JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Serikali ya Wahimiza Wananchi kutumia Fursa ya Biashara Mtandao


Serikali ya Wahimiza Wananchi kutumia Fursa ya Biashara Mtan...

 

Serikali imewataka watumiaji wa huduma za Mawasiliano nchini wanaotumia huduma za simu za kiganjani kuhakiki laini zao za simu ili wawe salama wakati wote wanapotumia huduma hizo.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati alipotembelea banda la maonesho ya biashara ya 45, Kimataifa la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amesisitiza kuwa ni muhimu kila Mwananchi ahakiki laini yake ya simu kwa kutumia Namba ya  Kitambulisho cha Taifa.

Ndugulile amesisitiza kuwa, Serikali inalichukulia zoezi la uhakiki wa Usajili wa laini za simu kwa uzito mkubwa na ndio sababu imetoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano ishirikiane na Kampuni za Simu kutoa elimu kuwahamasisha watumiaji wa huduma za Mawasiliano kuhakiki laini  zao za simu.

Amesisitiza kuwa ikiwa mtumiaji bado anapokea ujumbe wa uhakiki upo uwezekano bado hajahakiki na ni muhimu kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano akahakikisha anahakiki kadi yake ya simu.

“Uhakiki unaweza kufanya kwa njia rahisi tu kwa kubonyeza *106# utaingiza namba za kitambulisho chako cha NIDA pale, utaona namba zote zilizosajiliwa kwa jina lako; namba ambazo huzitambui niwaombe sana uende kwa wakala ukazifute” amesisitiza Ndugulile.

Wakati huo huo Ndugulile ameonya kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria mtu kumsajilia kadi ya simu mtu mwingine kwa kuwa ikiwa mtumiaji huyo aliesajiliwa kadi yake ya simu atatenda jinai ya namna yoyote aliemsajilia ataunganishwa kwenye jinai hiyo.

“Lakini sambamba na hili katika zoezi hilihili kuna wengine kwa bahati mbaya kwa kutojua alienda kwa wakala akaambiwa bonyeza weka alama yako ya kidole akaambiwa haisomi bonyeza tena, huo ni utapeli mwingine ambao unatumika, wanakwambia bonyeza kidole chako hakijasoma kumbe wanatumia alama zako za kidole kuwasajilia simu watu wengine na mawakala wasio waaminifu wanaziuza kwa watu wengine kufanya uhalifu” aliongeza Ndugulile.

Amewataka wananchi wanaosajili kadi zao za simu kutoweka alama ya kidole zaidi ya mara moja. 

Ndugulile aidha ameonya kuwa, kampuni yoyote ya simu itakayoruhusu usajili wa simu unaohusisha vitendo vya ulaghai kwa kusajili laini ambazo mlengwa hakuziridhia, adhabu itatolewa kwa kampuni hiyo.

Waziri Ndugulile amesisitiza kuwa ni muhimu kila Mwananchi akachukua tahadhari dhidi ya simu za ulaghai zinazopigwa na watu wanaonuia kutenda utapeli kwa kutopokea na kutendea kazi ujumbe huo unaotumwa na matapeli na badala yake wanapopata ujumbe huo wautume ujumbe huo pamoja na namba husika kwenda namba 15040 ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Tuna namba mahsusi ya kupokea ujumbe wa matapeli ambayo ni 15040, ili sasa na sisi huku kuna hatua ambazo tunaendelea kuzichukua” aliongeza Ndugulile.

Akizungumzia idadi ya laini za simu zilizosajiliwa Waziri Ndugulile amesema mpaka sasa kadi za simu zilizosajiliwa ni Milioni Hamsini na Mbili, kadi za simu zinazotumia huduma za intaneti Milioni Ishirini na Tisa na Kadi za simu zinazofanya miamala ya simu zaidi ya Milioni Thelathini na Mbili.

Aidha serikali imeonya kuwa haitaacha kuchukua hatua stahiki dhidi ya mtandao wowote wa simu unaoruhusu mawakala kufanya udanganyifu kwa kusajili laini za ziada ambazo mlengwa anaesajili hazitambui.

“Kuna maelekezo ambayo tumeyatoa kwa makampuni ya simu kupitia TCRA wewe uko mtandao mmoja unapigiwa simu na mtu mwingine wa mtandao mwingine, anaanza kukupa maelekezo kwa njia ya simu bonyeza hiki na hiki, usikubali, kampuni za simu watumie namba fupi ‘short codes’ ambayo ni 100, kuwasiliana na wateja wao” alisema na kuongeza Waziri Ndugulile.

Waziri amesisitiza kuwa ni muhimu kila mtumiaji wa Mawasiliano akatumia huduma za Mawasiliano kwa ajili ya kujiletea maendeleo na kwamba serikali kwa sasa inawekeza nguvu katika kutoa elimu na kuonya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya wanaotumia huduma za Mawasiliano kinyume na sheria za nchi.

Awali akimpokea Waziri Ndugulile kwenye banda la Mawasiliano, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha TCRA Bi. Lucy Mbogoro alimshukuru Waziri kwa kufika kwenye banda hilo na kuzungumza na wananchi juu ya zoezi la uhakiki wa usajili na usalama wa Mawasiliano.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!