JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Nchi Wanachama, zamchagua Doreen Bogdan-Martin kuwa Katibu Mkuu Mtendaji,ITU


Nchi Wanachama,  zamchagua Doreen Bogdan-Martin kuwa Katibu...

 

Nchi Wanachama wa Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) wamemchagua Doreen Bogdan-Martin wa Marekani kuwa Katibu Mkuu ajaye wa shirika hilo. Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama 193 zilizoshiriki Uchaguzi huo unaoamua hatima ya sekta ya Mawasiliano ulimwenguni.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye (Mb.) ameongoza ujumbe wa wataalamu wa Mawasiliano kwenye Mkutano huo wakiwemo wataalamu wa Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Bogdan-Martin atakuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza ITU, ambayo ilianzishwa mwaka 1865 na kuwa wakala maalumu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1947.

Uchaguzi huo ulifanyika Septemba 29, 2022 wakati wa Mkutano huo al’maarufu kama Plenipotentiary wa ITU (PP-22) huko Bucharest, Romania, siku ya Alhamisi, huku wawakilishi wa Nchi Wanachama wakipiga kura wakati wa kikao cha asubuhi cha mkutano huo. Bogdan-Martin alishinda nafasi hiyo kwa kura 139, kati ya kura 172 zilizopigwa.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa Bogdan-Martin alisema. "Dunia inakabiliwa na changamoto kubwa - migogoro inayoongezeka, mgogoro wa hali ya hewa, usalama wa chakula, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na watu bilioni 2.7 wasio na mtandao. Ninaamini sisi, ITU na wanachama wetu, tuna fursa ya kutoa mchango wa kuleta mabadiliko. Ubunifu unaoendelea duniani hivi sasa unaweza na utawezesha utatuzi wa changamoto nyingi," alisisitiza.

Bogdan-Martin ataanza muhula wake wa miaka minne kama Katibu Mkuu wa ITU tarehe 1 Januari 2023.

Katibu Mkuu mteule ameahidi "kuendelea kuendesha taasisi hiyo kuwa ya ubunifu na inayozidi kuwa muhimu kwa Nchi Wanachama, kuweka nafasi nzuri zaidi katika kukumbatia mazingira ya ukuzaji teknolojia za kidijitali ulimwenguni.

Mkutano huo pia utachagua Baraza-Tendaji litakalosimamia utekelezaji wa Sera, Mipango na Mikakati ya ukuzaji sekta ya Mawasiliano duniani kwa miaka minne kuanzia 2024 hadi 2027; huku ajenda ya msingi ikiwa kuhakikisha wakazi wa sayari dunia wanaunganishwa na huduma za Mawasiliano zenye uhakika na ubora.

 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!