Chuo cha Maafisa Wakuu wa Jeshi Uganda (SCSC) Chatembelea TCRA Kujifunza Usalama wa Mtandao
Ili kuongeza maarifa na ujuzi kuhusu usalama wa mtandao na TEHAMA kwenye majeshi ya ulinzi katika nchi za Afrika Mashariki, Chuo cha maafisa wakuu wa Jeshi Uganda (SCSC) kikiongozwa na Meja Jenerali George Igumba, kilifanya ziara ya mafunzo katika makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam wiki hii.
Ujumbe huo uliohusisha maafisa wakuu wa mafunzo na wanafunzi kutoka Chuo cha Maafisa Wakuu wa Jeshi Uganda, ulijumuisha maafisa wa ngazi ya juu kutoka nchi kadhaa akiwemo Brigedia Jenerali Bhupendra Singh Fogat , kiongozi wa taasisi ya mafunzo ya kijeshi ya India.Aidha ujumbe huo ulikua na wanajeshi kutoka Kenya, Rwanda, India, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Afrika Kusini na Malawi mpango ambao uliwezeshwa kwa mwaliko wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania chini ya uratibu wa kanali Robert John Mbuba.
Walipowasili katika makao makuu ya TCRA jijini Dar es Salaam, ujumbe huo wa Kijeshi ulipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari.Ziara hiyo ilijumuisha mawasilisho mbalimbali kuhusu sekta ya mawasiliano, kutembelea makumbusho ya mawasiliano, huku ikijenga uelewa wa sekta ya mawasiliano, ulinzi wa anga la mtandao na majukumu ya Mamlaka za usimamizi.
Meja Jenerali George Igumba aliishukuru TCRA kwa fursa ya kuelewa kwa kina masuala muhimu ya usimamizi wa mawasiliano. "Tunashukuru sana kwa TCRA kutupatia fursa hii ya kujifunza, na tunaamini wanafunzi wetu wamepata ufahamu muhimu wa sekta ya mawasiliano," alisema, alisistiza kuhusu umuhimu wa kubadilishana uzoefu,ujuzi na kujenga uwezo wa wanajeshi katika enzi ya maendeleo ya haraka ya teknolojia hususani katika teknolojia ya habari na mawasiliano.
Maafisa hao pia walishuhudia mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano kupitia makumbusho ya mawasiliano yanayosimamiwa na TCRA.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma TCRA, Rolf Kibaja, alisisitiza umuhimu wa makumbusho kuwa ni rasilimali ya elimu ya kipekee inayohifadhiwa na TCRA. Mbali na ziara ya maafisa wa kijeshi, Kibaja alitumia fursa hiyo kuwakaribisha na kuwahimiza wadau mbalimbali, ikiwemo wanafunzi kutembelea makumbusho ya mawasiliano.
"Kuingia katika makumbusho ni bure, tumejidhatiti kuhakikisha watu weni zaidi wanapata ufahamu wa teknolojia za mawasiliano, hivyo wadau wote hasa wanafunzi wanakaribishwa katika makumbusho yetu ya mawasiliano kwa ajili ya kujifunza," alisisitiza.
Ziara ya mafunzo, iliyoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuongozwa na Kanali Mbuba, ni ziara ya ushirikiano iliyolenga kukuza, kubadilishana maarifa na kuimarisha uwezo wa kiteknolojia wa vikosi vya kijeshi. Hatua hii inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa yanayoshiriki na kurahisisha kubadilishana uzoefu na ujuzi katika tasnia ya ulinzi.