JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Serikali yaendesha Mafunzo ya Kujenga Uelewa Kuhusu Uchumi wa Kidijitali


Serikali yaendesha Mafunzo ya Kujenga Uelewa Kuhusu Uchumi w...

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendesha mafunzo ya kujenga uelewa kwa viongozi wa Serikali kuhusu uchumi wa kidijitali

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Hussein Katanga amefungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu uchumi wa kidijitali. Mafunzo hayo yanafanyika kwenye ukumbi wa Marijani Hoteli iliyopo eneo la Pwani ya Kichangani, Zanzibar kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 8 Machi, 2022 hadi tarehe 11 Machi, 2022

Mheshimiwa Balozi Katanga ameupongeza uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuandaa mafunzo hayo kwa viongozi hao kwa kuwakutanisha pamoja

“Mmefanya jambo jema leo kwa kuwakutanisha viongozi hawa wenye maarifa, ujuzi na uelewa mbali mbali kwa lengo la kuwaongezea maarifa yao kuhusu ujenzi wa uchumi wa kidijitali,” amesema Mhe. Balozi Katanga

Mhe. Balozi Katanga amesema kuwa suala hili la uchumi wa kidjitali ni mtambuka hivyo amewataka viongozi hao wenye nafasi ya kufanya maamuzi ya masuala ya kisera na kiutendaji ndani ya Serikali kutumia fursa ya mafunzo hayo kujenga uelewa kuhusu mabadiliko haya ya TEHAMA yanaliwezesha taifa letu kukuza uchumi ili kuhakikisha kuwa nchi inanufaika na maendeleo ya TEHAMA hivyo kujenga uchumi wa kidijitali

Ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuchukua jukumu la kuendelea kuwa wazazi kwa kukuza Sekta ya Mawasiliano baina ya Serikali; sekta binafsi na wananchi na kubadilika kwa haraka kuendana na maendeleo ya Sekta hii  ili kuweza kwenda sambamba na mabadiliko haya na kwenda na wakati ili kuipeleka nchi yetu kwenye kiwango cha juu cha  uchumi ili tufikie uchumi wa kidijitali ikiwemo kufungua fursa mpya; kuongeza mapato ya kodi; mifumo ya kiutendaji; upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi; huduma za utalii na kuitangaza nchi kimataifa; kufanikisha ongezeko la huduma za intaneti na upatikanaji wa ajira ili mfumo huu mpya ulete mabadiliko kwenye nchi yetu ikiwa ni pamoja na kuongeza wabobezi wenye ujuzi; kuendeleza na kupanua miundombinu ya kimkakati ya TEHAMA na anwani za makazi ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko.

Ni imani yangu kuwa mafunzo haya yataliwezesha taifa letu kunufaika na kwenda kasi na ukuaji wa TEHAMA duniani ikiwa ni pamoja na kuwa na mtandao wenye kasi kubwa; usalama wa mtandao; kupatikana kwa bidhaa na huduma ambapo maendeleo ya TEHAMA yameondoa mipaka ya upatikanaji na ufikishaji wa huduma kwenye maeneo mbali mbali hivyo Serikali iko tayari kuwezesha mabadaliko haya ili kufanikisha ujenzi wa uchumi wa kidijitali

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa mafunzo haya yatafanyika kwa makundi mbali mbali ili viongozi wengine waweze kupata mafunzo haya na kunufaika nayo kwa kuwa viongozi ndio wanaoshika usukani wa kuendehsa nchi hivyo wakielewa tunaamini wataendesha vema taasisi za Serikali ili kuendana na ukuaji wa uchumi na uchumi wa kidijitali ili wananchi na taifa lilweze kunufaika na maendeleo ya TEHAMA nchini kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambapo Tanzania imeamua kujikita kujenga uchumi wa kisasa wa kidijitali kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambapo mafunzo haya ni hatua ya kujenga msingi imara ili kuwa na Tanzania ya kisasa ili tuweze kujiunganisha na dunia.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa ana amini kuwa baada ya mafunzo haya Serikali itabadilisha kabisa namna ya utendaji kazi kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kukuza,  kuendeleza na kuongeza matumizi ya uchumi wa kidijitali na Serikai itatumia fursa hii ya kidijitali kuhakikisha kuwa sekta mbali mbali zinatumia uchumi wa kidijitali ili kuwezesha muingiliano wa masuala ya TEHAMA katika kunufaisha taifa hili kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ambapo majina ya mitaa/barabara na namba za nyumba zitawawezesha wananchi kunufaika na uchumi wa kidijitali kwa kuwa watatambulika; kufahamika na kupata huduma mahali walipo na kujitambulisha pale walipo hivyo kupitia uchumi wa kidijitali nchi yetu itaenda kufunguka zaidi

“Ni muhimu kwa taasisi zetu kuweka mipango mizuri ili kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zilizopo ili tuweze kuhakikisha kuwa usalama, faragha, ujuzi unapatikana ili wananchi na taifa waweze kunufaika na uchumi huu wa kidijitali na juhudi za kila mmoja zitaleta manufaa kwa taifa letu kwa kuwa dunia tunayoendea ni dunia yenye muungano mkubwa katika TEHAMA hivyo hakuna sekta ambayo haitaguswa, mabadiliko ya kila siku yatatokea na Wizara iko tayari kushirikiana na kila taasisi ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inatumia na kunufaika na fursa zinazojitokeza za TEHAMA,” amesema Dkt. Yonazi

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari Kuwe amesema kuwa mafunzo haya yataiwezesha Serikali kutambua tuko wapi katika nyanja ya ukuaji wa uchumi; tunapotaka kwenda ili TEHAMA iweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu kwa kuwa semina hii imejumuisha viongozi mbalimbali ambao ni watunga sera na wafanya maamuzi ili kuwa na uelewa wa pamoja wa namna bora ya kutumia TEHAMA katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali  kwa kuangalia upya sera zilizopo nchini ili nchi yetu iweze kufika mbali na kwa tija zaidi hivyo TCRA inaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwawezesha wawekezaji kuwekeza nchini ili wananchi wapate huduma bora na za uhakika za mawasiliano ambapo Serikali inaandaa na kuboresha sera, sheria na kanuni ili kuendeleza Sekta hii

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na baadhi ya Mawaziri; Makatibu Wakuu; Wakuu wa taasisi mbali mbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na yanatolewa na wataalam wabobezi wa ndani na nje ya Tanzania.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!