JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Asisitiza Ushirikiano na TCRA ili Kuhakikisha Mitandao Salama


Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Asisitiza Ushirikiano na TC...

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amesisitiza kuwa, Jeshi analoliongoza litaendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), katika  kuhakikisha watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania, yakiwemo ya intaneti, simu na Ujumbe wa maandishi  wanasalia salama wakati wote wanapotumia huduma hizo.

Alibainisha hayo wakati alipotembelea banda la maonesho la TCRA kwenye viwanja vya maonesho ya 46 ya biashara, barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa,  hakuna mtu yeyote anaeweza kufanya uhalifu kwenye  mtandao asipatikane kwani Jeshi kwa ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano wamejidhatiti kuwadhibiti watumiaji wanaoharibu usalama kwenye mazingira ya kimtandao.

“Hakuna namna unaweza kufanya uhalifu mtandaoni na usipatikane, na bahati mbaya utaadhirika kwa familia yako na jamii, kwa sababu utakamatwa tu, hivyo nawaasa sana watanzania wenzangu tujiepushe na utapeli mtandaoni” alionya IGP Sirro na kuongeza.

Alitoa wito kwa TCRA kutoa elimu zaidi kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano akibainisha kuwa hiyo ndiyo njia sahihi na muhimu zaidi ya kupunguza matukio ya uhalifu mtandaoni.

“TCRA najua wamejipanga na sisi Jeshi la Polisi pia tumejipanga,suala muhimu ambalo ningependa kuwashauri ni kwamba tuendelee kutoa elimu, tuna watu wetu wengine wanatenda uhalifu bila kujua kwamba ni uhalifu kwenye mtandao; hivyo elimu ni jambo la msingi sana”, alisisitiza IGP.

Awali, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Semu Sauli Mwakyanjala, akimkaribisha IGP Sirro bandani hapo alimweleza kwamba TCRA imeendelea na jitihada ya kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi na salama ya huduma za Mawasiliano na kwamba imeweka utaratibu wa watumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa ya uhalifu kupitia namba maalum, sambamba na kuwataka watumiaji wote wa huduma za mawasiliano ya simu kuhakiki laini za simu zilizosajiliwa kwa namba za kitambulisho cha Taifa.

“Kamanda, TCRA tuna utaratibu unaomwezesha mtumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa ikiwa atapokea ujumbe au simu ya utapeli kw kutuma namba ya tapeli kwenda namba 15040, utaratibu huu tunautekeleza kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi na Watoa Huduma umesaidia sana kupunguza ripoti za uhalifu” Semu alimweleza IGP.

Aliongeza kuwa, watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapaswa kuhakiki usajili wa laini zao za simu kwa kubofya *106# ili kusalia salama akisisitiza kuwa hatua hiyo inamwezesha mtumiaji kufuta namba asiyoitambua kupitia wakala wa mtoa.

Mbali na banda la TCRA Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini, alizuru mabanda kadhaa ya maonesho ya biashara likiwemo banda la Zanzibar linalojumuisha Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wajasiriamali wa visiwa vya karafuu.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!