JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yakabidhi vifaa vya TEHAMA Shule ya Sekondari Tumbatu, Zanzibar


TCRA yakabidhi vifaa vya TEHAMA Shule ya Sekondari Tumbatu,...
  • SMZ yabainisha dira, kukuza uchumi wa bluu sambamba na matumizi ya TEHAMA kufikia azma hiyo.
  • Kituo kurahisisha elimu na mawasiliano Tumbatu

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanakuza uchumi wa kisasa unaoendana na falsafa ya uchumi wa kidijitali na uchumi wa bluu.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Amoul Hamil wakati akikabidhi kituo cha Kompyuta kwa Umma (Tele-Center) kwa Skuli ya Sekondari Tumbatu kilichojengwa kwa udhamini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Lengo la ujenzi wa kituo hicho ni kutoa huduma za TEHAMA kwa walimu, wanafunzi na jamii ya kisiwa kidogo cha Tumbatu kilichopo jirani na Unguja.

“Matarajio yetu kama serikali ni kwamba sasa tunakwenda kutekeleza dhamira yetu ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza dira zetu za Maendeleo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na matumizi bora na matumizi mapana ya suala zima la TEHAMA” aliongeza Katibu Mkuu.

Alibainisha kwamba wizara yake itakachofanya ni kuhakikisha inaweka mikakati ya kuhakikisha shule nyingi zaidi na jamii ambazo hazijafikiwa na TEHAMA zinapata huduma hiyo muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa kisasa.

“Niwahakikishie baadhi ya wadau naweza kuwasiliana nao ili kuhakikisha tunakuza TEHAMA kwa manufaa ya jamii zetu,” alisisitiza Katibu Mkuu.

Kituo hicho cha TEHAMA ambacho kimedhaminiwa na TCRA ni kituo cha Sita miongoni mwa vituo vilivyopatiwa miundombinu wezeshi ya TEHAMA chini ya mpango wa mamlaka hiyo. TCRA hutoa fungu la TEHAMA (ICT-pack) kwa lengo la kuhakikisha watu wengi zaidi wanafikiwa na huduma za Mawasiliano hasa maeneo ya pembezoni. Kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 3,000.

Akizungumzia kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA wakati wa makabidhiano ya kituo hicho katika Skuli ya Tumbatu, Mkuu wa TCRA Ofisi ya Zanzibar, Esuvatie Masinga alibainisha kuwa lengo la Mamlaka hiyo ni kuhakikisha huduma za TEHAMA zinakuwa jumuishi na kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini.

“TCRA Ofisi ya Zanzibar katika kutekeleza mpango huu wa kutoa kwa jamii vifaa vya TEHAMA, tumeamua kwa awamu hii kujikita kwenye visiwa ndani ya visiwa kwa upande wa hapa Unguja tuna vituo viwili tumevifungua; hiki ni kituo cha Sita na tuna mpango kwamba mwaka ujao wa fedha tutaomba fedha ili twende kisiwa cha Kojani na maeneo mengine ya Zanzibar lengo likiwa kufikisha huduma za Mawasiliano na TEHAMA kwa jamii kubwa zaidi,” alibainisha Masinga.

Kituo hicho kikiwa ni kituo cha Sita miongoni mwa vingine vilivyofadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kitahudumia shule mbili zilizopo katika kisiwa cha Tumbatu ambacho ni moja miongoni mwa visiwa vikubwa vya Zanzibar sambamba na kuhudumia jamii yote, wanafunzi na walimu.

Wanufaika wa mradi huo wameelezea furaha yao kwa kujengewa kituo cha TEHAMA kwa kuwa kitarahisisha upatikanaji wa huduma za elimu na kuwawezesha wananchi wa Tumbatu kuwasiliana kwa urahisi na kuendana na ukuaji wa TEHAMA.

Akiwasilisha salamu za wakazi wa Tumbatu na Menejimenti ya Shule, Mkuu wa shule hiyo alieleza kuwa kituo hicho si tu kitasaidia ujifunzishaji miongoni mwa wanafunzi lakini pia kitawezesha upatikanaji wa huduma za TEHAMA miongoni mwa wanafunzi wa shule mbili za sekondari zilizopo kwenye kisiwa hicho. 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!