kumi kulingana na huduma. Lakini sasa, kwa ushirikiano wa TCRA na COSTECH, wabunifu chipukizi wanapata rasilimali hizo bila malipo.

“Hii imesaidia kupunguza mzigo kwa wabunifu wengi, ambao mara nyingi ni vijana kutoka vyuo vya kati na vikuu, na ambao wamekabiliana na changamoto za upatikanaji wa mitaji. Hatua hii inaleta rasilimali adimu na za gharama kwa wabunifu, ambazo zitasaidia kuboresha jamii ya Watanzania,” alisisitiza.

Mkuu wa Kitengo cha Habari wa COSTECH, Mary Kigosi, alisema kuwa ushirikiano kati ya taasisi yao na TCRA umesaidia sana kupunguza changamoto kwa wabunifu wa teknolojia ya kidijiti ambao hapo awali walikuwa wanakabiliana na changamoto ya kupata zana hizi muhimu kwa maendeleo yao.

"Rasilimali za namba na masafa, kwa mfano, ni muhimu sana kwa wabunifu wa teknolojia ya kidijiti katika sekta za kilimo, ujasiriamali, biashara mtandao, suluhu za kielimu, na zaidi. Hata hivyo, wabunifu walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kuzipata hapo awali, lakini baada ya makubaliano kati yetu na TCRA, sasa wanapata rasilimali hizi bila malipo, na hii ni hatua kubwa kwa Tanzania katika enzi hizi za ulimwengu wa kidijitali," alifafanua.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliyoasisiwa kwa Sheria nambari 12 ya mwaka 2003, inalo jukumu muhimu la kusimamia mawasiliano nchini Tanzania, ikisimamia sekta ndogo za simu na intaneti, huduma za utangazaji na mitandao ya kijamii inayotoa habari, na huduma za posta.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!