JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yatoa Mafunzo ya Tahadhari na Kinga dhidi ya Majanga ya Moto


TCRA yatoa Mafunzo ya Tahadhari na Kinga dhidi ya Majanga ya...

Na Jasmine Kiyungi 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mafunzo ya kujilinda na kuchukua tahadhari juu ya majanga ya moto. 

Mafunzo yametolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoji kupitia Sajenti Hassan Amani na kuhudhuriwa na Watumishi wa ndani pamoja na watumishi wa nje ikiwemo wafanyakazi wa Benki ya Azania, wafanyakazi za usafi, Maaskari wa Ulinzi na wafanyanyakazi wa hotelini. 

Baadhi ya Watumishi wa TCRA ikiwemo Bw. Edward Nchimbi na Bi. Aziza Charira wamesema kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga juu ya kuweza kuchukua tahadhari kuhusu majanga ya moto sio tu hapo ofisini katika jengo la TCRA lakini pia hata majumbani ambapo mara nyingi hatari ya moto hutokea na huwa wanashindwa kutoa msaada. 

Nae Mfanyakazi wa Usafi katika jengo la Mamlaka ya Mawasiliano kutoka kampuni ya Feeof Investiment Limited Bi. Hadija Mohamed Said amesema kuwa, amepokea mafunzo hayo kwa ukubwa mno kwa kuwa amepata elimu ambayo imempatia mbinu za kawaida mno, ambazo zinaweza kufanyika bila shida wala ugumu wowote na kuweza kusaidia kuepusha madhara makubwa. 

Pia aliongeza kuwa ana hakika madhara makubwa yasingekuwa yakitokea kila moto ulipokuwa unatokea kama watu wangekuwa na maarifa hayo muhimu yaliyotolewa. Bi Hadija alitaja mbinu alizozipata katika mafunzo hayo ambazo ni kufunika blanketi lenye maji kwenye sehemu inayoanza kuungua, kufunika sehemu inayotaka kuungua na kitu kitakachozuia hewa kuingia katika eneo linalowaka moto ili kuzuia uchochezi wa moto huo, pamoja na kutumia vizimamoto sahihi kutokana na aina ya moto uliojitokeza. 

Mtumishi wa hoteli katika jengo la Mamlaka anayetambulika kwa jina la Mohamed Kitole hakubaki nyuma, Mtumishi huyo ambaye ni Kiongozi wa Kampuni ya chakula 

iitwayo Aikama Catering Services iliyopo katika jengo hilo alisema kuwa, mara nyingi katika kazi zao huwa wanakutana na hatari za kutaka kutokea kwa moto kutokana na kuwa na vifaa vingi vyenye kuzalisha moto ikiwemo majiko ya umeme na gesi. 

Mtumishi huyu aliongeza kuwa tangu apate mafunzo hayo amekuwa na imani na kazi yake sasa, kwa kuwa amepata mbinu za kuzuia kutokutokea kwa ulipukaji wa moto ikiwemo kuwa makini na mwangalifu, kuacha uzembe, na kuchukua hatua mapema na haraka mara tu hitilafu inapotokea. 

Mtoa mafunzo kutoka jeshi la zimamoto na uokoaji Sajenti Hassan Amani , anaipongeza TCRA kwa kuja na mkakati huo madhubuti wa kutoa mafunzo haya kwa watumishi mbalimbali waliopo katika jengo la Mamlaka ya Mawasiliano. Na anaamini hapo hajatoa elimu kwa watumishi hao tu bali anaamini elimu hiyo itafika hadi majumbani kwa watumishi hao na itasaidia kufanya watu kujikinga na majanga ya moto. 

TCRA kupitia uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Jabiri Bakari inathamini usalama wa watumishi wake . Hivyo itaendelea kutoa mafunzo mbali mbali yanayolenga kuleta ulinzi na usalama wa afya za watumishi wa Mamlaka ya Mawasiliano. 

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!