Ada za Idhini ya Vifaa zinaweza kupatikana ukurasa wa 11 wa mwongozo wa Idhini ya vifaa ambao uko kwenye https://otas.tcra.go.tz/downloads/Type_Approval_Guidelines.pdf.
Idhini ya vifaa inahitajika kwa antena ambazo zinaweza kuwashwa kielektroniki. Idhini ya Vifaa haihitajiki kwa antena ambazo haziwashwi.
Vifaa vinavyopokea tu mawimbi vinahitaji Idhini; kwa mfano vifaa vya kufuatilia mwenendo na mahali na vifaa vya kupokea mawimbi ya utangazaji
Cheti cha Idhini ya Kifaa hakiwezi kutolewa kwa aina nyingi za kifaa. Cheti hicho kinatolewa kwa msingi wa kila aina ya kifaa.
Cheti cha Idhini ya Vifaa kinachukuliwa kwamba wakati wote hakijamaliza muda wake iwapo hakuna mabadiliko yatakayofanywa kwenye kifaa kilichoidinishwa. Kifaa kinaidhinishwa mara moja tu lakini mtengenezaji au msambazaji anatakiwa kuitaarifu Mamlaka pale yanapotokea mabadiliko yanayoweza kuleta utofauti wa taarifa zilizohifadhiwa kwenye kanzidata ya Idhini ya Vifaa
Inachukua muda usiozidi siku 14 za kazi kutoa Cheti cha Idhini ya Vifaa kuanzia siku mwombaji atakapowasilisha nyaraka zote zinazohitajika na kama hapatakuwa na ucheleweshaji wa malipo na kuwasilisha sampuni ya kifaa husika (pale ambapo sampuni inahitajika kwa mujibu wa utaratibu wa maombi).
Muombaji wa Idhini ya Vifaa vya Mawasiliano ya Kielektroniki atawasilisha maombi yake kupitia mfumo wa mtandaoni wa maombi ya idhini ya vifaa, yaani OTAS, kifupisho cha Online Type Approval System ambao unapatikana kwenye https://otas.tcra.go.tz, ambamo mwombaji anaweza pia kupata taarifa za ziada.
Idhini ya vifaa inatakiwa ipatikane kabla kifaa husika hakijaingia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Watengenezaji wa vifaa na wawakilishi wao, kampuni za ndani na nje ya nchi zilizoidhinishwa, waagizaji au wasambazaji wa ndani wanaweza kuomba idhini kwa aina mpya ya vifaa vya mawasiliano vinavyokusudiwa kutumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa ujumla, Idhini ya Vifaa inatakiwa kwa vifaa vyote vya mawasiliano ya kielektroniki (vinavyotumia waya na visivyotumia waya) kabla ya kuingia soko la Tanzania. Mifano ya vifaa vinavyohitaji kuidhinishwa ni:
a) Vifaa vinavyotumiwa na wanaopata huduma za mawasiliano ya kielektroniki kama vile simu za mkononi, vishkwambi, simu za kawida, simu zisizo na waya, mod, redio za mawasiliano zinazotumia masafa ya VHF/UHF, Vifaa visivyotumia waya, kompyuta mpakato, skana, mashine ya faksi,vifaa vinavyoweza kusafirisha umbali mrefu taarifa zilizohifadhiwa kwenye kompyuta, ikiwa ni pamoja na vinavyowezesha kufuatilia na kutambua mwelekeo na mahali (GPS tracking devices), vifaa vya mawasiliano ya karibu, vifaa vinavyowasiliana kati yao kupitia intaneti na vifaa vya mawasiliano vyenye uweo mkubwa.
b) Vifaa vya mawasiliano ofisini kama vile mifumo inayosimamia usambazaji wa simu za ndani (PABX).
c) Vifaa vya mawasiliano mtandaoni kama vile vifaa vya swichi, vifaa kwenye minara ya mawasiliano, vifaa vya kuunganisha watumiaji wa intaneti, kompyuta za uwezo mkubwa zinazohifadhi taarifa na vifaa vya kusambaza mawasiliano.
d) Vifaa vya utangazaji kama vile transmita, vifaa vya mawasiliano kati ya studio na transmita, televisheni zenye uwezo mkubwa, visimbuzi, redio za kidijitali na amplifaya
Lengo la uidhinishaji wa vifaa ni kuhakikisha kwamba vifaa vyote vya mawasiliano ya kielektroniki vinakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Vilevile, ni kuzuia madhara yoyote au athari zozote za kiafya kwa watumiaji, kuhakikisha usalama wa watumiaji na mazingira, kuzuia uwezekano wa vifaa hivyo kuingilia na kuharibu mitandao ya mawasiliano ya simu na kuimarisha ubora wa huduma za mawasiliano
Uidhinishaji wa Vifaa ni njia ya kuhakiki utengamano na muingiliano wa vifaa vyote vya mawasiliano ya kielektroniki na mtandao wowote wa mawasiliano ya kielektroniki na iwapo vinakidhi viwango.



