JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tanzania Yang’ara Mashindano Ya Ubunifu Wa TEHAMA Barani Afrika


Tanzania Yang’ara Mashindano Ya Ubunifu Wa TEHAMA Barani Afr...

 

Tanzania imeibuka kidedea katika Mashindano ya Ubunifu Barani Afrika ya Umoja wa Mawasiliano ya Simu wa Afrika (ATU) huku ikizipiku nchi nyingi za Afrika katika ubunifu wa TEHAMA.

Mashindano ya mwaka huu yaliyoongozwa na kauli mbiu isemayo “Mazingira bora yanayochagiza Ubunifu wa TEHAMA kwa vijana” yameshuhudia Tanzania iking’ara kwa washiriki Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Open University of Tanzania) na Chuo Kikuu cha St. Joseph University in Tanzania vikiibuka kinara na kuweka rekodi katika ukanda wa Afrika Mashariki katika mashindano ya mwaka huu ambayo huratibiwa na Jumuiya ya Mawasiliano Afrika (ATU) ikishirikiana na Jumuiya ya Mawasiliano Ulimwenguni (ITU).

Shindano hilo ambalo liliratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania mwezi Julai mwaka huu hufanyika kila mwaka ili kuibua vipaji vya ubunifu katika TEHAMA hasa miongoni mwa vijana katika bara la Afrika.

Ikishika nafasi ya Pili baada ya Tunisia Tanzania imeng’ara kupitia ingizo la ubunifu na ujasiriamali wenye mrengo wa TEHAMA kupitia vituo atamizi vya TEHAMA vya chuo kikuu cha St. Joseph na Chuo Kikuu Huria kupitia kituo atamizi cha Huria Innovation Hub. Tanzania imeingia ndani ya Kumi Bora kwenye mashindano hayo ikizipiku nchi zote za Afrika Mashariki.

Ushindi wa Tanzania kwenye mashindano haya umekuja katika kipindi ambacho serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kujenga Uchumi wa Kidijitali abapo Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa akizungumza mnamo Oktoba 22 kwenye Mkutano wa Tano wa Wataalam wa TEHAMA nchini uliofanyika jijini Arusha alibainisha kuwa serikali imejidhatiti kuwawezesha vijana wabunifu katika TEHAMA kuiwezesha Tanzania kuwa kinara wa TEHAMA Afrika Mashariki na kote barani Afrika.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaimarisha uchumi wa kisasa unaotegemea TEHAMA na ninyi kama wataalam wetu mnayo nafasi ya kutufikisha kwenye uchumi huu” alisisitiza Waziri Mkuu akizungumza na wataalam wa TEHAMA zaidi ya 700 waliokusanyika kwenye kongamano la mwaka jijini Arusha mapema Oktoba 2021.

Katika mashindano ya mwaka huu Tanzania, Tunisia na Zambia zimeibuka kama vinara wa Jumla kwa bara la Afrika katika kuweka mazingira wezeshi kwa ubunifu wa TEHAMA miongoni mwa vijana. Tunisia imeibuka kama mshindi wa jumla ikifuatiwa na Tanzania kisha Zambia. Tanzania imepata nuru kwa kuwawezesha zaidi ya wasichana 34,686 kutatua changamoto katika ujifunzishaji wao kwenye TEHAMA na kuwawezesha wasichana hao kuboresha uwezo wao katika ubunifu na kufanya vema katika masomo ya TEHAMA. Jitihada hizo zimewezesha kuanzishwa kwa biashara 69 kupitia TEHAMA.

Mashindano ya ATU katika Ubunifu wa TEHAMA mwaka huu yalilenga kubainisha taasisi za mafunzo ya TEHAMA barani Afrika ambazo zinawezesha ubunifu katika tasnia hiyo miongoni mwa vijana. Miongoni mwa taasisi zilizobainishwa na ATU kushiriki kwenye mashindano ya mwaka huu ni pamoja na Watunga Sera, Vituo Atamizi vya TEHAMA k.v COSTECH, Vyuo Vikuu na Mashirika yasiyokuwa ya Serikali.

Haya yanajiri wakati serikali ikiwa tayari imeonyesha nia ya kuwashika mkono vijana wabunifu katika TEHAMA ikiwa ni mkakati wa kukuza Uchumi wa Kidijitali; msimamo wa serikali uliobainishwa na Waziri mwenye dhamana na TEHAMA Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji aliebainisha hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Wataalam wa TEHAMA uliofanyika Arusha Oktoba 2021.

"Tunahitaji kuwekeza kwenye utafiti na kuwashika mkono vijana wetu wanaojishughulisha na TEHAMA" alisisitiza Waziri Kijaji.

Katika mashindano ya mwaka huu ATU iliwataka washiriki kueleza jinsi walivyounga mkono ubunifu na walitakiwa kubainisha makundi mawili ya walengwa waliofaidishwa na uungaji mkono bayana ambapo Tanzania iliongoza kwa kutoa washiriki wengi ambapo katika Kumi Bora, Tanzania imeshinda nafasi Tatu ikiwemo ya pili kwenye mnyororo wa washindi, Kenya ilishika nafasi moja na Zambia nafasi moja.  

 

 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!