JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Serikali Yawahimiza Wananchi Kuhakiki Usajili wa Laini za Simu ili Kuwa Salama Mtandaoni


Serikali Yawahimiza Wananchi Kuhakiki Usajili wa Laini za Si...

 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (MB) amesisitiza juu ya umuhimu wa wananchi kupata elimu stahiki juu ya matumizi sahihi ya huduma za Mawasiliano.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), katika viwanja vya Maonesho ya biashara ya kimataifa, Kigahe amesisitiza kuwa ni muhimu wananchi wakapata elimu ambayo inatolewa na Mamlaka hiyo juu ya matumizi sahihi ya huduma za Mawasiliano.

Kigahe aidha amesisitiza kuwa, ili kutokomeza matukio ya utapeli mtandaoni wananchi hawana budi kushirikiana na Mamlaka hiyo katika kutoa taarifa juu ya matukio ya kitapeli kwenye mtandao, ikiwemo jumbe fupi za kitapeli zinazotumwa kwa watumiaji huduma za Mawasiliano ili kuwalaghai.

Mamlaka ya Mawasiliano ilitoa namba maalum ambayo inamwezesha mtumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa juu ya ujumbe wowote wa kitapeli kwa kuutuma ujumbe huo kwenda namba 15040 ukihusisha namba ya mhusika anaefanya jaribio la utapeli kwa mtumiaji wa huduma za Mawasiliano.

Akiwa kwenye banda hilo Naibu Waziri aidha amepokea maelezo juu ya zoezi la uhakiki wa usajili wa laini za simu kwa mtumiaji huduma za Mawasiliano kwa kutumia namba maalum ya *106# inayomwezesha mtumiaji simu ya mkononi kupata maelekezo ya namna ya kuhakiki namba zilizosajiliwa kwa utambulisho wa namba za kitambulisho cha Taifa, na ikiwa kuna namba ambazo mtumiaji hazitambui anapaswa kuzifuta kupitia kwa wakala wa usajili wa simu anaeiwakilisha kampuni husika ya Mawasiliano.

“Kwa mfano hata mimi laini yangu nimerudia yaani kwenda kuhakiki na kuhakiki tena, tunategemea zile namba za utapeli zisiwe zinatumika tena” alisisitiza Kigahe.

Kigahe aliipongeza TCRA kwa kazi nzuri inayofanya ya kuelimisha umma juu ya matumizi salama ya huduma za Mawasiliano.

Maonesho ya 45 ya biashara ya kimataifa maarufu kama SabaSaba huwakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali wa kitaifa na kimataifa sambamba na taasisi ambazo hupata nafasi ya kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa kwa jamii.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!