JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Rais Samia Aipongeza TCRA Kwa Kazi Nzuri ya Usimamizi wa Mradi wa Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU)


Rais Samia Aipongeza TCRA Kwa Kazi Nzuri ya Usimamizi wa Mra...

 

Rais wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta barani Afrika (PAPU) lililojengwa eneo Philips Arusha. Katika hotuba yake aliyowasilisha baada ya zoezi la uzinduzi Rais Samia aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kazi yake nzuri katika usimamizi na ufadhili wa mradi kwa niaba ya Serikali ikishirikiana na PAPU.

“Kukamilika kwa jengo hili la ghorofa 17, ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania yaani TCRA na Umoja wa Posta Afrika yaani PAPU; huu ni mradi wa ubia uliogharamiwa na PAPU kwa asilimia 60 na TCRA ikiiwakilisha Serikali yetu kwa asilimia 40,” alisema na kuongeza “…nawapongeza sana TCRA na PAPU kwa kukamilisha mradi huu mkubwa sana,” alibainisha Rais Samia.

Jengo hilo lililojengwa kwa kuzingatia teknolojia ya hali ya juu na ya kisasa inayohakikisha utunzaji wa mazingira na matumizi salama na kidogo ya nishati lina ukubwa wa mita za mraba 22,421 ambapo litakuwa makao makuu ya PAPU, pia litakuwa na ofisi ya TCRA inayohudumia mikoa ya Kanda ya Kaskazini. “Aidha humu ndani kuna nafasi za vyumba vya biashara, mikahawa, na kumbi za mikutano zenye viwango vya kimataifa zikiwa na uwezo wa kuchukua makumi hadi mamia ya washiriki huku zikiwa na teknolojia ya kisasa sana ya mikutano” alibainisha Afisa Mkuu wa Mawasiliano wa PAPU Bw. Oyuke Phoustine.

Sherehe ya uzinduzi ilihudhuriwa na maafisa wa serikali, wawakilishi kutoka Umoja wa Posta Duniani (UPU) Wawakilishi kutoka nchi wanachama wa PAPU, Bodi na Menejimenti ya TCRA, maafisa wa serikali, na wananchi wakazi wa Arusha.

Katika hotuba yake, Rais Samia alitoa changamoto kwa PAPU, akiwataka kutumia fursa ya kituo cha kitega uchumi kuboresha uwezo wao wa kiuchumi, kuchagiza ukuzaji wa maarifa miongoni wanachama wa PAPU, kuchochea uvumbuzi, na kuboresha utendaji wa huduma za posta katika bara la Afrika.

Pia aliishukuru Arusha Gymkhana Club kwa kutoa kwa ukarimu eneo la ardhi ambalo liliruhusu upanuzi wa kituo hicho na kuwezesha ujenzi wa barabara inayowezesha kulifikia jengo hilo upenuni.

"Uzinduzi wa makao makuu ya PAPU ni mafanikio makubwa kwa sekta ya posta barani Afrika, ukiashiria azma thabiti ya serikali yetu " alisema Bwana Chrysostom Pallangyo, mkazi wa Arusha aliyehudhuria sherehe hiyo ya uzinduzi. Aliongeza kuwa, amefurahishwa na uwekezaji huo wa kipekee mjini Arusha, akibainisha kuwa "jengo hili la kisasa limeongeza uzuri wa jiji letu linalopendwa na watalii."

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!