JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA – COMORO KUSHIRIKIANA KWENYE TEHAMA


TCRA – COMORO KUSHIRIKIANA KWENYE TEHAMA

Dar es Salaam,

Mamlaka ya Mawasiliano nchini inatarajia kuingia makubaliano ya ushirikiano kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA) na Wakala wa Maendeleo ya Huduma za Mtandao nchini Comoro (ANADEN). Hayo yamesemwa kwenye ziara ya kubadilishana uzoefu iliyofanywa na Mkurugenzi wa wakala hiyo kwenye ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano tarehe 22/11/2024.

Akiambatana na ujumbe kutoka ANADEN Balozi wa Shirikisho la Visiwa vya Comoro nchini Said Yakub pamoja na Ndugu Said Moinuo Ahamada Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa Maendeleo ya huduma za Mtandao, walisema ni heshima kubwa kwao kuweza kupata fursa ya kujifunza na kuona namna Tanzania kupitia Mamlaka ya Mawasiliano ilivyopiga hatua kubwa kwenye sekta ya Mawasiliano.

Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Mhandisi Felician Mwesigwa aliwapongeza kwa kuchagua Tanzania na TCRA kama sehemu ya kupata uzoefu kwa masuala ya TEHAMA. Wakati akitoa wasilisho juu ya Kazi na Majukumu ya Mamlaka alisema Tanzania inajivunia kwa hatua kubwa iliyofikia kwenye maendeleo ya TEHAMA kwa kuweza kuwa na kituo kikuu cha kitaifa cha Taarifa (Data center).

Mkurugenzi wa ANADEN alisema dhumuni la ziara yao ni kujifunza na kuona namna Comoro inavyoweza kupata wataalamu watakaowezesha kuanzishwa kwa mifumo ya kuhudumia serikali kama vile ilivyo wakala wa Serikali Mtandao, uanzishwaji wa Kikoa cha kitaifa (Domain names) na kuanzisha kituo cha kitaifa cha taarifa (data center) ambayo yatachagiza ukuaji wa matumizi ya mtandao kwenye shuguli za serikali na binafsi.

Alisema Comoro inatarajia kupokea Msaada wa fedha toka Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) ambao wamepanga kutumia kwenye maendeleo ya TEHAMA kupitia ANADEM. Mkurugenzi Ahamada alisema “kupitia fedha hii tunatarajia kufanya maboresho kwenye mifumo yetu ya mtandao kama vile kuongeza uwezo kwa wataalamu wetu na kuboresha uwezo wa mifumo kuwasiliana.

Nae Balozi Yakubu, aliongeza kuwa ni matumaini yao kusaini Hati za Ushirikiano baina ya TCRA na ANADEM ili kuweza kubadilishana wataalamu na uwezo kuiwezesha nchi ya Comoro kupiga hatua kwenye eneo la TEHAMA. “Ni matarajio yetu kikao kijacho wataalamu wenu watakuja Comoro ili waone na kushauri maboresho ya mifumo”

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!