JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yajizatiti Kuboresha Utangazaji


TCRA yajizatiti Kuboresha Utangazaji

Na Mwandishi wetu

USIMAMIZI wa huduma za Utangazaji Tanzania, unaofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), unaendelea kuboreshwa, kuanzia kwenye utoaji wa leseni hadi usimamizi wa maudhui.

TCRA inashirikisha wadau wa utangazaji kwenye masuala mengi ya kisekta. Pamoja na utoaji leseni za huduma za maudhui na kufuatilia masharti ya leseni hizo na kanuni husika, Mamlaka inatoa elimu kuhusu maudhui sahihi na inahamasisha uzingatiaji wa kanuni ili kupunguza matukio ya ukiukwaji.

Umuhimu wa kusimamia maudhui unatokana na upekee wa redio na televisheni kama njia ya mawasiliano kwa umma. Utangazaji ni njia pekee ya mawasiliano inayowafikia watu wengi kwa haraka na wakati huo huo. Maudhui yanawafikia na kusikilizwa au kutazamwa na watu ambao sio lazima wawe wateja wa mtoa huduma.

Vilevile muda wa rejea ya maudhui yanayotolewa na redio na televisheni ni mfupi; yaani maudhui yakishatoka yanaweza kufikia watu wengi hata kama yataondolewa an kusahihishwa.

Kwa kuwa utangazaji unahusisha maudhui ambayo yanaathiri watu kwa namna tofauti, TCRA ina wajibu wa kuwalinda.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt Jabiri Bakari amesema majukumu ya TCRA kuhusiana na maudhui yanahusisha kusimamia kanuni ili watoa huduma wasitoe maudhui ambayo yatadhuru watazamaji au wasikilizaji kwa namna yoyote ile.  

TCRA inasimamia utangazaji kwa kubuni na kuratibu mipango ya kuendeleza sekta ya mawasilianmo, kutoa masafa ya redio na televisheni, kutoa leseni za utangazaji na za uwekaji mitambo inayowezesha utangazaji. Inasimamia na masharti ya leseni zinazotolewa na pia kanuni na miongozo ya utangazaji.

Lengo ni  kuhakikisha weledi na uzingatiaji wa maadili ya utangazaji na pia ubora wa huduma uliowekwa kikanuni.

Takwimu za hali ya mawasiliano Tanzania hadi Aprili 2024 zinaonesha kuwa vituo vya kurusha matangazo ya televisheni vimeongezeka kwa asilimia 4.6, kutoka 65 mwaka 2023 hadi 68 Aprili, 2024. Televisheni za waya zimeongezeka kwa asillimia 5.3; kutoka 57 Aprili 2023 hadi 60 Aprili 2024.  Vituo vya redio vimeongezeka kwa asilimia 7.4, kutoka 215    mwaka 2023 hadi 231 Aprili 2024.

Ukuaji wa kasi umejitokeza kwenye aina mpya ya leseni iliyoanza kutolewa mwaka 2023 – ya Maudhui ya televisheni yanayolipiwa kwa ngazi ya wilaya. Leseni hizi zimeongezeka zaidi ya mara nne ndani ya mwaka mmoja, kutoka mbili (2) mwaka 2023 hadi tisa (9) Machi mwaka huu.

Idadi ya leseni za maudhui ya utangazaji wa redio na televisheni hadi Machi 2024 imeoneshwa kwenye jedwali 1.

Jedwali 1: Hali ya leseni zote zilizotolewa na TCRA hadi Machi 2024

Aina/kundi la leseni

Idadi

Maudhui ya televisheni yasiyolipiwa Kitaifa

16

Maudhui ya televisheni Wilaya

24

Maudhui ya redio Kitaifa

14

Maudhui ya redio Mkoa

31

Maudhui ya redio Wilaya

169

Redio za jamii

17

Maudhui ya televisheni yanayolipiwa Kitaifa

16

Maudhui ya televisheni yanayolipiwa Wilaya

9

Maudhui ya televisheni kwa waya

60

Televisheni mtandaoni

231

Redio mtandaoni

7

Blogu za habari na matukio

67

Usimamizi imara wa TCRA uliiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza Mashariki na Kusini mwa Afrika mwaka 2014, ilipohamia kwenye mfumo wa utangazaji wa televisheni wa kidijitali, kwa mitambo ya ardhini.

Dkt. Bakari alieleza kuwa mfumo wa utangazaji wa televisheni kupitia mitambo ya ardhini umeongeza ubora wa maudhui, ufanisi kwenye matumizi ya masafa nafursa za watazamaji kupata maudhui ya aina tofauti.

Kama ilivyo kwa huduma za mawasiliano ya simu, ambazo zimetoa fursa za ajira kwenye mfumo wote wa utoaji huduma, utangazaji nao umekuza ujasiriamali. Watu wengine wamejiajiri kwenye shughuli zinazohusiana na utoaji maudhui, usambazaji na matengenezo ya vifaa vya utangazaji na mauzo ya ving’amuzi.

Utangazaji wa kidijitali, wa mifumo ya ardhini na setilaiti unahitaji ving’amuzi. Kwa Utangazaji wa mifumo ya ardhini, ambao unajulikana kama DTT, vinatolewa na kampuni zenye leseni ya huduma  zinazowezesha utangazaji.  Vile vile vya mfumo wa setilaiti vinagtolewa na kamouni zenye leseni ya maudhui ya televisheni kwa kulipia.

Ving’amuzi vya televisheni mifumo yote miwili, yaani DTT na DTH, vimeongezeka kwa asilimia 50 kati ya Desemba 2019 na Machi 2024. Hii ni kutoka milioni 2.53 hadi  milioni 3.80.

Kati ya hivyo, vya DTT vimeongezeka kwa asilimia 29, kutoka milioni 1.4 hadi milioni 1.8 kipindi hicho.

Jedwali 2: Idadi ya visimbuzi kwa njia ya ardhini (DTT) na Satelaiti (DTH) kati ya Desemba 2029 na Machi 2024

Aina ya king’amuzi

Mwaka

 

2019

2020

2021

2022

2023

2024

Mfumo wa ardhini  (DTT)

1,432,398

1,472,317

1,613,031

1,667,465

1,781,341

1,801,979

Mfumo wa setilaiti (DTH)

1,092,891

1,341,686

1,577,315

1,702,877

1,880,636

1,950,191

Jumla

2,525,289

2,814,003

3,190,346

3,370.342

3,661,977

3,752,170

Kupitia Kamati ya Maudhui, TCRA imeendelea kushirikisha watoa huduma za maudhui katikat mipango ya kuandaa na kutoa maudhui ya redio na televisheni za kawaida na zile zenye leseni za kuruisha maudhui ya habari na matukio mitandaoni.

Ushirikishaji huu umehusisha kujadili na kutafuta suluhu ya kudumu kuhusiana na ukiukwaji wa kanuni za maudhui, hasa kasoro zilizobainishwa baada ya  utafiti uliofanywa na TCRA mwaka 2021/22 na 2022/2023 kuhusiana na maudhui.

Utafiti huo, kupitia ufuatiliaji wa maudhui ya redio na televisheni na mitandao yenye lesdeni ulionesha kwamba  asilimia 26 ya ukiukwaji ulihusu kutozingatia kanuni za kumlinda mtoto.

Kanuni za utangazaji na za maudhui zinawataka watoa huduma kuepuka maudhui yasiyofaa kwa watoto wakati wa muda wa familia nzima kusikiliza redio au kutazama televisheni; kuzingatia kanuni za utoaji taarifa za watoto wahanga wa uhalifu na namna ya kuwahoji watoto.

Wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka maudhui yanayoweza kuwasumbua au kuwadhuru watoto kisaikolojia.

Asilimia 15 ya ukiukwaji ulihusu kutokuzingatia muda wa kutoa vipindi vinavyofaa kuangaliwa na watu wote

Asilimia 15 nyingine zilikuwa matumizi mabaya ya lugha, kutokuzingatia mizania, kuweka maoni binafsi kwenye maudhui.

Mengine yaliyojitokeza ni taarifa nyingi zimejaa kuhama kutoka kwenye ukweli kwa makusudi, kuongeza chumvi au kuacha baadhi ya taarifa na kupotosha maana. Pia kumekuwa na utoaji taarifa zinazohamasisha uchochezi na vurugu.

Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Bi Saida Mukhi amesema watoa huduma walifikiwa na Kamati hiyo kwa elimu na majadiliano ya kanuni wameongeza kiwango cha uzingatiaji. Hata hivyo bado kuna ukiukwaji kwenye televisheni za mitandaoni; jambo ambalo amesema Kamati inaendelea kulishughulikia..

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!