Ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Jabiri K. Bakari katika Kuadhimisha Siku ya Mawasiliano na Jamii ya Habari Duniani
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inajumuika na wadau wengine duniani kuadhimisha siku ya Mawasiliano na Jamii Ya Habari Duniani (World Telecommunication and Information Society Day - WTISD) katika siku hii ya tarehe 17 Mei 2024. Maadhimisho haya yanayofanyika kila mwaka siku ya tarehe 17 Mei ni sehemu ya kumbukumbu ya siku ya kusainiwa mkataba ulioasisi Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Mawasiliano (ITU). ITU ilianzishwa kuwezesha mataifa kuunganishwa katika mitandao ya mawasiliano na kusimamia mgawanyo wa masafa ya redio kimataifa na obiti za setilaiti. Majukumu mengine ni kuendeleza viwango vya kiufundi vinavyohakikisha mitandao na teknolojia inaunganishwa bila vikwazo, na kuboresha kupatikana na kuchukuliwa kwa matumizi kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa jamii ambazo hazihudumiwi ipasavyo katika maeneo yote ulimwenguni. TCRA kama msimamizi wa Sekta ya Mawasiliano/TEHAMA nchini inajivunia kuwa sehemu ya kufanikisha malengo ya kuasisiwa kwa ITU.
Kaulimbiu ya mwaka huu – "Ubunifu wa Kidijiti kwa Maendeleo Endelevu" ni kauli mbiu inayolenga kuwa na mustakabali jumuishi na endelevu katika uchumi wa kidijiti kupitia ubunifu. Ubunifu wa kidijiti ni nguzo muhimu kwenye uchumi wa kidijiti ili kuendana na maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya kimataifa. Katika mazingira ya kisasa ya kidijitali yanayobadilika kwa kasi, ubunifu huwezesha kuzitambua fursa zilizopo na kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kutoa majawabu yenye tija kupitia TEHAMA.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni wito wa kuwepo jitihada za maksudi za kuweka mazingira ya kuchagiza ubunifu wa kidijiti nchini kuendana na kasi ya maendeleo ya Dunia ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN Sustainable Development Goals) ifikapo mwaka 2030.
Kwa kutambua umuhimu wa Ubunifu, TCRA kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inaunga mkono kazi za ubunifu wa kiteknolojia kwa kutoa rasilimali za mawasiliano kama vile rasilimali za namba, masafa, na Kikoa cha Dot tz bure kwa wabunifu mbalimbali (start-ups) ambao wanahitaji kujaribu huduma zao za kibunifu kwa kipindi cha miezi mitatu (siku 90) ili kuwawezesha na kuinua mawazo ya bunifu mbalimbali. Kwa mfano TCRA imetenga rasilimali namba *146*XX ambayo inatolewa bure kwa majaribio ya wabunifu. TCRA inaendelea kuangalia na kuunda mazingira yanayoweza kusaidia zaidi mzunguko wa maisha ya start-ups kuelekea kuwa biashara huru zenye mafanikio.
Aidha, katika kuweka mazingira ya ubunifu kwa wanafunzi TCRA, inaratibu klabu za kidijiti kuanzia shule za awali, za msingi, sekondari , vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini zenye lengo la kuhimiza wanafunzi kujifunza na kuyapenda masomo ya STEM (sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati) ambayo yana umuhimu mkubwa katika kukuza ujuzi wa uchumi wa kidijiti unaohitajika ili kufanikiwa kujengaTanzania ya kidijiti.
Vile vile TCRA inashirikiana na Watoa Huduma katika kuwawezesha wabunifu kufanikisha bunifu zao kupitia mifumo ya TEHAMA(platforms).
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inatambua mchango wa watoa huduma na wadau wote wa Sekta ya mawasiliano na hivyo inahimiza kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya mawasiliano na TEHAMA na kutoa huduma mbalimbali za TEHAMA ili kuiwezesha nchi kuwa na miundombinu na mazingira imara ya mawasiliano yenye kuwezesha mabadiliko ya kidijiti na kuchochea ubunifu nchini.
Nawatakia Watanzania wote, Wadau wa Sekta ya Mawasiliano na jamii ya Habari na Mataifa Wanachama wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), siku ya Mawasiliano na Jamii Ya Habari Duniani (WTISD) yenye kumbukumbu nzuri kwa mwaka wa 2024.