JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wabunge wa Uganda Watembelea TCRA kwa Mafunzo


Wabunge wa Uganda Watembelea TCRA kwa Mafunzo

Kamati ya Bunge ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na Miongozo ya Kitaifa kutoka Uganda, ikishirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda (NITA-U), imetembelea Ofisi Kuu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Lengo la ziara hiyo lilikuwa kujifunza jinsi Tanzania inavyosimamia sekta ya mawasiliano, ikihusisha mawasiliano ya simu, intaneti, utangazaji, na huduma za posta.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Tony Ayoo (Mb), wajumbe wa kamati walipata fursa ya kuelewa jinsi TCRA inavyohudumia wadau mbalimbali katika sekta ya mawasiliano, ikiwemo wamiliki wa leseni, watumiaji wa huduma za mawasiliano, na wadau wa sekta ya umma.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, John Daffa, aliwakaribisha wabunge hao na kuwapitisha katika maelezo kuhusu majukumu ya TCRA na mchango wake katika kusimamia mawasiliano. 

 “Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba huduma zote zinazohusu mawasiliano, zilizo ndani ya ikolojia ya teknolojia ya habari na mawasiliano, zinasimamiwa kwa ufanisi ili zichangie maendeleo ya nchi yetu” alifafanua Daffa.

Kamati hiyo pia ilijifunza kuhusu namna TCRA inavyotekeleza majukumu yake ya kusimamia rasilimali muhimu za mawasiliano kama vile masafa ya mawasiliano, nambari za mawasiliano, kikoa cha taifa cha .tz, kanzidata ya anwani na postikodi.

Vilevile, walijifunza kuhusu uboreshaji wa utoaji wa leseni za mawasiliano, ambazo sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia jukwaa la Tanzanite, hivyo kuondoa ulazima wa waombaji kufika ofisini.

“Tumeweka mfumo wa utoaji leseni mtandaoni, unaorahisisha upatikanaji wa leseni kwa waombaji wapya na kupunguza changamoto za ufuatiliaji wa leseni kwa wawekezaji, maboresho haya yameleta ufanisi mkubwa katika usimamizi wa mawasiliano hapa nchini” alieleza.

Kuhusu upatikanaji wa teknolojia ya mawasiliano, Daffa alifafanua kwamba TCRA inahakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano ya kasi na zenye ubora.

Alitaja upatikanaji wa teknolojia ya mawasiliano ya simu kufikia asilimia 98 kwa 2G, 86% kwa 3G, 79% kwa 4G, na 10% kwa teknolojia ya 5G.

Wajumbe wa kamati hiyo kutoka Uganda walitoa pongezi kwa TCRA na Tanzania wakiuliza maswali baada ya wasilisha wakilenga kujifunza zaidi kuhusu usimamizi wa masafa ya utangazaji wa redio, usimamizi wa kikoa cha taifa cha .tz, utangazaji wa redio kidijitali, na jinsi Tanzania inavyowezesha vijana kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Akijibu hoja za waheshimiwa wabunge hao, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA alieleza kuwa TCRA imeanzisha mfumo wa kiusimamizi unaoimarisha usimamizi wa sekta za simu, intaneti, utangazaji na posta. Kuhusu utangazaji wa redio kidijitali, alibainisha kuwa TCRA inaandaa muongozo utakaowezesha Tanzania kuanza kutumia teknolojia ya Digital Sound Broadcasting.

Ziara hii ya siku tatu, iliyolenga kujifunza kuhusu miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!