JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mchango wa TEHAMA katika Kuimarisha Kilimo Kama Nguzo Mama Ya Uchumi


Mchango wa TEHAMA katika Kuimarisha Kilimo Kama Nguzo Mama Y...

 

Pasina tashwishi yoyote kilimo ndiyo nguzo mama ya uchumi wa Tanzania sekta ambayo inasaidia zaidi ya watu milioni 40. Sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania hulimwa na wakulima wadogo; Wizara ya Kilimo inakadiria kuwa sekta inatoa ajira kwa asilimia zaidi ya sitini.

Ni muhimu kujikumbusha kuwa Dira ya Maendeleo ya Tanzania imeweka lengo katika kuhakikisha kilimo kinatoa mchango chanya katika ukuaji wa maendeleo endelevu. Aidha kwa kuzingatia zama hizi za ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ni kweli kwamba Teknolojia hii itawezesha pakubwa ukuzaji sekta ya kilimo kwa manufaa ya ukuzaji maendeleo endelevu ya wananchi na Taifa.

Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO) linabainisha kuwa idadi ya watu ulimwenguni inatarajiwa kuzidi bilioni 9 ifikapo mwaka 2050, na kwamba sekta ya kilimo itapaswa kuongeza uzalishaji wa chakula chenye lishe mara dufu, ili kukidhi mahitaji hayo yanayoongezeka kila uchao na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wote, kote duniani; Tanzania ikiwemo.

Aidha sekta ya kilimo inapaswa kuzalisha ajira, kuboresha mapato na kuchangia kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa wananchi hasa waishio vijijini na kubwa zaidi kutanua wigo wa ajira kwa kundi la vijana ambalo linaongezeka kwa kasi.

TEHAMA, inarahisisha mawasiliano baina ya mkulima na masoko kwa kuzingatia ukweli kwamba mkulima anaweza kupata taarifa za masoko na huduma nyingine sokoni kama vile viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni, msimamo wa bei za mazao katika soko la ndani na nje, usafirishaji, ushuru nakadhalika kwa urahisi kupitia miundo wezeshi ya mawasiliano.

Fursa ya upatikanaji wa taarifa za masoko kupitia huduma za TEHAMA si tu itamwezesha mkulima kuongeza tija kwenye shughuli za kilimo Lakini pia itawezesha mkulima kubainisha fursa mpya zinazoambatana na biashara katika kilimo ikiwemo usindikaji, usafirishaji na huduma ndogo za kifedha kwenye sekta ya kilimo.

FAO linabainisha kuwa karibu asilimia 40 ya idadi ya watu ulimwenguni wanafikiwa au kuunganishwa na huduma za mtandao wa intaneti suala ambalo linamaanisha kwamba mtandao wa masoko katika zama za sasa unaweza kuwaunganisha wakulima, wauzaji na wanunuzi kwa urahisi zaidi kupitia mtandao kote duniani.

Nchini Tanzania wakulima wameonyesha uthubutu wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kwa kujikita katika kilimo cha kisasa; bidhaa mbalimbali za kilimo zikiwemo za matunda na mbogamboga, nafaka na kadhalika kwa mfano zimekuwa zikizalishwa kwa njia ya kisasa. Mfano hai ni wakulima katika mikoa ya Njombe, Iringa,Kilimanjaro, Kagera na Mbeya ambao wamegundua fursa zilizomo kwenye kilimo cha matunda ya parachichi na tofaa ambayo yana fursa kubwa ya masoko kimataifa kwa kulima na kufungasha kisasa.

Ili kuteka soko la kimataifa kwa mfano kwa wakulima hawa wamekuwa wakitumia TEHAMA ili kupata taarifa halisi za bei ya bidhaa wanayozalisha sambamba na kugundua masoko mapya  ili wauze kwa faida TEHAMA inachukua nafasi ya umuhimu wa kiwango cha juu.

Aidha TEHAMA inayo nafasi ya kuwaunganisha wakulima na vyama vyao vya Ushirika ili kupata taarifa mbalimbali kutoka menejimenti za vyama hivyo kuhusu mwenendo wa bei ya bidhaa wanazozalisha na taarifa muhimu za ughani na pembejeo.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pia inayo nafasi katika kuhakikisha TEHAMA inakuwa mwimo wa ukuaji wa sekta ya kilimo nchini; TCRA imekuwa ikihakikisha huduma za TEHAMA kwenye sekta zote ikiwemo ya kilimo inakua kwa kiwango kinachopasa kwa kushirikiana na watoa huduma ambao hupatiwa leseni ya kutoa huduma zinazohusiana moja kwa moja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. TCRA aidha huhakikisha huduma za TEHAMA zinakidhi ubora ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za TEHAMA wanapata huduma yenye viwango stahiki.   Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Jabir Kuwe mara kadhaa amekuwa akisisitiza kuwa TEHAMA ndiyo msingi muhimu wa kukuza uchumi wa kisasa (uchumi wa kidijitali) ambao unategemea sekta ya mawasiliano iliyoboreshwa kwa kiwango stahiki.

Hivi karibuni tu Shirikisho la Taasisi za TEHAMA Afrika Mashariki (EACO) kupitia kwa Katibu Mtendaji wake Daktari Yahya Simba lilibainisha mkakati wake katika kuhakikisha wakulima wadogo kwenye nchi wanachama wa Afrika Mashariki wananufaika na fursa za matumizi ya TEHAMA kwenye kuongeza tija katika kilimo kwa kutambua mchango wa teknolojia hiyo katika ukuzaji sekta ya kilimo. EACO tayari imeanza kuwaunganisha wakulima wadogo walioko kwenye vyama vya ushirika katika matumizi ya TEHAMA kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuanzia na Rwanda ikifuatiwa na nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ikiwemo.

Mfumo wa pamoja wa taarifa za masoko ni fursa nyingine inayoletwa na matumizi ya TEHAMA kwenye kilimo, unawezesha wakulima kupata taarifa za masoko sambamba na kuwawezesha wafanyabiashara kupata taarifa za upatikanaji wa bidhaa za kilimo kwa urahisi na hivyo kukuza tija kwenye shughuli za kilimo kwa kuwa mkulima ataweza kupata taarifa zote muhimu zikiwemo bei za bidhaa anazozalisha kupitia aplikesheni moja inayotoa taarifa zote za masoko kuja kwa mkulima na mnunuzi kupata taarifa za bidhaa zinazozalishwa.

TEHAMA imebadilisha jinsi biashara, watu na serikali zinavyofanya kazi. Imesaidia pakubwa kupunguza gharama za manunuzi na kuwezesha mawasiliano na ni nyenzo muhimu katika kufikia azma ya serikali ya Tanzania kujenga uchumi wa kidijitali.

Aidha wakulima wanaweza kupata taarifa mbalimbali kupitia midia tofauti kama vile video, maandishi, picha na vielelezo; aidha TEHAMA imesaidia kupunguza gharama za upatikanaji wa taarifa na huduma huku ikikuza ufanisi na ujumuishaji wa wakulima na wataalam wa kilimo pamoja na wanunuzi. TEHAMA inawezesha kazi nyingi kwenye sekta ya kilimo kufanyika kwa wakati mmoja na gharama nafuu huku ikiokoa muda wa upatikanaji huduma mbalimbali zikiwemo huduma za kifedha, masoko, ushauri katika shughuli za kilimo, utafiti na ujifunzishaji.

Katika ripoti yake ya mwaka 2017 kuhusu TEHAMA na Kilimo FAO linasema kuwa nchi zilizoendelea sekta ya kilimo imekuwa ikitumia vilivyo fursa na huduma zinazopatikana katika TEHAMA kukuza kilimo na hatimae kuongeza tija ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za teknolojia mpya katika kilimo, masoko-mtandao na taarifa za kisera hivyo kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani katika soko la bidhaa za kilimo.

Hatua ya serikali ya Tanzania katika Bajeti ya 2021/22 kufuta kodi ya vifaa vya mawasiliano itawezesha kukuza tija katika matumizi ya TEHAMA kwenye kilimo kwa kuwa wananchi wengi sasa watapata fursa ya kupata vifaa vinavyowezesha matumizi ya TEHAMA hivyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa ikiwemo elimu ya kilimo bora chenye tija kwa mkulima sanjari na kuwawezesha wafanyabiashara kufahamu hali halisi ya upatikanaji wa bidhaa shambani.

Mfano wa mifumo ya TEHAMA ambayo ni muhimu kwa ukuzaji wa matumizi ya TEHAMA katika kilimo ni pamoja na kuwepo kwa Mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa taarifa za bei ya mazao, pembejeo na usafirishaji bidhaa za kilimo kutoka shambani kwenda sokoni. 

Katika ulimwengu unaoendelea, matumizi ya TEHAMA kwenye kilimo ni muhimu katika kupunguza mkwamo wa upatikanaji taarifa na uratibu wa gharama za uzalishaji kwa mkulima. Kuenea kwa simu za rununu katika maeneo ya vijijini tayari kumesababisha mabadiliko muhimu katika sekta ya kilimo na bado hitajio la elimu zaidi kwa wakulima hasa maeneo ya vijijini juu ya matumizi sahihi ya huduma za TEHAMA ni suala linalopaswa kuwa endelevu na kutekelezwa kwa dhati ili Tanzania ifikie lengo la uchumi wa kidijitali ambao unatafsiri hali halisi ya uchumi wa dunia ya sasa.

Matumizi ya huduma za TEHAMA hasa matumizi ya simu za rununu, yanasaidia kuongeza ufikishaji wa habari na fursa za kujenga uwezo kwa wakulima vijijini. Hii inaleta faida zinazoonekana. Wakulima wanaweza kuongeza tija kwa kuwa na mavuno mengi ya mazao, kwani wanapata habari kwa muda mfupi juu ya njia bora za uzalishaji na hali ya mazingira na soko kupitia TEHAMA.

TEHAMA inawezesha kukuza ujifunzaji, suala linalowezesha wakulima kupata elimu ya teknolojia mpya au iliyoboreshwa katika kilimo pia kufahamu juu ya njia sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea na mifugo. Aidha TEHAMA inawezesha kuwaunganisha wakulima na maafisa ughani waliopo maeneo jirani nao au mbali ili kutoa huduma ya ushauri katika kilimo chenye tija.

Tunapobainisha umuhimu wa TEHAMA kwenye shughuli za kilimo ni muhimu kusisitiza matumizi miongoni mwa wananchi kwa kiwango cha kuridhisha ili kuhakikisha teknolojia ya mawasiliano inakuwa yenye manufaa, hatua ambayo serikali imekuwa ikitekeleza kwa kuhakikisha wananchi wanabainisha fursa zilizomo kwenye mtandao. Serikali imeweka bayana kuwa tayari idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania wamefikiwa na huduma ya mawasiliano, kama alivyobainisha Waziri Ndugulile mwezi Julai mwaka huu wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar es salaam.

"Sisi kama Serikali tunaamini mawasiliano ni haki ya kila Mtanzania, na hapa ninavyoongea na ninyi asilimia 94 ya Watanzania tumewafikia kwa njia ya mawasiliano.Katika eneo la kijiografia la Tanzania zaidi ya 60 tumeifikia na mawasiliano” alibainisha Waziri Ndugulile wakati alipozuru banda la Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwenye Maonesho ya SabaSaba 2021 yaliyofanyika Dar es salaam.

EACO, FAO na Umoja wa Mataifa kupitia Chama cha kimataifa cha mawasiliano (ITU) vinaamini kwamba ili mataifa yaweze kufikia uchumi wa kidijitali, kilimo ndio nguzo mama ikisaidiwa kwa karibu sana na TEHAMA kwa kuzingatia zama za biashara ya aina yoyote duniani kwa sasa inabebwa na teknolojia hiyo.

Wadau wengi wanakubali hitajio la mkakati wa kitaifa wa kilimo-mtandao hatua ambayo jumuiya za kimataifa za FAO-ITU katika mwongozo wao wa pamoja juu ya kilimo mtandao wanabainisha fursa lukuki zinazoweza kupatika kwenye matumizi sahihi ya kilimo-mtandao (e-agriculture). Mikakati ya kilimo-mtandao inasaidia kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima katika maeneo ya huduma za ughani, upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora, kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya kilimo na zaidi. Mikakati kama hiyo pia itasaidia kuunda mito mipya ya mapato na kuboresha maisha ya jamii ya vijijini na pia kuhakikisha kuwa malengo ya mpango mkuu wa kitaifa wa kukuza uchumi wa kidijitali unafanikiwa.

Kwa muhtasari ni kwamba TEHAMA inayo nafasi ya kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaojihusisha na shughuli za kilimo vijijini wakiwemo vijana na wanawake ili kuwapa fursa mpya za biashara hivyo kuboresha maisha yao; TEHAMA inatanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha miongoni mwa wakulima hivyo kupunguza hasara na upotevu wa rasilimali fedha unaosababishwa na ufuatiliaji wa fedha mbali na maeneo waliyopo; TEHAMA inafanikisha upatikanaji wa takwimu zenye viwango katika sekta ya kilimo zinazoweza kuiwezesha serikali kupanga mipango na mikakati ya kuboresha zaidi sekta hiyo kwa maendeleo ya nchi; TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa masoko miongoni mwa wakulima na kurahisisha wafanyabiashara kupata bidhaa za kilimo bila vikwazo vingi; TEHAMA hurahisisha upatikanaji wa taarifa za kufanyiwa kazi miongoni mwa wakulima zikiwemo taarifa za kitaalam kwenye kilimo au ufugaji; TEHAMA inawezesha utekelezaji wa mkakati wa pamoja wa kitaifa juu ya utunzaji mazingira wakati wa shughuli za kilimo; TEHAMA huziba ufa uliopo baina ya watafiti,wakulima,masoko na serikali hivyo kuboresha mnyororo wa thamani kwenye shughuli za kilimo; TEHAMA huwezesha utekelezaji wa sera, Sheria na kanuni zinazolinda sekta ya kilimo na TEHAMA ni nyenzo katika kazi za kilimo kama vile husaidia umwagiliaji, kuuwa vijidudu waharibifu na teknolojia nyinginezo zinazotumia programu tumizi ambazo hutumika katika kazi za kilimo.

Matumizi ya TEHAMA ni muhimu kutiliwa mkazo na kipaumbele cha juu kwa kuanzia katika ngazi ya elimu ili kuhakikisha TEHAMA inaleta mchango chanya wenye ukuzaji uchumi wa Tanzania, katika shabaha ya kukuza uchumi wa kidijitali na kufikia azma ya Maendeleo Endelevu.   

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!