JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

SIKU YA POSTA DUNIANI, 9 OKTOBA 2024 - UJUMBE WA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA (TCRA), DK. JABIRI K. BAKARI KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA POSTA DUNIANI, TAREHE 9 OKTOBA 2024


SIKU YA POSTA  DUNIANI, 9 OKTOBA 2024 - UJUMBE WA MKURUGENZI...

LEO tarehe 9 Oktoba, 2024 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Posta Duniani. Mwaka huu ni wa 150 tangu kuanzishwa Umoja wa Posta Duniani (UPU) mwaka 1874. Tangu kuanzishwa kwa Umoja huo, huduma za posta zimebadilika kutoka kwa njia rahisi za mawasiliano ya barua hadi kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za mawasiliano duniani.

Kaulimbiu ya Siku ya Posta Duniani mwaka huu ni: " Miaka 150 ya kuwezesha mawasiliano ya posta katika kuboresha maisha ya watu duniani".   Inasisitiza umuhimu wa huduma za posta kama kichocheo cha uwezeshaji wa maendeleo kijamii na kiuchumi duniani. Kaulimbiu hii pia inasisitiza jukumu la huduma ya posta, ambalo ni kuwezesha mawasiliano na kuiwezesha jamii.

Mawasiliano ni uhai wa jamii zetu; na huduma za posta zimekuwa  muhimu katika kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa na kuwa kichocheo katika shuguli za kiuchumi na kijamii. Hivyo, sekta ya posta inaunganisha watu, biashara na jumuia mbalimbali, na  bila kujali vikwazo vya kijiografia, inawaleta watu pamoja.

Utekelezaji wa jukumu la kuwawezesha watu kutumia huduma za posta husaidia maendeleo ya kiuchumi, hukuza fursa za elimu, hurahisisha mawasiliano, huimarisha uhusiano wa kijamii, na pia hukuza ushirikishwaji wa kidijiti na kifedha kwa Watanzania wote bila kujali maeneo ya walipo.

Zaidi ya hayo, huduma za posta zimekuwa uti wa mgongo wa mawasiliano na biashara mtandao. Huduma za posta zinasaidia si tu mawasiliano ya kibinafsi bali pia hufanikisha kubadilishana habari muhimu na shughuli za biashara.

Katika maeneo ya vijijini na ambayo hayana mvuto wa kibiashara, huduma za posta zinakuwa kiungo muhimu za kuwezesha huduma kufikia watu wengi zaidi. Zinasaidia mawasiliano na ushirikiano  kijamii na kiuchumi.

Kwa kusimamia huduma za Posta, serikali inahakikisha kuwa huduma, ambazo ni mhimili wa maendeleo kijamii na kiuchumi, zinatolewa kwa wakati na kwa uhakika.

TCRA, kama msimamizi wa mawasiliano katika sekta hii muhimu, inatekeleza kwa  uadilifu wajibu wa kuhamasisha jitihada za kuunganisha jamii, kutoa huduma za msingi, na kuwezesha mawasiliano ya sekta ya posta ambayo yanasaidia biashara, biashara-mtandao na kubadilishana bidhaa za kitamaduni na  nchi nyingine.

Ahadi ya TCRA daima imekuwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za posta, kuwepo kwa gharama nafuu, na ufanisi  unaowezesha upatikanaji wa huduma za msingi za posta na huduma za vifurushi na vipeto.

Miaka 150 iliyopita tumeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta ya posta, mabadiliko kutoka utumaji wa barua binafsi hadi huduma za kidijiti zinazotumia teknolojia za kisasa. Katika muktadha huu, TCRA inatambua jukumu muhimu la ubunifu wa kidijitali katika kutengeneza mustakabali ujao wa sekta ya posta.

Mfumo wetu wa usimamizi umeundwa ili kukuza na kusaidia mabadiliko katika sekta ya posta, kuhakikisha manufaa ya maendeleo ya kidijitali yanawafikia watu wote. Kazi kubwa imefanyika kuunganisha teknolojia za kisasa na ya zamani, kama vile mifumo ya kidijiti na mifumo inayojiendesha  yenyewe ambayo hurahisisha utendaji na kuboresha upatikanaji wa huduma za  posta.

 Hivyo, Ubunifu wa kiteknolojia  unatarajiwa kupanua na kusaidia mawasiliano ya sekta ya posta kuvuka mipaka ya nchi na pia kuwezesha watu kutoka mataifa mbalimbali kuunganishwa na kufanya biashara kwa urahisi.

Mtandao wa posta una jukumu kubwa katika kusafirisha bidhaa muhimu, kuwezesha biashara-mtandao, na kusaidia jamii na biashara kustawi katika ulimwengu huu wa utandawazi. Ili kuunga mkono jambo hili, Serikali kupitia TCRA, inaendelea kuunganisha na kukuza uchumi na kuimarisha mahusiano ya jamii nchini.

TCRA imejizatiti kuwasaidia wadau wa posta kwa kuweka viwango vya utoaji huduma  na usalama wa huduma, kukuza ubunifu, kuweka kipaumbele cha maendeleo na kulinda maslahi ya umma.

Usimamizi wa sekta ya posta una manufaa mengi, ikiwemo ufuatiliaji wa mienendo ya soko, utoaji elimu ya kutosafirisha bidhaa hatarishi na kuongeza uelewa wa kina wa jinsi ushindani unavyoweza kuboresha uchumi wa taifa.

Sekta ya posta imebadilika kwa haraka. Katika enzi hizi mpya za maendeleo ya teknolojia, TCRA inaimarisha mifumo ya ufuatiliaji mwenendo wa bidhaa za posta kidijitali ambao utaboresha uwazi, na kuruhusu wateja kufuatilia maendeleo ya bidhaa za posta kwa wakati. 

Utunzaji wa mazingira endelevu unazidi kuwa muhimu. Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa  huduma za posta zinatunza mazingira. Hii ni pamoja na matumizi ya  magari yasiyochafua mazingira na vifungashia vilivyo rafiki kwa mazingira. TCRA inaendelea kuhimiza utoaji huduma rafiki wa mazingira ili kuelekeza sekta hii katika mustakabali endelevu zaidi.

Pamoja na hilo, utandawazi unahitaji ushirikiano katika mipaka ya nchi na ubunifu katika utoaji wa huduma za posta. Kupitia kanuni za UPU na makubaliano kati ya nchi husika kunaweza kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na  ubadilishanaji wa barua na vifurushi vya kimataifa. Kwa kuhimiza uvumbuzi wa kushirikiana kunaweza kuleta suluhu za pamoja za changamoto zinazofanana,  na pia kujenga mtandao wa sekta ya posta wa kimataifa ambao  una ustahimilivu zaidi.

TCRA inaendelea kusimamia sekta ya Posta kwa kutoa leseni na pia  kuhakikisha viwango vya huduma kwa wateja vinaboreshwa. Inatarajiwa kuwa watumiaji wa huduma za Posta wataendelea kunufaika na uwepo wa huduma mbalimbali zenye ubunifu na zinazokidhi mahitaji yao.

TCRA inawahimiza watumiaji wa huduma za kiposta kuendelea kupata  huduma zao zinazoaminika kutoka kwa watoa huduma wenye leseni.

Chini ya mfumo wa TCRA wa utoaji leseni sekta ya Posta, kuna mtoa huduma mmoja wa Posta wa Umma – Shirika la Posta Tanzania (TPC), kwa  utoaji wa huduma za posta kwa wote, zikiwemo huduma nyingine za usafirishaji wa vifurushi.

Kufikia tarehe 11 Septemba 2024, TCRA imetoa jumla ya leseni 146 katika sekta ya posta kwenye aina, makundi na masoko mbalimbali.  Aidha, leseni moja moja (1)  imetolewa kwa TPC, ambaye ni mtoa huduma za Posta wa umma.

Huduma za usafirishaji vifurushi zimetolewa kwa makundi yafuatayo na idadi kwenye mabano: watoa huduma za kimataifa (6), watoa huduma ndani ya Afrika ya Mashariki (2) na  watoa huduma ndani ya mipaka ya Tanzania (47). Nyingine ni watoa huduma ndani ya mji mmoja (16) na wasafirishaji vifurushi  kati ya miji miwili (74).

TCRA inaendelea kusimamia sekta ya posta ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na kuwawezesha waendeshaji na watoaji wa huduma za kiposta kuhudumia umma kwa gharama nafuu, salama, na kwa viwango vya juu vya ubora.

Tunapoadhimisha miaka 150 ya huduma ya Posta duniani, tunaamini kuwa sekta ya Posta Tanzania itaendelea kuimarika. Vilevile, tutahakikisha kwamba sekta hiyo inachukua nafasi muhimu katika kuwawezesha na kuwaunganisha Watanzania kijamii na kiuchumi ndani ya nchi na kimataifa kwa miaka mingi ijayo.

Tuungane na kwa pamoja tuadhimishe siku hii ya Posta Duniani!

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!