JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA na Jitihada Katika Kukuza Uchumi wa kidijiti na Bluu Nchini


TCRA na Jitihada Katika Kukuza Uchumi wa kidijiti na Bluu Nc...

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imechukua hatua muhimu katika kuchangia ujenzi wa uchumi wa kidijiti na buluu nchini, ikidhihirisha mafanikio katika kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa sekta ya mawasiliano unaowezesha ushiriki wa wananchi kwenye uchumi wa kidijiti.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tanzania Editors Forum) uliofanyika mjini Lindi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma-TCRA, Bw. Rolf Kibaja, alifafanua kuwa, TCRA imeendelea kuchukua hatua katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, kuendeleza ujuzi wa kidijiti, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kidijiti katika sekta mbalimbali nchini.

Kibaja alisema TCRA imejizatiti kuhakikisha Tanzania inakuwa na miundombinu ya mawasiliano ya kisasa inayowezesha ukuaji wa uchumi wa kidijiti. ikitoa rasilimali masafa kwa intaneti ya kasi ya 4G na 5G ikiwa miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na TCRA katika kufanikisha uimarishaji wa uchumi wa kidijiti.

Kwa upande wa elimu, alisema TCRA inatekeleza programu za kuendeleza ujuzi wa kidijiti, ikiwa ni pamoja na kuandaa kitabu cha kuanzisha na kuratibu klabu za kidijiti katika shule,vyuo na vyuo vikuu. Bw. Kibaja alieleza kuwa klabu hizo zinasaidia wanafunzi kujifunza kuhusu teknolojia za kidijiti na namna ya kuzitumia kwa faida yao, akitoa wito kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya Elimu ya awali hadi vyuo vikuu kujiunga na klabu za kidijiti.

Alibainisha kuwa TCRA inasisitiza kupitia kampeni zake za Elimu kwa umma matumizi ya teknolojia za kidijiti katika sekta za kilimo, utalii, na elimu, ikiamini kuwa teknolojia hizi zina uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.

Katika kutoa wito kwa vyombo vya habari, Kibaja aliwaomba Wahariri kuongeza ushirikiano zaidi katika kueneza taarifa kuhusu uchumi wa kidijiti na buluu.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!