TCRA na kampeni kabambe ya kuigeuza mitandao ya kijamii kuwa fursa

Dunia inakwenda kasi, na teknolojia inazidi kuimarika watu wanahabarika kupitia mitandao ya kijamii.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zinazofanya vizuri katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Na hii inachagizwa na ongezeko la watumiaji wa simu janja na huduma ya mtandao (intaneti) nchini.
Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema watumiaji wa intaneti mpaka kufikia Juni 2021 walikuwa milioni 29 sawa na asilimia 49 ya Watanzania.
Mitandao hii si tu majukwaa ya kimawasiliano, bali ni fursa katika ulimwengu wa leo ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla endapo itatumika vizuri.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa huduma za intaneti na simu janja, lakini matumizi ya mitandao ya kijamii yameendelea kuwa kitendawili kwa Watanzania wengi.
Wapo ambao wamekuwa wakiitumia mitandao hiyo kwa namna sahihi ambayo imekuwa ikiwanufaisha kama vile kibiashara, kikazi na kielimu na wale ambao wamekuwa wakiitumia ndivyo sivyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumeshuhudiwa kukithiri kwa matukio ya upotoshwaji wa taarifa, usambazaji wa maudhui yasiyo na maadili (picha na video za utupu na lugha za matusi) na udhalilishaji yanayofanywa mitandaoni.
Hii inaashiria kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuwepo kwa kundi kubwa la Watanzania ambao hawajui kutumia mitandao hiyo kwa malengo ya kunufaika.
Ikumbukwe kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yana athari kubwa kwa ustawi wa jamii ya sasa na hata baadaye kwa kuwa maudhui yanayopandishwa katika majukwaa hayo zinadumu vizazi kwa vizazi.
Kutokana na kadhia hiyo, TCRA imeamua kuja na kampeni kabambe iitwayo “Sambaza Mchongo na Sio Uongo” ambayo lengo lake kuu ni kudhibiti ongezeko la matukio haya katika mitandao ya kijamii katika njia ya kubadilisha mitazamo ya watu juu ya matumizi sahihi ya mitandao hiyo.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Jabiri Bakari anasema kuwa kampeni hii inafanyika ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na mwenendo huo ambao umekuwa ukiwaumiza watu wengi.
Kwa upande mwingine, TCRA inajielekeza kuwafungulia fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi watumiaji wote wa mitandao ya kijamii kupitia kampeni hiyo kama sehemu ya kuhanikiza matumizi sahihi ya mitandao hiyo inayopendwa na maelfu ya watu nchini.
“Kampeni hii ni kubwa na imebeba jumbe kuu nne ambazo ni; kuzuia usambazaji wa taarifa za uongo na uchochezi, uchukuaji wa uhalisia wa mtu mwingine kwa maslahi binafsi, usambazaji wa picha na video za utupu, vurugu au vitisho na Uonevu kwenye mtandao,” Dk Bakari anafafanua kuwa ni kosa kuchapisha kitu chochote kuhusu mtu mwingine bila ridhaa yake, pia ni muhimu kutoa taarifa kwa jeshi la polisi iwapo utapata shambulio la mtandaoni.
Kulingana na Dk Bakari, katika kipindi hichi cha kampeni tunaongeza elimu ya matumizi sahihi ya kijitali kwa wananchi na pia tunahamasisha wananchi wanaonunua bidhaa mitandaoni wanunue bidhaa hizo kwa watu wanaoaminika ili kuepuka kutapeliwa.
“Tutahakikisha kuwa tunatumia watu mashuhuri katika jamii, wahamasishaji, mashuhuda wa matumizi ya mitandao sambamba na vyombo vya habari kupaza sauti kuhusiana na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii,” anaeleza Dk Bakari ambaye anaongeza kuwa hiyo yote ni katika kuhakikisha mitandao ya kijamii inakuwa mahala salama zaidi na fursa kwa wananchi.
Imani ya Dk Bakari ni kuwa kampeni hii itafanikiwa kwa ushirikiano mkubwa wa wadau wote wa sekta ya mawasiliano na si mamlaka hiyo pekee, na kupunguza malalamiko ya watumiaji kupitia matumizi salama ya mitandao ya kijamii maana ni kosa kisheria kutumia vibaya mitandao ya kijamii.
Shuhuda za wanufaika wa mitandao ya kijamii
Mnufaika wa kwanza
Veronica Kundya ambaye ni mtaalamu wa biashara ya mtandaoni, ni moja kati ya watu wachache walioweza kubadilisha maisha yao kupitia biashara ya mtandaoni.
Ni mke na mama wa watoto wawili. Ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wa fani ya Sayansi ya Kompyuta.
Bi Veronica anasema safari yake ya biashara mtandaoni ilianzia tangu alipokuwa chuoni. Baadaye ilichagizwa na msukumo alioupata kutoka katika moja ya mikutano wa biashara ya mtandaoni aliyohudhuria kwa kipindi hiko.
“Wakati naanza sikuwa kabisa na mawazo ya kujiajiri nilikuwa sawa na watu wengine wanaopigiwa kelele wasome hadi chuo kikuu ili waweze kuajiriwa baadaye,” anaeleza Veronica.
Anasema tamanio la kufanya lilizaliwa alipokutana na moja ya watu waliomshawishi kufikira biashara hiyo akiwa bado chuoni.
“Wakati naanza biashara, sikuweza kujiamini, niliogopa, na nilichekwa sana, wazazi hawakuelewa na nililia nilipoona hata nilipoanza biashara haikuwa na mwenendo mzuri,” anaeleza.
Bahati nzuri nilikuwa nazungukwa na watu walionitia moyo, hivyo nilipambana na miezi minne baadaye nilianza kutengeneza kipato cha Sh3 milioni kwa mwezi.
Veronica anadai kuwa hayo yote yamewezekana kutokana na kutumia mitandao ya kijamii kwa malengo na si tu kuwasiliana.
“Ili uweze kufanikiwa kutumia mitandao kwa faida ni lazima uwe na malengo na kuzungukwa na watu wanaokusukuma kufikia lengo na si kila mtu,” anaeleza Veronica ambaye kwa sasa anapata wafuasi wapya 2000 kwa mwezi mtandaoni.
Veronica kwa sasa ni mjasiriamali mashuhuri wa bidhaa za kupunguza uzito wa mwili mtandaoni ambaye ameweza kubadilisha pia maisha ya Watanzania wengine wengi kupitia biashara yake hiyo.
Anasema kupitia biashara yake hiyo sasa anaweza kuyafikia masoko ya dunia nzima bila ya kuwa na duka rasmi.
Mnufaika wa pili
Philip Mbonde ni mjasiriamali wa utengenezaji keki kwa ajili ya sherehe za harusi, siku za kuzaliwa na matukio mengine.
Baada tu ya kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dar es Salaam alifikiria kujiajiri na kwa kuwa keki ilikuwa ni moja ya vitu anavyovipenda, ilikuwa rahisi kuanzisha biashara ya keki.
Mwaka 2009, kipindi ambacho mtandao wa Facebook ulikuwa gumzo duniani, Mbonde aliutumia kutangaza bidhaa zake za keki.
“Wakati ule, nilikuwa natangaza keki zangu katika ukurasa wangu wa Facebook kwa ajili ya kuwaonyesha watu wangu wa karibu kile ambacho napenda kufanya lakini haikuwa kibiashara,”anaeleza Mbonde.
Anasema kwa kadri muda ulivyozidi kwenda, kutokana na kuweka keki zake mtandaoni, watu walianza kuonyesha uhitaji na hapo akaanza kuutumia mtandao kibiashara rasmi.
“Ujio wa mtandao wa Instagram umesaidia kuongeza wafuasi wangu ambao naamini ndiyo wateja pia na mtandao huu ni rahisi kufikiwa na watu wengi tofauti na Facebook na mitandao mingine,” anafafanua zaidi.
Mbonde anakiri kuwa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ndiyo yamemuwezesha kusimama na kufikia hapo ambapo sasa anasambaza keki katika tafrija mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam.
“Ukiwa unazungukwa na watu wasio na malengo, watu ambao wanathamini maisha yao tu na si vitu vingine katika mitandao basi hautakuwa na muda kusonga mbele,” ndivyo anavyoamini Mbonde.