JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Ujumbe wa Taasisi ya Mawasiliano ya Kitaifa ya Msumbiji Wajifunza kutoka TCRA


Ujumbe wa Taasisi ya Mawasiliano ya Kitaifa ya Msumbiji Waji...

 

Ili kuimarisha ufahamu wao wa udhibiti na usimamizi wa sekta ya mawasiliano, ujumbe kutoka Taasisi ya Mawasiliano ya Kitaifa ya Msumbiji (INCM) hivi karibuni ulifanya ziara ya kujifunza ya siku tatu katika Ofisi ya makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Ziara hiyo, ambayo ilifanyika kuanzia Jumatatu, Septemba 4, hadi Jumatano, Septemba 6, 2023, iliwawezesha ujumbe huo kupata ufahamu na uelewa zaidi wa masuala katika nyanja mbalimbali za usimamizi wa mawasiliano, zikiwemo huduma na bidhaa zinazohusiana na sekta hiyo.

Ujumbe wa Msumbiji uliojumuisha maafisa waandamizi wa INCM, ulifika Tanzania kujifunza masuala mbalimbali yakiwemo utoaji wa leseni, usimamizi wa huduma za mawasiliano na huduma za mtandao, na ugawaji wa rasilimali kwa ufanisi ndani ya mfumo wa udhibiti na usimamizi wa mawasiliano.

Aidha ujumbe huo ulishirikiana na wenzao wa TCRA kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa sekta huku ziara hiyo ikilenga kuwawezesha INCM na TCRA kuboresha zaidi mbinu za kitaalamu za usimamizi wa sekta ya mawasiliano kwenye nchi hizo mbili majirani.

Walipowasili makao makuu ya TCRA jijini Dar es Salaam, ujumbe ulikaribishwa kwa upendo na ujirani Mwema na ndugu Modestus Ndunguru, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, ambaye aliwakaribisha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari; mara baada ya utambulisho wataalamu wa vitengo mbalimbali vya TCRA walishirikiana na wataalamu hao kubadilishana uzoefu.

Katika kipindi cha ziara yao ya siku tatu, ujumbe wa Msumbiji ulipata fursa ya kujifunza kwa undani masuala mbalimbali ya usimamizi wa mawasiliano. Walijifunza kuhusu usimamizi wa Usalama mtandaoni, utoaji wa leseni za mawasiliano, usimamizi wa mawasiliano ya simu na Intaneti, huduma za Utangazaji na posta.

Helena Fernandes, Mjumbe wa Bodi ya Utendaji ya INCM na kiongozi wa ujumbe, huo akitoa shukrani zake mwishoni mwa ziara hiyo aliipongeza TCRA kwa ukarimu wao na ufahamu kamili uliowekwa wazi wakati wa ziara hiyo ambao wamefanikiwa kuupata.

"Tunawashukuru sana TCRA kwa ukaribisho wao; tumejifunza mambo mengi muhimu kwa utendaji wetu na tunakwenda nyumbani kuyatendea kazi,” alibainisha. Aliongeza kuwa, “miongoni mwa mambo yaliyotupa mafunzo mapya ni pamoja na namna TCRA walivyofanikiwa kutoa leseni za mawasiliano kwa mfumo wa TEHAMA bila kuwalazimu wanaohudumiwa kufika ofisini moja kwa moja; sisi bado tuna mfumo wa zamani, funzo tulilopata hapa tunakwenda kulifanyia kazi,” alibainisha Fernandes.  

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikipokea ugeni wa taasisi zinazofanya kazi kama ya Mamlaka hiyo kutoka nchi za Kusini na Kaskazini mwa bara la Afrika ambapo mwaka 2022 pekee zaidi ya Mamlaka Tano zilifika TCRA kwa ziara za mafunzo zikiwemo Malawi, Msumbiji, Zambia, Botswana, Rwanda na Burundi.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!