JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mfumo wa Anwani za Makazi ni Muhimu Katika Kukuza Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi, Tanzania.


Mfumo wa Anwani za Makazi ni Muhimu Katika Kukuza Maendeleo...

 

 Mfumo wa Kitaifa wa anwani za makazi na msimbo wa Posta ni mfumo muhimu wa anwani na utambulisho wa mkazi, biashara na kwa sababu unatambulisha anwani ya kila mtu, iwe ni mahali pa kazi,makazi au eneo la biashara. Mfumo huu wa anwani unabainisha eneo sahihi la makazi ya mtu, pamoja na eneo la biashara yake au ofisi. Mfumo huu, unafanya kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo, na postikodi— huu ni mfumo maalum ambao pia unatunzwa kidijitali uaotambulisha eneo ambalo huduma za posta na huduma mbalimbali zikiwemo za kijamii, dharura na kibiashara zinafikishwa kwa mlengwa bila vikwazo; mfumo huu unaliunganisha taifa kuanzia ngazi ya kitongoji au mtaa, kijijini, kata, wilaya, mkoa na taifa.

Nchini Tanzania, mradi wa anwani za makazi unatekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano, utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi na utekelezaji wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala.

Meneja Huduma za Posta katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Haruni Lemanya, katika mazungumzo na Mwandishi wa Makala hii aliutaja mfumo huo kuwa muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini na kwamba mara baada ya zoezi kukamilika Tanzania itawanufaisha wananchi wake pakubwa kwa Kuwezesha utoaji huduma mbalimbali kwa urahisi. Anuani za makazi na mfumo wa posta, alisisitiza, utafanya nchi kufikiwa zaidi na kuruhusu watu kushiriki katika uchumi wa kidijitali. Kimsingi hata huduma muhimu za kisasa kama vile usafiri wa Taxi uliozoeleka kutumia Tehama katika siku za hivi karibuni utakuwa rahisi zaidi mara baada ya mfumo huu kukamilika kwani maeneo yote ya makazi yatatambuliwa.

Mfumo huo utasaidia Watanzania kufanya biashara wao kwa wao na nchi za nje kwa sababu kutakuwa na njia ya kisasa zaidi ya kupata bidhaa, fedha na mizigo mingine kwenda pale inapostahiki pasipo vikwazo vingi, tofauti na hali ilivyo kabla ya kuwekwa mfumo huo. Tofauti na siku za awali, wakati suala la anwani lilikuwa la mtu binafsi, mfumo wa anwani za makazi wa sasa unaruhusu kila mtu kuwa na anwani halali ya makazi.

Wageni wataweza kutambua wanakoenda kwa urahisi zaidi badala ya kuuliza mara kwa mara kupata maelekezo ya uelekeo suala ambalo wakati mwingine huchagiza jinai ikiwemo uporaji na wizi kwa wageni wakiwemo watalii.

Mfumo huu wa anwani za makazi unazingatia viwango vilivyowekwa na Umoja wa Posta Ulimwenguni (UPU), Umoja wa Posta wa Pan-African (PAPU), na mashirika mengine yanayotambulika kimataifa kama vile Shirika la Viwango vya Kimataifa ISO ambayo yote pamoja na mengine huweka utaratibu Maalum wa misimbo ambayo ni rasilimali muhimu katika kukamilisha uwekaji wa anwani za makazi katika nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwemo.

Tanzania imekuwa ikizingatia taratibu hizi na ndiyo sababu nchi nzima ina utaratibu sawia wa anwani za makazi unaofuata utaratibu uliokubaliwa Kitaifa na Kimataifa. Tanzania ina Mwongozo wa Anwani za Makazi unaotolewa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI (unapatikana kwenye tovuti hii) ukielekeza hatua na taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuweka Anwani za Makazi nchini. Mwongozo huo ndiyo unatumiwa hivi sasa wakati wa uwekaji wa anwani za makazi, zoezi linaloendelea kote nchini mwaka huu wa 2022.

 “Vyombo vyote hivi vya Kimataifa ni msingi wa ushirikiano kati ya watoa huduma za posta duniani, jambo ambalo linasaidia kujenga mtandao wa kimataifa wa uhakika unaohakikisha utoaji wa huduma za kisasa za posta na anwani,” aliongeza na kusisitiza Lemanya. Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa Mwongozo wa anwani na taratibu zilizokubaliwa Kimataifa katika anwani za makazi na msimbo alifafanua kuwa “utaratibu huu ni muhimu kuzingatiwa kwa sababu unaondoa uwezekano wa migogoro na utoaji wa majina bila mpangilio na utoaji wa anwani."

Mwongozo wa anwani za makazi umeelekeza kwamba utaratibu wa kutaja mitaa na barabara utaanza katika ngazi ya kijiji, hadi ngazi ya kata, na hatimaye hadi ngazi ya wilaya, ambapo uamuzi wa mwisho ya majina ya mitaa na barabara yaliyopitishwa katika wilaya Fulani unaweza kuridhiwa katika ngazi ya Wilaya kwa namna ilivyoelekezwa na Mwongozo huo au kwa kadri utaratibu wa kiuongozi utakavyotolewa. "Mtazamo shirikishi katika suala la kutaja mitaa na barabara ni muhimu sana kwa sababu barabara na mitaa ni miundombinu ya umma; na anwani za makazi ni suala linaloathiri jamii nzima,hivyo ushirikishwaji ni suala muhimu sana" alisisitiza Lemanya.

Februari mwaka huu, wakati wa kikao cha kazi na Wakuu wa Mikoa mjini Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan pia alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua ya mradi wa anwani za makazi. “Kwa hiyo, tukiwashirikisha wananchi ipasavyo, zoezi hili litakuwa rahisi na la gharama nafuu kuliko tulivyotarajia,” alisisitiza Rais Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wakuu wa Mikoa.

Ili kuepusha mivutano inayoweza kujitokeza baina ya watu wa makundi mbalimbali kuhusu kutaja majina ya Barabara, mwongozo umebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya na wananchi kupitia uongozi wao wa ngazi za chini, watatoa orodha ya majina na barabara zilizoidhinishwa. Serikali katika ngazi ya Wilaya itakuwa na jukumu la kutoa taarifa kwa wadau wote kuhusu majina ya mitaa yaliyoidhinishwa na kujumuisha orodha hiyo kwenye Daftari la Kudumu la Barabara.

Faida za Anwani za Makazi

Anwani za makazi zina faida lukuki awali ni kurahisisha utoaji huduma ambazo ni pamoja na ulinzi, kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wananchi na Serikali au sehemu za huduma, kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za kijamii, kibiashara na huduma za dharura na uokoaji.

Nyingine ni kurahisisha sensa, kuboresha daftari la wapigakura, huduma za posta na kuwezesha utoaji wa biashara mtandao na pia kurahisisha ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya Serikali.Mfumo wa anwani unayo manufaa kwa ukuaji wa biashara. Anwani za makazi zitasaidia wafanyabiashara kutambua maeneo ya kufikisha bidhaa na kuchukua malighafi kwa ajili ya uzalishaji viwandani na kibiashara kwa ujumla katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kama vile soko la Kariakoo jiji Dar es salaam. Kimsingi, aina zote za biashara zinahitaji anwani. Takriban kila biashara lazima ishughulike na wachuuzi, ndiyo maana makampuni yanahitaji maelezo ya wasambazaji wa bidhaa na huduma ambao wanaweza kufikiwa au kufikisha huduma zao ikiwa kuna mfumo mzuri wa anwani. “Mfumo huu pia utasaidia ukuaji wa biashara na ujasiriamali” alisisitiza Lemanya.

Anwani za wateja zinahitajika kwa karibu kila biashara: biashara zenye utaratibu na mpango Thabiti wa ukuaji huweka rekodi za wateja wao; ili kutunza kumbukumbu hizo, ni muhimu wateja hawa wawe na anwani ili kuwawezesha wafanyabiashara kuwafikia na kuwafikishia bidhaa bila kuwa na wateja kwenda maeneo ya biashara. Utaratibu huu unasaidia biashara kukua na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato na maduhuri.

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imejiwekea lengo la kukamilisha mradi wa anwani za makazi katika mikoa yote ifikapo Mei 2022, ikiwa ni maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Agosti 2022. Katika kikao-kazi na Wakuu wa Mikoa mnamo Februari 2022 Rais Samia alisisitiza kuwa mfumo huu wa anwani utafaa sana katika kuwezesha uendeshaji wa zoezi la sensa, kuipatia Tanzania takwimu sahihi za watu na makazi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya nchi na watu wake.Zaidi ya hayo, Rais Samia alisisitiza kwamba, utekelezaji mzuri wa mradi wa anwani utaitambulisha Tanzania kwenye mtandao wa ulimwengu wa kisasa na kuhakikisha malengo ya Tanzania kujenga uchumi wa Kidijitali yanafikiwa. 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!