TCRA Yajidhatiti Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi wa Kidijitali
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeweka bayana mpango wa kuwawezesha vijana wabunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuibua bunifu nyingi zaidi zitakazonufaisha uchumi wa nchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Dkt. Jabiri Bakari wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam.
Dkt. Bakari amesisitiza kuwa mwelekeo wa Uchumi unavutia matumizi makubwa ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kusisitiza kuwa vijana wenye ubunifu katika sekta ya Mawasiliano wanayo nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.
“Tupo kwenye zama za kidijitali; kwa hiyo mawazo na fikra kwa jinsi walivyo hawa vijana ni tofauti na kipindi cha nyuma, vijana wanafikiri na kuona vitu tofauti, kwa hiyo ni lazima tuweze kupata mambo mengi kutoka kwao (vijana)” alisisitiza Kuwe.
Akizungumzia changamoto ya usalama mtandaoni wakati huu Tanzania na dunia ikiwa katika mabadiliko makubwa kwenye sekta ya Mawasiliano Mkurugenzi Mkuu huyo alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mwananchi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanakuja pamoja ili kukomesha vitendo vya uhalifu mtandaoni.
Ili Tanzania iweze kufikia azma ya kuwa na uchumi wa kidijitali usalama wa watumiaji huduma za Mawasiliano kwenye mtandao ni suala ambalo Mamlaka ya Mawasiliano inalitilia mkazo.
Alisisitiza kuwa Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ipo macho wakati wote kuhakikisha inadhibiti uhalifu mtandaoni kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu stahiki juu ya matumizi salama ya huduma za Mawasiliano mtandaoni.
“Mafanikio ni mazuri kwa maana kwamba watu walikuwa wakipata meseji za kitapeli, nataka nichukue muda huu kuwaeleza kwamba serikali iko kazini, Mamlaka na sekta ziko kazini, tunavyozungumza hivi baadhi ya hao matapeli wengi tu wapo kwenye vyombo vya sheria” aliongeza.
Mkurugenzi Mkuu, alisisitiza kumba ni muhimu kwa upande wa wananchi wakashirikiana na mamlaka pamoja na serikali kwa ujumla kwa kutoa taarifa za wahalifu wa mtandaoni kwa kutuma ujumbe na namba za washukiwa wa utapeli kwenda namba 15040 ili kutoa taarifa ya vitendo hivyo kwa shabaha ya kutokomeza vitendo vya uhalifu kwenye mtandao.
Kuhusu zoezi la kuhakiki namba za simu zilizosajiliwa na mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu, Kuwe alisisitiza kuwa ni muhimu kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano akahakikisha anahakiki namba zake zilizosajiliwa kwa kutumia namba za kitambulisho cha Taifa kwa kubofya *106# kisha kufuata maelekezo na hatimae kufuta usajili kwa namba ambazo mtumiaji atabaini kutozitambua; ili kufuta namba za simu ambazo mtumiaji hazitambui atapaswa kufika kwa wakala wa mtoa huduma za Mawasiliano ambae ndie pekee aliepewa haki ya kufuta namba asizozitambua.
Akizungumzia sababu za mtumiaji wa huduma za Mawasiliano kutopewa haki ya kuzifuta namba za simu alizobaini kutozitambua kwenye simu yake; Mkuu wa Kitengo cha Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano cha TCRA Thadayo Ringo alifafanua kuwa hatua ya kutoruhusu mtumiaji kufuta namba asizozitambua inalenga kumlinda mtumiaji kwa kuwa zoezi la kufuta namba hizo linahitaji kuchukua alama ya kidole ili kuthibitisha kwamba anaetaka kufuta namba ambazo hakuzitambua au ambazo asingependa kuendelea kuzimiliki.
Awali Mkurugenzi Mkuu alibainisha kuwa TCRA inaweka mazingira wezeshi kuhakikisha sekta ya Mawasiliano inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.