TCRA yahimiza Kujilinda Mtandaoni kwa Kutumia namba Fupi
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imehimiza Wananchi, nchi nzima kujilinda na matapeli na wahalifu mtandaoni kwa kutumia namba fupi ambazo Mamlaka hiyo imetengeza ili kuripoti matukio ya kihalifu na kujilinda.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt Jabiri Bakari ametanabaisha hayo wakati wa mahojiano maalum jijini Dar Es Salaam jana akisema kwa Taasisi hiyo ipo kwenye jukumu la kueneza elimu kwa watumiaji na umma kuhusu namna bora ya kujilinda na wahalifu wanapo endelea kunufaika na fursa zitokanazo na mitandao.
Dkt. Jabiri amebainisha kwamba Maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na kuenea kwa huduma zilizowezeshwa kwa mifumo ya Kidijiti vimeongeza kasi ya maendeleo na ufanisi katika upatikanaji wa huduma kwahiyo ulinzi kwa watumiaji ni jambo la msingi.
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni msingi mkuu wa mfumo wezeshi kwende sekta zote, ikiwemo huduma za Kiposta na Uasifirishaji wa vifulushio na vipeto, Utangazaji, huduma za simu na intaneti yakiwemo maeneo mengine pamoja na kilimo, utalii, fedha, elimu, matibabu, usafiri na usafirishaji na uchimbaji madini.
TCRA imewakumbusha watumiaji wanaopigiwa simu au kutumiwa meseji zozote zinazoashiria utapeli kutuma namba hiyo ya tapeli kwa ujumbe mfupi (SMS) kwenda namba 15040 BURE ambayo ni ya bure ili namba ya tapeli ifungiwe.
Aidha, amekumbusha kwamba watumiaji wasikubali kutii maelekezo yeyote kutoka kwa mtu aliyewapigia na namba ya simu binafsi na kujitambulisha kuwa ni Mtoa Huduma wa mtandao. Watumiaji wamekumbushwa kuwa namba ya huduma kwa wateja ni 100 pekee.
Watumiaji pia wanakumbushwa kutokujibu ujumbe kwa njia ya simu au barua pepe unaowataarifu kuwa wameshinda bahati nasibu wakati hawajashiriki kwenye mchezo wowote wa aina hiyo. Wanaelekezwa kuufuta.
Kampeni hiyo pia inaeleza namna ya kuhakiki idadi ya laini za simu zilizosajiliwa kibaometria kwa namba ya kitambulisho cha cha taifa cha mtumiaji kwa kubofya *106#, ambapo wanatakiwa kuripoti kwa watoa huduma wao wanapogundua namba wasizozitambua ili zifutwe.
Sekta ya Mawasiliano imepata maendeleo makubwa ambapo takwimu za Desemba 2025 za hali ya mawasiliano Tanzania zinaonesha akaunti za pesa kupitia simu za mkononi zimefikia 76,466,691. Laini zilizotumia huduma za intaneti zilizongezeka kwa asilimia 3.2 kati ya Septemba na Desemba 2025, kutoka 56,322,287 hadi 58,106,264.
TCRA inasisitiza kwamba watumiaji wasitekeleze na wasitoe taarifa zao kabla ya kujidhihirisha kwamba wanaowasiliana nao ni watu sahihi na sio matapeli.
Ripoti ya hali ya mawasiliano Tanzania kufikia Desemba inasema ingawaje matukio na majaribio ya ulaghai yaliyoripotiwa kwenye mitandao ya simu yalipungua, kushuka kwa asilimia 24 kati ya Septemba na Desemba 2025, bado kuna wahalifu wanaondelea na utapeli. Yalipungua kutoka 12,475 hadi 9,450 kipindi hicho.
Kwa ujumla, matukio ya ulaghai yamepungua kwa asilimia 150 kati ya Septemba 2023 na Desemba 2025, kutoka matukio 23,328 hadi 9,450. Hata hivyo, licha ya hali hiyo, mikoa ya Rukwa na Morogoro imeendelea kuongoza kwa matukio mengi zaidi ya ulaghai.